http://www.swahilihub.com/image/view/-/4611828/medRes/2008456/-/dffci2/-/mjilisa.jpg

 

Garissa: Kaunti ya Kaskazini Mashariki mwa Kenya

Garissa

Mbunge wa Garissa Mjini, Aden Duale (kushoto) akiwa na Waziri wa Kawi Bw Charles Keter (aliyeashiria kidole), na mbunge wa Balambala Omar Shurie na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Usambazaji Umeme Mashinani (REA) Bw Simon Gicharu katika kituo cha umeme kutokana na jua kilichopo Raya, Kaunti ya Garissa County. Picha/ABDIMALIK ISMAIL 

Na SAMMY WAWERU, MASHIRIKA na KABRASHA LA HISTORIA

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  11:17

Kwa Muhtasari

Garissa ni kaunti iliyoko Kaskazini Mashariki mwa Kenya, na inapakana na Turkana, Wajir, Marsabit, Mandera na nchi ya Somalia.

 

KWA utambulisho, Garissa ni kaunti nambari 007 kulingana na katiba iliyozinduliwa 2010 na kuanza kutumika 2013.

Ina ukubwa wa kilomita 45,720.2 mraba, na kukadiriwa kuwa na zaidi ya watu 923,060 kwa mujibu wa sensa ya 2009. Wakazi wengi wa Garissa ni wenye asili ya jamii ya Somalia.

Kaunti hiyo ndiyo yenye kambi kubwa nchini ya wakimbizi - Dadaab na huwa na wakimbizi 260,000 kutoka nchini Somalia kulingana na ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) la kushughulikia wakimbizi ya 2016.

Aidha, ina maeneobunge sita; Garissa Mjini, Dadaab, Lagderaz Balambala na Ijara.

Bw Aden Duale ambaye ni kiongozi wa wengi bungeni ni mmoja wa viongozi wanaotoka Garissa, na anawakilisha eneobunge la Garissa Mjini.

Jamii inayoishi Garissa inaaminika kuendesha shughuli za ufugaji wa kuhamahama, ambapo ng'ombe, mbuzi na ngamia ndiyo utajiri wao mkuu.

Hata hivyo, kaunti hiyo inaonekana kubadilisha taswira hiyo na kuzamia zaraa.

Msimu wa kiangazi Garissa huwa mojawapo ya kaunti zinazopokea msaada wa vyakula, japo kutokana na mikakati inayoonekana kuwekwa na serikali ya kaunti chini ya uongozi wa gavana Ali Korane kwa ushirikiano na serikali ya kitaifa huenda baa la njaa likawa historia na kulisha eneo la Kaskazini Mashariki.

Maji ya Mto Tana yanatumiwa na wakazi waliojiunga kwa makundi kufanya kilimomseto.

Ukuzaji wa mahindi katika mazingira yanayokaribia mto huo umeshika kasi.

Ni kutokana na uwepo wa maji ya Mto Tana ambapo wakazi, mabwanyenye na makampuni yameanza kuwekeza katika sekta ya kilimo Garissa. Bw Michael Ogola, meneja wa Maendeleo Farm Garissa, mradi wa kilimo unaofanywa Garissa na kumilikiwa Meja (mstaafu) anasema wakazi wa kaunti hiyo wametambua umuhimu wa kilimo.

“Mkulima wa mashamba madogo madogo ana uwezo wa kupata Sh480, 000 zikikokotolewa kwa mwezi ni Sh40, 000. Ni wangapi wanaopokea mshahara kama huo kwa mwezi nchini licha ya kufuzu kwa shahada?” ahoji Ogola.

Anaongeza kuwa wakulima wa mashamba makubwa huingiza kati ya Sh3 milioni hadi Sh10 milioni kwa mwaka kwa kukuza mimea aina mbalimbali kama mahindi, matunda, na mboga.

“Wote wananyunyizia mimea yao maji kupitia Mto Tana,” anaeleza meneja huyo.

Kwa muda wa miaka kadha sasa, Meja Mohamed amekuwa akifanya kilimo kwenye shamba lililo na ukubwa ekari 146.

Halikadhalika, kuna zaidi ya makundi 73 yanayofanya kilimo Garissa. Hata hivyo, mvua ya mafuriko iliyoshuhudiwa kuanzia mwezi Machi 2018, baadhi ya wakulima walishuhudia hasara kubwa kwa mazao yao shambani kusombwa na maji.

Shambulizi chuoni Garissa

Licha ya tija hizo tele za kilimo, mashambulizi katika Chuo Kikuu cha Garissa mnamo Aprili 2, 2015, yatasalia kwenye kumbukumbu za historia ya Kenya. Wanafunzi wapatao 148 walipoteza maisha yao kufuatia mashambulizi hayo ya kigaidi yaliyoshukiwa kutekelezwa na kundi haramu la Al-Shabaab. Hata hivyo, shughuli za masomo zimerejea hali yake ya kawaida chuoni humo na utangamano miongoni mwa jamii zinazoishi Garissa pamoja na zile geni, kutiliwa mkazo.

Kisa cha hivi punde Garissa, ni kile cha walimu kushambuliwa na baadhi yao kuuawa kupitia kundi haramu la Al-Shabaab.

Tangu Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wa Rais William Ruto wachukue hatamu ya uongozi 2013, sekta ya usafiri na uchukuzi imeonekana kuimarika Garissa kutokana na brabara zinazoundwa. Kufikia sasa, serikali ya kitaifa imetumia zaidi ya Sh600 kuunda barabara mpya Garissa ikiwa ni pamoja na kukarabati zilizotengenezwa katika serikali za awali.

Kutokana na mikakati ya serikali ya Jubilee, biashara zinaimarika Garissa huku watu kutoka sehemu mbalimbali za nchi wakikipiga kambi kaunti hiyo angaa kuzimbua riziki.

Mbali na Duale na gavana Korane, viongozi wengine Garissa ni Mohamed Yusuf Haji (seneta) na Bi Anab Mohamed Gure (mwakilishi wa wanawake wa kaunti katika bunge la kitaifa).