HESLB ibuni mbinu zaidi za kuwafikia wanufaika

Mkurugenzi wa idara ya urejeshaji mikopo,Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Ignatus Oscar 

Imepakiwa - Thursday, March 7  2019 at  10:04

 

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema inatafuta wahitimu 100,009 wanaodaiwa mikopo ya Sh277 bilioni.

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa idara ya urejeshaji mikopo, Ignatus Oscar inasema jumla ya wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu ambao mikopo yao imeiva ni 300,008 na ambao waliojitokeza kulipa wako 100,098 sawa na asilimia 63.

Oscar yuko mikoa ya Kanda ya Ziwa akihamasisha waajiri kutoa ushirikiano wa namna ya kuwapata wahitimu ambao hawajarejesha mikopo yao.

Bodi imepewa nguvu ya kisheria ya kukusanya mikopo kwa kuwaeleza waajiri kwamba wanapaswa kukata asilimia 15 ya mshahara ghafi (basic salary) wa mnufaika na kuwasilisha makato hayo HESLB ndani ya siku 14 baada ya tarehe ya mwisho wa mwezi.

Miongoni mwa changamoto ambazo bodi inalalamika kukutana nazo ni baadhi ya waajiri kutoa ushirikiano hafifu wa kuwasilisha taarifa za waajiriwa wapya kwenye bodi hiyo kama sheria inavyotaka.

Changamoto nyingine ni kitendo cha wanufaika hao kutolipa uzito suala la urejeshaji huku wakichukua mikopo mingine kwenye taasisi za fedha.

Rai yetu ni kuwa, pamoja na changamoto wanazozipata katika kukusanya marejesho kutoka kwa wanufaika walioajiriwa, bado bodi inatakiwa kushirikiana na Serikali kuweka mikakati bora zaidi ya kuwapata wahitimu ambao hawapo kwenye ajira rasmi.

Serikali ilipoanzisha bodi hiyo mwaka 2005 na kuipa jukumu la kukusanya fedha za mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika waliokopeshwa tangu mwaka 1994/1995, ilijua itaweka mfumo wa namna ya kuwapata wasomi hao.

Taarifa ya kuwasaka wahitimu 100,009 inaonyesha wazi kwamba bodi hiyo haifahamu waliko na hivyo inatumia fedha nyingine kuzunguka mikoani kuhamasisha waajiri wawang’amue na kuwakata marejesho hayo, jambo linalokula zaidi fedha za walipakodi.

Na ukweli kwamba soko la ajira linachukua sehemu ndogo ya wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu na unaiweka bodi hiyo katika hali ngumu ya kuwafutilia na kuwapata wahitimu ambao hawako katika ajira rasmi na hivyo fedha zinazotarajiwa kutoka kwao ili zirejee kunufaisha wengine zipo hatarini kutorudi kwenye mzunguko.

Maana yake ni kwamba, bodi hupotezana na mhitimu aliyenufaika na mkopo mara tu anapopokea fedha za mwisho kabla ya kumaliza chuo. Baada ya hapo hajulikani ameenda wapi na anafanya nini.

Upo uwezekano kwamba wasio katika ajira, wana shughuli za ujasiriamli zinazowaingizia fedha nyingi kuliko waajiriwa, lakini ni kitu gani kitakachoiwezesha bodi kuwafikia?

Kwa hiyo kitu muhimu ni bodi kuanza kutumia vizuri mifumo ya Serikali ya kukusanya taarifa za watu mbalimbali, kama ile ya Vitambulisho vya Taifa au Vitambulisho vya Kupigia Kura, ambayo taarifa za kila mtu aliyeandikishwa zipo.

Yaani kama kila mwanafunzi mwenye sifa ya kupata mkopo, ni lazima awe na Kitambulisho cha Taifa chenye taarifa zake muhimu zinazoweza kufuatiliwa hata baada ya kumaliza chuo.

Kama hatapatikana yeye, basi wazazi wake, ama walezi ama ndugu wengine walioorodheshwa kwenye taarifa hizo ili ajulikane baadaye anafanya shughuli gani na yupo wapi.

Hii itawezesha angalau kuwafikie wanufaika wengi tofauti na sasa.