http://www.swahilihub.com/image/view/-/4532650/medRes/1954602/-/4mvdyyz/-/mali.jpg

 

Emmanuel Macron: Rais wa Ufaransa aliyechaguliwa akiwa na umri wa miaka 39

Emmanuel Macron

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ahutubu katika kongamano la siku mbili la kutafuta ufumbuzi wa jinsi ya kuzima ufadhili wa makundi ya kigaidi lililoandaliwa Aprili 26, 2018, jijini Paris. Picha/AFP 

Na SAMMY WAWERU na KABRASHA LA HISTORIA

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  14:20

Kwa Muhtasari

Rais Emmanuel Jean-Michel Frederic Macron wa Ufaransa aliingia katika Ikulu ya Élysée mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 39.

 

EMMANUEL Jean-Michel Frederic Macron ndiye Rais wa nchi ya Ufaransa, na alikwea katika wadhifa huo mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 39.

Kuwa Rais na umri huo, alinakiliwa katika mabuku ya historia ya Ufaransa kuwa kiongozi wa taifa aliyepata wadhifa huo akiwa na umri mdogo zaidi. Bw Macron alizaliwa Disemba 21, 1977 mjini Amiens.

Rais huyo amesoma hadi chuo kikuu, ambapo alifuzu kwa shahada ya uzamili kisha akajiunga na serikali kuhudumu katika wizara ya fedha. Akiwa serikalini, alikuwa mwanachama wa chama chama Party Socialiste (PS) kati ya 2006-2009. Chama hicho kikitafsiriwa kwa Kiswahili ni Chama cha Kisoshalisti cha Ufaransa.

Mnamo 2008, Macron aliasi utumishi wa umma na kujiunga na benki ya Rothschild.

Miaka minne baadaye, 2012 alipata fursa ya kipekee kufanya kazi katika ofisi ya Rais wa Ufaransa wakati huo Francois Hollande kama naibu katibu mkuu.

Nyota yake ya jaha iliendelea kumuonekania, ambapo 2014 aliteuliwa kuwa Waziri wa Uchumi, Viwanda na Teknolojia.

Mwaka wa 2016, Macron aliunda chama chake cha "'La Republique En Marche'.

Hata hivyo, Rais Hollande ambaye kwa sasa ni mstaafu hakufurahishwa na hatua hiyo. Utangulizi wake haukuwa rahisi kwa kuwa Hollande alimkosoa kwa kuchukua hatua nyingine kisiasa.

Bw Macron alikata kauli kujiuzulu serikalini na kutangaza azma ya kuwania urais mwaka wa 2017. Mpinzani wake alikuwa Francois Fillon wa chama cha "de Gaulle". Msimu wa kampeni, kura za maoni zilionesha kuwa endapo uchaguzi ungefanyika wakati huo Macron angekuwa wa tatu.

Mgombea mwenza Fallon hata kabla ya uchaguzi alisakamwa na sakata za ufisadi ambazo zulishusha umaarufu wake. Awamu ya kwanza ya kura, alishikania na mgombea mwenza Marie Le Pen wa chama cha Front National. Katika awamu ya pili, Macron aliibuka kidedea kwa kuzoa asilimia 66 ya kura zilizopigwa na raia wa Ufaransa.

Mke wa Macron

Mkewe Rais Macron ni Bi Brigitte Trogneux, ambaye alikuwa mwalimu wake katika shule ya upili. Wawili hao walianza  uhusiano wakati Macron akiwa shuleni.

Licha ya wazazi wake kupinga uhusiano wao na hata kumhamisha shule, waliendelea kuchumbiana ikizingatiwa kuwa Bi Brigitte amemzidi Macron kwa miaka 24. Walifunga ndoa mnamo 2007.

Macron ni kiongozi mwenye msimamo ambao haumzuii kukosoa kitu aonapo hitilafu.

Kisa cha hivi punde ni mgogoro unaonekana kuibuka kati ya Italia, Malta, na Ufaransa; kwa jinsi Italia ilivyoshughulikia meli iliyowachwa katika bahari ya Meditarenia mnamo wikendi ambapo raia 629 wa Libya waliokolewa.

Italia na Malta zilikataa meli hiyo kufunga gati katika pwani yake.

Rais huyo aliikosoa Italia akiitaja kama nchi tepetevu kwa kutoruhusu meli hiyo kushusha abiria hao wa Libya katika bandari yake. Nchi ya Hispania Jumatatu ndiyo ilitatua uhasama wa meli hiyo na kutangaza kwamba itakapowasili itue katika bandari yake ya Valencia.

Italia kwa upande wake inasema Ufaransa katika ukosoaji wake imedhihirisha undumakuwili wake.

Kauli ya Rais Macron imezua utata, Roma ikitaka Ufaransa kuomba Italia msamaha kwa matamshi hayo.

"Kauli kama hizo ni za kudunisha uhusiano kati ya Ufaransa na Italia," wizara ya maswala ya nchi za kigeni Italia ikasema kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari mnamo Jumatano.

Aidha, mvutano huo ulisababisha waziri wa Biashara na Uchumi Italia, Giovanni Tria, kufutilia mbali ziara yake katika nchi ya Ufaransa kwa msingi kuwa meli ambayo angeabiri nayo imejaa abiria.