http://www.swahilihub.com/image/view/-/4759066/medRes/2109470/-/uwb8k1z/-/guninita.jpg

 

Guninita afariki, wanasiasa wapata pigo

Aliyekuwa Mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita  

Na Kelvin Matandiko

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  12:12

Kwa Muhtasari

Alizaliwa mwaka 1958 katika Kijiji cha Epanko wilayani Ulanga mkoani Morogoro


 

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita amefariki dunia huku jina lake likibaki katika orodha ya wanasiasa waliokuwa wanatenda kile walichokiamini kwenye siasa na uongozi.

Kutokana na misimamo yake, Guninita aliishi maisha ya kisiasa katika vyama viwili tofauti, CCM na Chadema, ambako alikuwa ‘anaingia na kutoka.’

Jana, ndugu, jamaa, wanasiasa wakongwe na viongozi walitoa salamu za pole kwa nyakati tofauti huku wakieleza masikitiko yao kuhusu msiba huo.

Guninita aliyeacha mke na watoto watatu, alifariki dunia jana asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu ya uvimbe tumboni.

Gerald Guninita, ambaye ni mdogo wa marehemu, alisema kabla ya kifo, kaka yake alianza kusumbuliwa na kwikwi, kiungulia alipopelekwa hospitalini vipimo vilibainisha alikuwa na uvimbe tumboni.

Tangu Agosti 10 hadi jana asubuhi ya Septemba 13, mwaka huu, Guninita alikuwa akipatiwa huduma za matibabu ili kuokoa uhai wake na kulikuwa na mpango wa kumpeleka India kwa matibabu zaidi.

Siasa na uongozi

Guninita aliyezaliwa mwaka 1958 katika Kijiji cha Epanko wilayani Ulanga mkoani Morogoro, alishika nyadhifa za juu za uongozi ikiwamo Mkuu wa Wilaya ya Kasulu na Mwenyekiti wa CCM mkoani Dar es Salaam.

Guninita ambaye pia alipigana vita vya Uganda mwaka 1979, aliwahi kuwa katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kati ya mwaka 1987/88 na baadaye mwenyekiti wa umoja huo mwaka 1989 hadi 1996 ulipotokea mtikisiko.

Mtikisiko huo ulitokana na uamuzi wa umoja huo kueleza msimamo kuhusu wagombea urais waliowataka mwaka 1995.

Kutokana na mtikisiko huo, mwenyekiti (Guninita) na makamu mwenyekiti, katibu mkuu, naibu katibu walitakiwa na vikao vya CCM kujiuzulu.

Baada ya hatua hiyo, Guninita alijiunga Chadema ambako alidumu kwa miaka minne kuanzia mwaka 1996 hadi mwaka 2000 aliporejea CCM.

Miaka miwili baadaye alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, nafasi aliyoitumikia kwa kipindi kimoja baada ya mwaka 2007 kushindwa kutetea nafasi hiyo iliyochukuliwa na Ramadhani Madabida.