http://www.swahilihub.com/image/view/-/4217974/medRes/1829724/-/123lml7/-/nyenze.jpg

 

Francis Nyenze: Juni 2, 1957 hadi Desemba 6, 2017

Francis Nyenze

Francis Nyenze. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  07:31

Kwa Muhtasari

Francis Nyenze amemwacha nyuma mjane na watoto wao watatu, wakiwa ni mvulana mmoja na wasichana wawili.

 

WAKENYA waliamka Desemba 6, 2017 habari za kifo cha mbunge wa Kitui Magharibi zikiwasubiri.

Mbunge huyo imeripotiwa alifariki baada ya kuugua kwa muda.

Mheshimiwa Nyenze aliripotiwa kuwa na Saratani ya matumbo na iliyomuua katika hospitali ya Nairobi.

Sasa kutakuwa na uchaguzi mdogo katika eneo hilo.

Katika uchaguzi wa Agosti 8, 2017, Nyenze alishinda wadhifa huo, akizoa kura 21,136 kuwakilisha asilimia 54.68 ya kura zilizojumlishwa.

Alifuatwa naye Robert Mutiso Lelli wa chama cha Ford Kenya aliyezoa kura 6,525 ikiwa ni asilimia 16.88.

Wa tatu bora alikuwa ni Hannington Mbiti aliyezoa kura 4,498 huku Rodgers Mbai wa Jubilee akiibuka wa nne kwa kuzoa kura 4,252 kumaanisha asilimia 11 ya kura zote.

Nyenze aliibuka kidedea miongoni mwa wapinzani wake saba akiwania kwa tiketi ya Wiper Democratic Movement of Kenya (WDM-K), chama tanzu ndani ya muungano wa National Super Alliance (Nasa), kinara wao akiwa ni Raila Amolo Odinga.

Nyenze alizaliwa Juni 2, 1957 katika kijiji cha Kabati na katika harakati zake za kusaka elimu, akaishia kuhitimu kuwa mtaalamu wa michoro ya ramani za nyumba kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi. 

Aliingia bungeni mwaka wa 1997 ambapo alishida wadhifa wake kwa tiketi ya chama cha Kanu na akateuliwa kuwa waziri wa Mazingira ndani ya utawala wa rais Daniel Moi na akahamishiwa pia katika wizara ya ruradhi za kitaifa na michezo katika huduma ya kipindi hicho chake bungeni.

Alitokomea kisiasa na akaibuka tena katika uchaguzi mkuu wa 2013 ambapo alishinda ubunge huo kwa tiketi ya Wiper Democratic Movement of Kenya chini ya uongozi wa kinara wao, Kalonzo Musyoka.

Hata hivyo, Kalonzo aliingiza chama hicho katika muungano wa Cord na ambapo akiwa mgombea mwenza wa Raila Odinga, walishindwa na muungano wa Jubilee ukiongozwa na Uhuru Kenyatta na William Ruto.

Marehemu Francis Nyenze amekuwa msingi mkuu wa Wiper Democratic Movement (WDM) kwa kuwa mtetezi wa daraja la juu wa Kalonzo Musyoka.

Bw Kalonzo ndiye kiongozi wa WDM na kinara mwenza wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) unaoongozwa na Raila Odinga. Kwa hakika si pigo tu kwa wakazi wa Kitui Magharibi alikokuwa mbunge wao, jamii ya Ukambani na taifa kwa jumla, ila dafrau kwa Kalonzo Musyoka pia.

Itakumbukwa kwamba mwanzoni mwa mwaka huu wakati wa harakati za kuteua mpeperusha bendera wa Nasa, Bw Nyenze alisimama kidete na kauli yake kuwa Kalonzo Musyoka sharti apewe bendera hiyo. Alishikilia sharti mkataba wa 2013 chini ya mwavuli wa Cord uliotiwa sahihi lazima uheshimiwa.

2013 Bw Raila aliwania urais kwa tiketi ya Cord akisaidiwa na mgombea mwenza Kalonzo, ambapo duru ziliarifu mkataba ulikuwa endapo Raila angeibuka mshindi kwenye uchaguzi huo au la, uchaguzi wa 2017 asingekuwa na budi ila kuheshimu mkataba na kuunga mkono Kalonzo awanie urais.

"Iwapo si Kalonzo Musyoka sisi tutaenda peke yetu, tusahau Nasa. Kwa sababu jamii ya Ukambani inasubiri 'mwana' wao avishwe taji la urais, awanie urais," akasema Nyenze kwenye kumbukumbu zake.

Hata hivyo, Kalonzo alipinga madai hayo akisema hayakuwa msimamo wa Wiper.

Nyenze alichukuliwa kuwa 'sauti' ya WDM kutokana na ushawishi wake chamani.

Mzozo uliibuka ambapo Nyenze aliungwa mkono na wabunge kadha kutoka jamii ya Ukambani wakitaka Kalonzo awanie urais 2017.

Bw Raila hatimaye aliteuliwa kuwa mpeperusha bendera ya Nasa akisaidiwa na Kalonzo, jambo ambalo Nyenze alilichukua kwa uzito. Kalonzo alilazimika kuketisha mbunge huyo na kumshawishi atulie ili 'nyumba' ya WDM isisambaratike. Marehemu alijitokeza na kukiri hadharani kuwa alikubali uteuzi wa Kalonzo kuwa mgombea mwenza wa Raila. "Iwapo Nyenze asingesema iwapo si Kalonzo hakuna Nasa, hata hiyo nambari mbili tusingepata," akaeleza na kutuliza mawimbi ya Wiper.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, Nyenze wakati mmoja alionekana kupigia debe Rais Uhuru Kenyatta wa Jubilee kwenye hafla ya vijana ya huduma kwa taifa (NYS) Kitui. Alipongeza miradi ya maendeleo ambayo serikali ya Kenyatta na Naibu Rais William Ruto imefanya kwa jamii ya Ukambani hususan kaunti ya Kitui.

"Mnaweza mkamsahau Rais Uhuru Kenyatta kwa maendeleo ambayo amewafanyia?" akauliza wakazi wa Kitui, kwenye hafla hiyo ya kuzindua mradi wa NYS eneo hilo.

Aidha matamshi hayo yalizua tumbojoto, ambapo baadhi ya wabunge wa Ukambani walioko Nasa walikashifu kauli yake. Hata hivyo, Nyenze alifafanua baadaye alichomaanisha na kueleza wazi kuwa yeye ni mfuasi wa Nasa.

Marehemu Nyenze aliaga jana Jumatano majira ya asubuhi saa moja na robo, katika Nairobi Hospital Hospital alikokuwa akipokea matibabu baada ya kuugua kwa muda mrefu Saratani. Mwili wake umehifadhiwa Lee Funeral Home, huku shughuli za kuandaa mazishi yake zikiendelea.

Itakumbukwa kwamba Marehemu alihudhuria hafla ya kuapishwa kwa wabunge bungeni akiwa na tenki ya hewa ya Oxijeni, ambapo ilikuwa ikimsaidia kupumua.
Nyenze alizaliwa mnamo Juni 2, 1957 akasomea katika shule ya upili ya wavulana ya Kagumo High kisha akajiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN).

Alichaguliwa mara ya kwanza kama mbunge wa Kitui Magharibi mwaka wa 1997 kwa tiketi ya chama cha KANU. Mwaka wa 2002 alibwagwa, na kurejea tena katika ulingo wa siasa mwaka wa 2013 ambapo alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha Wiper.

Katika kipindi cha huduma yake 2013 hadi 2017, alikumbwa na msukosuko wa kisiasa ambapo hakueleweka vyema kama ako ndani ya Nasa au ndani ya Jubilee lakini hatimaye akagombea kwa tiketi ya Wiper Agosti 8, 2017 na akaibuka mshindi.

Msukosuko huo uliishia yeye kukosa makali katika wadhifa wake wa kinara wa wachache bungeni na hadi taifa likielekea kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 8, alikuwa akipigia debe uwaniaji wa Rais Uhuru Kenyatta badala ya ule wa kinara wa muungano wake, Raila Odinga.

Nyenze amemwacha nyuma mjane na watoto wao watatu, wakiwa ni mvulana mmoja na wasichana wawili.