Elimu ukusanyaji taka hatarishi ni muhimu

Imepakiwa - Wednesday, March 27  2019 at  09:00

 

Ofisi ya Makamu wa Rais imewataka wakusanyaji taka hatarishi ikiwamo vyuma chakavu, betri zilizotumika na taka za kielektroniki kupeleka leseni zao kuhakikiwa ifikapo Aprili 2, vinginevyo zitafutwa.

Kwa mujibu wa wito huo, watu wanaojishughulisha na kazi hiyo wametakiwa kuwasilisha leseni halisi katika ofisi za Kanda za Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) ambako zitahakikiwa.

Tunaipongeza ofisi ya Makamu wa Rais kwa wito wake huu tukiamini kwamba umekuja katika kipindi muafaka ambacho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali katika suala la ukusanyaji, usafirishaji na utunzaji wa taka hatarishi.

Hatua hizo tatu zimekuwa zikisababisha matatizo ya aina mbalimbali katika udhibiti wa taka hatarishi ikiwamo milipuko, usafirishaji wake na hata utunzaji wa vitu ambavyo ni hatari kwa maisha ya binadamu na mali zao.

Ipo mifano kadhaa inayohusiana na taka hatarishi zilivyowahi kusababisha madhara kwa binadmu ikiwamo watoto kulipukiwa na bomu baada ya kuliokota kwa ajili ya kwenda kuliuza kama chuma chakavu na pia usafirishaji wa betri chakavu zenye kemikali ndani yake zilivyoathiri ngozi za wahusika.

Si hivyo tu, lakini vilevile lipo suala la utunzaji. Hili nalo ni changamoto kwa sababu kuna wakati taka za aina mbalimbali zinawekwa pamoja katika eneo moja bila kujali athari au hatari ya kila moja ikiwa ni pamoja na msuguano unapotokea.

Upo ushahidi kwamba msuguano au uwapo wa joto kali katika eneo fulani na kuwapo kwa vitu vilivyoundwa au kutengenezwa kwa kemikali, vinaweza kusababisha milipuko au athari za maisha au mazingira.

Athari hizo ni pamoja na afya za watu wanaohusika na ukusanyaji, usafirishaji na utunzaji.

Hayo ni miongoni mwa mambo muhimu ya kuzingatiwa wakati wote wa kushughulika na taka hatarishi ambazo kitendo cha kuitwa hivyo maana yake ni kuwa ni vitu ambavyo vimepoteza uhalisia, hivyo ni rahisi kusababisha athari.

Kutokana na hali hiyo tunaiomba Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ianze kutoa elimu ya namna ya kushughulika na taka hizo katika hatua hizo tatu – za ukusanyaji, usafirishaji na utunzaji wake.

Ni kutokana na umuhimu wa kufanya hivyo, maisha ya watu na mali zao yatakuwa kipaumbele cha kwanza cha wale wanaoshughulika na taka chakavu.

Aidha, katika utoaji wa elimu, mathalan ya ukusanyaji taka, Serikali ianzishe programu maalumu ya kuifundisha jamii namna ya kushughulika na vyuma chakavu, betri mbovu na taka za aina mbalimbali ikiwamo zile zenye kemikali.

Katika utoaji wa elimu hiyo ielezwe ni namna gani mtu anatakiwa kuzigusa taka zenye kemikali, kuzihifadhi na au kuzisafirisha bila kumsababishia athari za kiafya, pia mfumo mzuri wa usafirishaji taka za aina tofauti ili zisilete madhara kwa jamii na mazingira.

Yapo mambo mengi ambayo wakusanyaji wa taka hizo wanapaswa kuyazingatia ambayo yawezekana hawayajui au wanayajua lakini hawayatekelezi.

Katika hili, sheria inaweza kuwa msaada wa kuelekeza na kuadhibu, lakini iwe ni baada ya watu hao kuwa wameelimishwa. Tunaamini kwamba jamii ikipatiwa elimu inayostahili, suala la ukusanyaji, usafirishaji na uhifadhi wa taka hatarishi halitaleta madhara makubwa katika jamii au mazingira katika siku za usoni.