http://www.swahilihub.com/image/view/-/4701032/medRes/2071482/-/g058ue/-/githerimani.jpg

 

Githeri Man: Nimezaliwa upya

Githeri Man

Bw Martin Kamotho 'Githeri Man' baada ya kufuzu katika kituo cha kurekebisha tabia cha 'Mama Care' kilicho chini ya mwakilishi wa wanawake Kiambu Bi Gathoni Wa Muchomba mnamo Julai 24, 2018 mtaani Wangunyu. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Tuesday, August 7  2018 at  09:25

Kwa Muhtasari

Mwanamume mmoja alipata umaarufu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 baada ya picha zake kusambaa kwenye mitandao ya kijamii akionekana akila pure (githeri; mchanganyiko wa mahindi na maharage) wakati akiwa kwenye foleni akisubiri kupiga kura.

 

MWANAMUME mmoja alipata umaarufu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 baada ya picha zake kusambaa kwenye mitandao ya kijamii akionekana akila pure (githeri; mchanganyiko wa mahindi na maharage) wakati akiwa kwenye foleni akisubiri kupiga kura.

Bw Martin Kamotho 'Githeri Man', alipata umaarufu kama moto ueneavyo katika msitu wa nyika si tu anakoishi Kayole ila kote nchini.

Sifa zake hazikufikia hapo, alipokea zawadi aina mbalimbali ikiwamo kupewa kipande cha shamba.

Kilele chake kikawa kuwa miongoni mwa waliopokea tuzo ya taifa ( Head of State Commendation (HSC) 2017).

Hata hivyo, mapema Juni 2018 ilibainika mambo yalikuwa hayamwendei barabara baada ya kiongozi wa taifa, Uhuru Kenyatta kuagiza mwakilishi wa wanawake Kiambu Gathoni Wa Muchomba kuhakikisha Kamotho amejiunga na kituo cha kubadilisha tabia na mienendo. Sababu kuu hasa ikiwa ni unywaji wa pombe uliopitiliza.

Bw Kenyatta akitoa hati miliki za mashamba kwa wakazi wa Embakasi Mashariki katika uwanja wa Jacaranda jijini Nairobi, juhudi za Gatheri Man kuzungumza na kiongozi huyo wa taifa ana kwa ana ili amweleze ari yake ya kutaka kuacha pombe ziligonga mwamba. Dereva wa Rais hata hivyo, alimuona na kufanya mazungumzo naye na akaahidi kufikisha ujumbe wake ambao hatimaye ulizaa matunda.

Alijiunga na kituo cha kurekebisha tabia na mienendo kwa waathiriwa wa pombe na dawa za kulevya cha Mama Care kilichoko mtaani Wangunyu, Kiambu kwa muda wa miezi miwili.

Wa Muchomba ndiye patroni wa kituo hicho, na Kamotho ameambia Swahilihub kwa njia ya kipekee kuwa yeye sasa ni kiumbe mpya kutokana na marekebisho aliyopokea.

"Sitakubali kamwe kukaidi ahadi zangu kwa Rais Uhuru Kenyatta, alininusuru kutoka kwa minyororo ya unywaji wa pombe," akaeleza.

Mwaka 1989

Kulingana naye ni kwamba alianza kunywa pombe 1989 na juhudi zake kuiacha zimekuwa zikiambulia patupu. Kamotho ni mwajiriwa wa halmashauri ya jiji la Nairobi, ambapo hufanya shughuli za usafi.

Ameambia mtandao huu kuwa sasa atavalia njuga kampeni dhidi ya unywaji wa pombe, akijutia masaibu ambayo imemsababishia. "Nikikamilisha kipindi changu cha marekebisho ninayopitia, nitakuwa balozi wa kushauri vijana waache kunywa pombe na kuwanusuru," akaeleza.

Anasema kwa sasa anaendelea kupokea mafunzo katika Taasisi ya Kiufundi ya Kilima Mbogo, ambapo anasomea taaluma ya uhandisi wa magari. Mafunzo hayo yatachukua muda wa miezi miwili. Bw Kamotho ametoka kijiji cha Kiambururu, Githunguri kaunti ya Kiambu, na alikuwa miongoni mwa waathiriwa 77 waliofuzu katika kituo cha Mama Care awamu ya pili mwezi Juni.

Amesema akikamilisha mafunzo hayo, atarejea kazini na kwamba atayatumia kuimarisha utendakazi wake.

Wakati wa hafla ya waathiriwa hao kufuzu, Bi Wa Muchomba alifichua kuwa amepokea maombi ya vijana wapatao 600 Kiambu walio na ari ya kuasi unywaji wa pombe na utumizi wa dawa za kulevya. Kiambu ni mojawapo ya kaunti zilizoathirika na unywaji wa pombe haramu.

Gavana Ferdinand Waititu kwa ushirikiano na Wa Muchomba wamekuwa wakipambana na kero la unywaji Kiambu. Kwa siku kaunti hiyo hutumia Sh2 milioni katika jitihada za vita dhidi ya utumizi wa pombe haramu na dawa za kulevya. Kamotho anasema kuna haja ya vijana kutambua kuwa pombe haina faida zozote kwa mnywaji, akiwashauri kutathmini maisha yao ya usoni.