http://www.swahilihub.com/image/view/-/4656118/medRes/2039825/-/932a2a/-/gab.png

 

Gabriel kuing’arisha Tanzania kimataifa

Mwanariadha Gabriel Geay  

Na Imani Makongoro

Imepakiwa - Tuesday, July 10  2018 at  16:02

Kwa Muhtasari

Ametwaa medali ya pili ya dhahabu nchini Marekani

 

Dar es Salaam: Mwanariadha Gabriel Geay amezidi kuing’arisha Tanzania kimataifa, baada ya juzi jioni kutwaa medali ya pili ya dhahabu nchini Marekani.

Geay aliibuka kinara katika mbio za ‘Boilermaker Road Race’ zilizofanyika kwenye Mji wa New York akiwapiku Wakenya zaidi ya 10 waliokuwa kwenye kinyang’anyiro hicho. Nyota huyo wa mbio ndefu (mita 5,000 na 10,000), aliibuka shujaa wa mbio za kilomita 15 alipotumia dakika 43 na sekunde 40 kumaliza.

Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Geay ambaye hivi karibuni alitwaa medali ya dhahabu katika mbio za kilomita 10 za Boston zilizofanyika nchini humo. “Haikuwa kazi nyepesi kutwaa medali hiyo mbele ya Wakenya na Waethiopia wengi waliokuwa wakichuana,” alisema Geay jana alipokuwa akizungumza na gazeti hili.

“Hakuna ‘mchawi’ kwenye ushindi zaidi ya maandalizi, tangu nimefika Marekani nimekuwa nikifanya mazoezi, mazingira ya maandalizi huku nilipo yana tofauti kubwa na nyumbani Tanzania,” alisema Geay.

Katika mbio hizo, mwanariadha wa Ethiopia, Teshome Mekonen Asfa alitwaa medali ya pili ya fedha akitumia dakika 43:50 na Mkenya, Edwin Kibichiy alihitimisha tatu bora akikiambia kwa dakika 43:55.

Geay yuko Marekani kwa miezi kadhaa sasa akichuana katika mbio tofauti chini ya Kampuni ya Posso Sports ambayo imekuwa ikiwafadhili wanariadha kutoka nchi mbalimbali duniani.

“Nimebakiza mbio tatu katika mkataba wangu ambao unahitaji nikimbie mbio nane tofauti. wiki ijayo natarajia kwenda Colombia ambako nitakwenda kuchuana na nyingine zilizobaki zitafanyika hapa Marekani,” alisema mwanariadha huyo.

Mwanariadha huyo alikuwa katika kikosi cha timu ya Taifa kilichokwenda kwenye Olimpiki ya Rio 2016 Brazil, lakini alishindwa kushiriki baada ya kupata majeruha ya goti la kushoto akiwa nchini humo.