http://www.swahilihub.com/image/view/-/5015256/medRes/2274058/-/g92l1v/-/figo+pic.jpg

 

Fahamu sababu za figo kutofanya kazi

 

Na Mwandishi wetu

Imepakiwa - Friday, March 8  2019 at  12:39

 

Leo nitawapa ufahamu kuhusu sababu za kupata tatizo la figo lengo nikuipa elimu jamii ili kuwa na tahadhari ya mapema.

Figo ni ogani muhimu ya ndani ya mwili (pango la tumbo) inayohusika na uchujaji wa damu inayozunguka mwilini kwa jina la kitabibu hujulikana kama Kidney au Renal.

Katika mwili usio na hitilafu yoyote una figo mbili upande wa kushoto na kulia ambazo ndizo zinazotuwezesha kuchuja damu na kutoa taka mwili zinazotolewa kwa njia ya mkojo.

Ogani hii inaweza kushambuliwa na maradhi mbalimbali au madhara ya vitu ikiwamo sumu na kushindwa kufanya kazi yake kwa ufanisi, hali hii ikitokea mwili unakuwa katika wakati mgumu kiutendaji.

Mtu anaweza kupata tatizo la figo kushindwa kufanya kazi kwa muda tu au kupata tatizo sugu la figo kushindwa kufanya kazi na hivyo kuhitaji usaidizi wa mashine ijulikanayo kama dialyisis.

Figo zinaposhindwa kufanya kazi yake husababisha mwili kuwa na mrundikano wa maji yaliyozidi ambayo yangelihitaji kutolewa kwa njia ya mkojo.

Na hii ndiyo sababu mtu mwenye tatizo hili huweza kuonekana kuvimba kwa uso na miguu kutokana na maji kukusanyika na kujirundika.

Vilevile hali hii husababisha takasumu na mabaki (uchafu) mengine yasiyohitajika mwilini kurundikana hali inayosababisha mwili kupata madhara mbalimbali kutoka na mabaki hayo.

Matatizo haya yanapojitokeza huchochea kuibuka kwa madhara makubwa ya kiafya ikiwamo shinikizo la juu la damu, kutowiana kwa chumvi na maji mwilini na upungufu wa damu.

Vilevile magonjwa ya mifupa, kuongezeka kwa kiwango cha tindikali katika damu, kiwango cha mafuta mabaya kuongezeka mwilini, shambulizi la ubongo kutokana na takasumu kurundikana.

Magonjwa sugu mawili yasiyoambukiza ambayo ni Kisukari na shinikizo la juu la damu ndiyo chanzo kikubwa cha kujitokeza kwa ugonjwa sugu wa figo.

Matatizo haya mawili yatokanayo na mienendo na mitindo mibaya ya maisha ndiyo yanayochangia idadi kubwa ya wagonjwa wa figo kuongezeka duniani. Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu