http://www.swahilihub.com/image/view/-/4373516/medRes/1929993/-/13sq84vz/-/ngamau.jpg

 

Githurai baada ya Katitu kuhukumiwa jela miaka 15

Titus Ngamau Musila

Afisa wa polisi wa zamani, Titus Ngamau Musila 'Katitu' akiwa mahakamani Nairobi, Aprili 5, 2018, ambapo amehukumiwa kifungo cha miaka 15; mitatu itakuwa ni kifungo cha nje, kwa kukutwa na kosa la kumuua Kennedy Mwangi Machi 4, 2013, eneo la Githurai 45. Picha/PAUL WAWERU 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Thursday, April 12  2018 at  09:59

Kwa Muhtasari

Kuna hofu kuwa wezi wa kuhangaisha wenyeji wa eneo la Githurai wanasherehekea kwa kuzidisha ukora wao kufuatia hatua ya mahakama kumhukumu Titus Ngamau Musila 'Katitu', afisa wa polisi aliyekuwa akiwaandama, kifungo cha miaka 15 gerezani.

 

KUNA hofu kuwa wezi wa kuhangaisha wenyeji wa eneo la Githurai wanasherehekea kwa kuzidisha ukora wao kufuatia hatua ya mahakama kumhukumu Titus Ngamau Musila 'Katitu', afisa wa polisi aliyekuwa akiwaandama, kifungo cha miaka 15 gerezani.

Kifungo hicho ni hukumu iliyosomwa na Jaji James Wakiaga kufuatia kisa cha miaka mitano iliyopita ambapo Katitu alidaiwa kumuua mshukiwa wa ujambazi mtaani Githurai 45 kwa jina Kenneth Kimani.

Katitu anakubalika na wenyeji wa mitaa ya Githurai 44 na 45 kuwa shujaa wao wakati akihudumu kama afisa wa polisi eneo hilo ambapo aliwaandama majambazi kwa kujituma na kuwapa afueni wenyeji - ya kutembea wakiwa na uhai na mali zao bila wasiwasi.

Sasa, afisa huyo akiwa na umri wa miaka 45 amehukumiwa kifungo gerezani kwa kupatikana na makosa ya kumuua Kimani mnamo Aprili 14, 2013, na kifungo hicho kina maana kuwa kiliwekwa makusudi kumwondoa kutoka ajira ya polisi kwa kuwa miaka 15 ijayo, atakuwa amestaafu rasmi kiumri kutoka huduma ya serikali.

Makundi ya kutetea haki za binadamu pamoja na mamlaka ya kuthibiti utendakazi wa polisi (IPOA) kwa pamoja kukawa na uwiano kuwa tukio hilo la kumuua Kimani halikuwa la uadilifu bali lilikuwa la  mauaji, na jaji Wakiaga akakubaliana na hilo.

Sasa, wenyeji wa mitaa hiyo wanalia kuwa wamegeuzwa kuwa wali na kitoweo na wahalifu na ambapo wakishaibiwa mali zao wakitembea barabarani, wanaambiwa na magenge hayo wamwendee Katitu wao awasaidie.

“Nilinyongwa katika mtaa wa Githurai 45 wiki jana na vijana watatu. Walininyang’anya Sh300 na simu yangu ya mkononi na kisha nikapewa salamu za makofi mawili usoni. Kisha wakaniambia niende nikamwite Katitu wetu aje anisaidie,” akasema James Mwaura, mkazi wa Githurai 45.

Anasema kuwa magenge yamerejea katika eneo hilo na wakati Katitu alihukumiwa kifungo gerezani, makundi ya majambazi yalionekana hadharani na tena waziwazi katika mabaa yakibugia pombe na kutangaza kuwa kazi ya kuhangaisha na ianze.

Ni hali sawa na hiyo katika mtaa wa Githurai 44 na Zimmerman ambapo majambazi waliokuwa wanathibitiwa na Katitu huwa na ngome aidha za maficho au ya kutekelezea kazi zao haramu.

Bi Grace Mueni anasema kuwa tangu Katitu atiwe mbaroni, kuna hali ya kuwa kawaida watu kushambuliwa kiholela bila afueni kupatikana kutoka kwa walinda usalama.

“Shida sasa ni kuwa, kuhukumiwa kwa Katitu kumeishia kuwa msumari wa mwisho kwa jeneza la usalama wetu kwa kuwa maafisa walioko sasa wanatangaza hadharani kuwa hawataiga mfano wa Katitu kiutendakazi ili nao wasiishie kuhukumiwa vifungo gerezani,” asema.

Anasema kuwa maafisa watundu wa polisi ambao hushirikiana na majambazi sasa wanatabasamu kwa kuwa wamepata uhuru wa kushirikisha harakati za ujambazi bila hofu ya Katitu kusambaratiwsha njama zao chafu.

“Ukiongeza hali kwamba wazazi wengi wa majambazi hawa ni matajiri, tunaishia na hali kwamba hata wale wachache wa maafisa wanaojituma kuwakamata wanaotuhangaisha wanaishia kupewa vitisho vya kushtakiwa na wanawaachilia washukiwa. Kwa sasa tuko kivyetu tujitunze kiusalama na tukijipata katika hatari mikononi ya majambazi, tuombe tu Maulana atunusuru kwa kuwa maafisa wa kiusalama hawana jibu kwetu,” asema Lilian Kimotho, mchuuzi wa mboga na matunda katika soko la Githurai 45.

Kuna mwingine aliyeomba jina lake libanwe ambaye anasema kuwa magenge hayo huwa na ngome katika steji za eneo hilo; katika baa za vichochoroni hasa eneo maarufu kwa jina Double M kupanda juu hadi Kiangiciri na kuvuka hadi maeneo la Ngomongo na ambapo chang’aa na bangi ni maarufu siku hizi bila hofu yoyote ya Katitu kutoka gerezani na kuwaandama.

Katibu Maalum katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho anasema kuwa serikali daima inataka wahalifu wawe wakikabiliwa.

Anasema kuwa serikali inafanya juu chini pia kuhakikisha kuwa wakazi wa Githurai hawatakumbana na sherehe hizo za majambazi.

“Mkuki wetu dhidi ya majambazi haujafungwa na cha maana kujua ni kuwa tutakabiliana na wahalifu,” asema Kibicho.

Mkurugenzi wa mpango wa kiusalama wa Nyumba Kumi, Joseph Kaguthi anasema kuwa wenyeji wa Githurai 45 na 44 wamekuwa wakituma jumbe za kulalamika kuhusu kuongezeka kwa uhalifu eneo hilo.

“Ni wazi kuwa majambazi wamechukua fursa ya mkosi wa Katitu kuimarisha harakati zao. Ni hali ya kusikitisha kwamba Jaji Wakiaga alikosa kuelewa hali halisi ya utendakazi wa afisa wa polisi. Sio raia wengi ambao huripotiwa wakisifu maafisa wa polisi na visa vingi huwa ni vya raia hao wakiteta vikali kuwahusu polisi. Lakini Wakiaga alikuwa na fursa ya kuwasikiza raia wakimsifu afisa wa polisi na hakuona hali hiyo ikiwa ni ya kuzingatiwa kama nguzo muhimu ya kuafikia maamuzi yanayowiana na wanaohudumiwa na mahakama na pia serikali yote kwa ujumla na ambao ni raia,” asema.

Bi Mueni anateta vikali kuwa wanasiasa wa Nairobi wamebakia kuwa bubu katika masaibu yao na ambapo licha ya kuwa wananukuliwa wakisema kuwa watapambana na uhalifu, hakuna anayejiunga na raia kuomboleza mkasa wa Katitu.

“Wakati alikamatwa, kuna baadhi ya wanasiasa ambao walijumuika nasi tukiandamana barabarani tukitaka Katitu aachiliwe. Kwa sasa wamebakia wanyamavu na ni kama hakuna baba wa watoto wanne aliyetoa taaluma na maisha yake pamoja na familia yake kafara akitulinda. Ninahuzunika kusikia kuwa hata mke wa afisa huyo alitoweka nyumbani baada ya mumewe kukamatwa akitulinda. Hukumu hiyo ya Wakiaga ilikuwa ya moja kwa moja kuwatuza majambazi na ujasiri wa kutuhangaisha,” asema.

Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria anasema kuwa wale watu ambao wameaga dunia katika mitaa ya Githurai tangu Katitu akamatwe ni takriban 20.

“Tangu Katitu ahukumiwe, kipindi cha wiki moja tu, wengine watatu wameuawa na majambazi katika mtaa wa Githurai. Nitapanga jinsi miili yao itawasilishwa kwa Jaji Wakiaga ili aone vile amewapa majambazi leseni ya kuhangaisha Wakenya,” alilalamika mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria.