FUNGUKA: ‘Twatumia mpini mmoja kitandani...’

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Wednesday, January 3  2018 at  16:58

Kwa Mukhtasari

IKIWA unajihesabu kuwa mmoja wa watu ambao wamewahi kukumbana na mahusiano ya mapenzi ya kiajabu, basi huenda haujakutana na ule wa Jerry, Amanda, Christine na Vanessa.

 

Kwanza kabisa acha nikupe mwangaza kuhusu wanne hawa. Jerry ni kaka mwenye umri wa miaka 47 na mhasibu katika mojawapo ya mashirika makuu ya ukaguzi wa mahesabu.

Bwana huyu ameoa mabinti watatu, Amanda, Christine na Vanessa, ambao kando na kuwa wao ni madada, wao pia ni mapacha. Mabinti hawa wana umri wa miaka 37 ambapo pamoja na mume wao wanaishi kwenye jumba moja na hata kulala katika chumba kimoja.

Wanne hawa wamekuwa katika uhusiano huu kwa miaka tisa sasa na hata wamejaliwa watoto sita huku kila binti akimzalia kaka huyu wana wawili. Mabinti hawa wana taaluma za kutamaniwa kwani Amanda ni daktari, Christine ni mhudumu wa kiafya na Vanessa ni meneja wa benki.

Maisha yao kama anavyoeleza Amanda ni ya kawaida kiasi cha kuwa kama wanandoa wengine, wanawake wanakabiliwa na majukumu ya upishi, uzazi na usafi nyumbani, huku mume akiwajibikia mahitaji ya kifedha.

“Pamoja tuna watoto sita ambapo kila mmoja anachukulia kuwa watoto hawa ni wake na sote tuna jukumu la kudumisha nidhamu na kuchukua muda kukaa nao.

Tunalala katika chumba kimoja na katika masuala ya mahaba lazima kila mmoja ashiriki. Hakuna uwezekano wa wawili kujificha na kujihusisha na mahaba ikiwa wengine hawahisi vyema kiafya au hawana hamu.

Kwa kawaida sisi hushauriana kuhusu masuala yote katika nyumba yetu ikiwa ni pamoja na aina ya fanicha ya nyumbani, chakula cha kupika, shule ya watoto kuhudhuria na hata mahali pa kwenda likizoni au hata kuishi.

Kitandani, hakuna ana upande hususan wa kulala. Kila baada ya saa kadha wakati wa usiku, mume analala katikati huku sisi wake zake tukibadilishana kila mara ili kila mmoja apate fursa ya kuhisi joto lake.

Wikendi inapofika sote tunaenda deti pamoja huku sote tukiwa tumeshikana mikono. Kila mmoja wetu anaposhika mimba na kukaribia kujifungua, sharti sote tuliosalia tuchukue likizo na kumsaidia.

Sababu iliyotufanya kuolewa na mwanamume mmoja ni kuwa sisi ni mapacha na tangu tuzaliwe tumezoea kuishi pamoja na hatungekubali ndoa kututenganisha.

Mwanzoni ni mimi niliyekutana na mume wetu mtandaoni. Baada ya muda nilizungumza naye na kumweleza kuhusu madada zangu wengine na iwapo angekubali kutuoa sote na hakuwa na tatizo na hilo.

La kushangaza ni kuwa hakuna wakati hata mmoja ambapo tunatawaliwa na hisia za wivu. Siri yetu ni kuzungumza na kusuluhisha tatizo kila linapochipuka badala ya kukorofishana. Japo kuna baadhi ya jamaa zetu wasiokubaliana na uhusiano wetu, kwetu mradi sisi tuna furaha, basi hisia za wengine sio muhimu”.