http://www.swahilihub.com/image/view/-/3075064/medRes/1254703/-/vm3kjy/-/rose.jpg

 

PAMBO: Kuchagua mke kunahitaji kazi ya ziada, si kutazama makalio na matiti ya mabinti

Amber Rose

Amber Rose aonyesha makalio yake. Picha/HISANI 

Na BENSON MATHEKA

Imepakiwa - Sunday, December 3  2017 at  17:30

Kwa Mukhtasari

KUNA hulka moja inayomganda kila mwanamume: Kugeuza shingo kutazama makalio ya wanawake, kukazia macho vifua vya wanawake na kumezea mate maziwa yao na kupagawishwa na vishimo kwenye mashavu ya wanawake, maarufu kama dimples.

 

Kila mwanamume, hutamani kuoa mwanamke mwenye umbo nzuri, maarufu kama size 8, miguu ya chupa, shingo ya upanga na mwenye macho maangavu. Haya ni maradhi yanayowafanya wanaume kujuta kwa sababu sura na umbo nzuri hakumaanishi mwanamke anatosha kuwa mke.

Ni wengi ambao walitumia pesa nyingi kuwaoa wanawake warembo lakini baada ya muda wanagundua kuwa chochote king’aacho sio dhahabu, maisha waliyotarajia kuwa ya furaha na ufanisi yanabadilika kuwa jinamizi, majuto.

Hii ndiyo sababu wanaume wengi wanasumbuliwa na mfadhaiko na shinikizo la damu na vidonda vya utumbo kwa kukosa amani. Takwimu za mashirika tofauti zinaonyesha idadi ya wanaume wanaosumbuliwa na mfadhaiko na shinikizo la damu inazidi kuongezeka huku idadi ya ndoa zinazovunjika ikiendelea kupanda pia.

Majuto ni mjukuu, huja kinyume, wanaume tutazinduka lini kwa sababu hautuonekani kujifunza kutoka kwa tajiriba zetu au kwa waliotutangulia au majirani zetu.

Sio ajabu kuona mtu akimchukua mke wa jirani yake licha ya kuelewa tabia zake eti kwa sababu ana sura nzuri. Unampata jamaa akifunga na kuomba ili jirani yake akosane na mkewe aweze kumvamia eti kwa sababu ana sura nzuri.

Ni wanaume wengi wanaokosa usingizi wakiwaza wake za watu wengine. Nilimsikia mmoja akisema kuwa huwa anatuma mawazo yake kumchota mke wa jirani yake anapofanya mapenzi na mkewe eti ngoma na mkewe ni kawaida tu, raha kwa kuwafikiria vipusa wa nje.

Imesemwa mara nyingi na ninarudia kwamba furaha katika ndoa haipatikani katika urembo, sura au umbo. Furaha ya ndoa haipatikani katika elimu au mali ya mtu, furaha ya ndoa haipatikani kwa sababu mtu huenda kanisani au msikitini kila wakati na kutoa sadaka nono. 

Furaha ya ndoa haipatikani katika zawadi ambazo mtu anakununulia. Inapatikana katika moyo wa mtu, ni tabia zake, ni msingi wa imani yake kwa sababu anaweza kuwa ameokoka lakini tabia zake ni mbaya, akose heshima na utu.

Kumbilia kuoa mwanamke kwa sababu ana makalio yanayowafanya wanaume kuvunjika shingo wakimtazama au ana sauti ya ninga pekee ni kujitia majutoni.

Na sisemi wanawake wote wenye sura na umbo nzuri wana mioyo michafu la hasha. Kuna wale ambao sura zao zinaoana na mioyo yao.

Kuna walio na sura za malaika na mioyo ya ibilisi na kuna walio na sura mbaya na mioyo ya malaika. Kuchagua mke kunahitaji kazi ya ziada ikiwa wanaume wataepuka shinikizo la damu na mfadhaiko. Kunahitaji zaidi ya tamaa ya kula uroda.