http://www.swahilihub.com/image/view/-/1688292/medRes/413202/-/lt8di9/-/Bensoudaa.jpg

 

JAMVI: Fursa kwa ICC kujikomboa dhidi ya tuhuma kwamba inalenga Afrika pekee

Fatou Bensouda

Kiongozi wa mashtaka katika Mahakama ya ICC, Bi Fatou Bensouda. Picha/BILLY MUTAI 

Na VALENTINE OBARA

Imepakiwa - Sunday, November 12  2017 at  15:34

Kwa Muhtasari

KWA mara nyingine, macho yote yamo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) huku wengi wakitaka kuona ikiwa itafanikiwa kujiondolea sifa kwamba ni taasisi iliyobuniwa na Wazungu kwa lengo la kuwadhulumu viongozi wa mataifa ya Afrika pekee.

 

Upande wa mashtaka katika mahakama hiyo wikendi iliyopita uliomba majaji idhini ya kuanzisha uchunguzi kuhusu uhalifu wa kivita Afghanistan, na kuna uwezekano mkubwa upelelezi huo utalenga wanajeshi wa Amerika.

Ingawa Amerika si mwanachama wa ICC, Afghanistan ilitia sahihi Mkataba wa Roma unaosimamia mahakama hiyo mnamo 2003. Hivyo basi, ICC ina idhini ya kuchunguza uhalifu wa kivita uliotendeka nchini humo tangu wakati huo hadi sasa.

Kiongozi wa Mashtaka katika mahakama hiyo, Bi Fatou Bensouda, alitangaza ana sababu za kuamini kuna uhalifu wa kivita na ukiukaji haki za binadamu uliotendwa Afghanistan wakati wa vita vikali kati ya makundi tofauti.

“Jopo la majaji litakalochaguliwa na Rais wa ICC ndilo litaamua kama nimewaridhishwa kuwa kuna sababu za kutosha kuidhinisha upelelezi,” akasema.

Wanajeshi wa Amerika wamekuwa katika mstari wa mbele kwenye vita hivyo vilivyoanza punde baada ya shambulio la kigaidi Amerika mnamo Septemba 11, 2001, chini ya aliyekuwa Rais George Bush.

Kwenye ripoti iliyokuwa imetolewa awali na afisi ya Bi Bensouda, ilisemekana upande wa mashtaka unaamini wanajeshi hao walitesa washukiwa waliokamatwa na kuwatendea ukatili kwenye magereza ya siri ambayo yalisimamiwa na Idara Kuu ya Ujasusi (CIA) ya Amerika.

Tangazo la Bi Bensouda lilitokea siku chache baada ya Burundi kujiondoa rasmi katika mahakama hiyo.
Hatua hiyo ilifanya Burundi iwe nchi ya kwanza kutekeleza wito ambao umekuwa ukitolewa na nchi nyingi za Afrika kutaka zijiondoe kwa pamoja zikiwemo Kenya, Uganda, Afrika Kusini na Gambia.

“ICC imezidi kudhihirisha kwamba ni chombo cha kisiasa na silaha inayotumiwa na mataifa ya magharibi kufanya nchi zingine kama watumwa. Huu ni ushindi mkubwa kwa Burundi kwani imelinda uhuru wake,” msemaji wa rais, Bw Willy Nyamitwe, alinukuliwa kusema.

Nchi hiyo inayoongozwa na Rais Pierre Nkurunziza, inatuhumiwa kuhusika na matukio ya ukiukaji wa haki za kibinadamu kufikia sasa.

Mkurugenzi Msaidizi wa masuala ya haki kimataifa katika shirika la Human Rights Watch, Bi Param-Preet Singh, alisema hatua ya Bi Bensouda kuomba ruhusa ya kufanya upelelezi imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu.

Kulingana naye, kumekuwa na matukio mengi zaidi ya mauaji ya kikatili, kutoweka kwa watu katika hali isiyoeleweka, visa vya mateso na mashambulio dhidi ya raia nchini humo tangu upande wa mashtaka ulipoanza kutathmini hali ya Afghanistan miaka 10 iliyopita.

“Uwezekano wa kuwa upelelezi wa ICC utajumuisha ukandamizaji wa haki za binadamu uliofanywa na wanajeshi wa Amerika na maafisa wa CIA ni dhihirisho tosha kwamba katika mahakama hii, raia wa mataifa yenye ushawishi mkubwa zaidi hawataepuka sheria,” akasema kwenye taarifa.

Hata hivyo, wachanganuzi wengine wa masuala ya haki kimataifa wanaamini Bi Bensouda atakumbwa na changamoto kubwa endapo ataamua kufanya upelelezi kuhusu wanajeshi wa Amerika.

Kulingana na mkuu wa haki kimataifa katika shirika la Amnesty International, Bw Solomon Sacco, inafaa mkuu huyo wa mashtaka ajiandae kwa changamoto za kisiasa na kirasilimali endapo ataruhusiwa kuanzisha upelelezi.

“Mataifa makuu ulimwenguni na mataifa yaliyo wanachama wa ICC yana ushirika Afghanistan, na raia wao huenda wakapelelezwa na mahakama. ICC itategemea mataifa wanachama kukabiliana na changamoto hizi za upelelezi,” akasema.

Mbali na wanajeshi wa Amerika, inatarajiwa pia upelelezi ukifanywa, utalenga wanamgambo wa kundi la Taliban linaloshirikiana na Al-Qaeda, na maafisa katika serikali ya Afghanistan.

Pingamizi dhidi ya ICC kutoka kwa nchi za Afrika lilizidi wakati Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto waliposhinda uchaguzi wa urais 2013, kesi dhidi yao kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 zikiendelea.

Juhudi za viongozi wa Afrika hasa kupitia kwa Muungano wa Afrika (AU) kutaka kuwe na sheria ya kuzuia kushtakiwa kwa viongozi walio mamlakani hazikufua dafu.