Hakuna namna Ligi Kuu za Vijana ni muhimu kuanzishwa na kupewa kipaumbele

Na Charles Abel

Imepakiwa - Monday, May 13  2019 at  12:00

 

Hivi karibuni Serikali ya Uganda na Shirikisho
la Soka Uganda (Fufa) walizindua programu
maalumu ya mashindano ya mpira wa miguu
kwa shule za msingi nchini humo ijulikanayo
‘Odilo’.
Mashindano hayo yatafanyika katika nchi nzima
ya Uganda yakishirikisha wanafunzi
wanaosoma shule hizo ambao wengi wana umri
chini ya miaka 15.
Lengo la mashindano hayo ni kusaka vipaji vya
soka vyenye umri mdogo kutoka shule za
msingi nchini Uganda ambao wataandaliwa
vyema ili baadaye waje kuzitumikia timu za
Taifa kuanzia ile ya vijana wenye umri chini ya
miaka 17, 19, 20, 23 na ile ya wakubwa ya
Uganda.

Kuanzishwa mashindano hayo ni muendelezo
wa juhudi za Fufa za kuendeleza soka la vijana
ambalo ndilo limekuwa moyo wa maendeleo ya
mchezo huo katika nchi zote zilizopiga hatua.
Kabla ya kuanzishwa programu ya mashindano
hayo, kumekuwa na idadi kubwa ya michuano
ya soka ambayo imekuwa ikihusisha vijana
wenye umri mdogo nchini Uganda kwa muda
mrefu sasa.
Kuna mashindano ya soka kwa vijana wa shule
za sekondari, vyuo na taasisi za elimu, Copa
Coca Cola na Airtel Rising Stars ambayo
huhusisha vijana wenye umri chini ya miaka 15
na 17, pia kuna ligi ya vikosi vya vijana vya
timu zinazoshiriki Ligi Kuu.
Kupitia mashindano hayo, ni wazi Uganda
imevuna na inaendelea kuibua vipaji vya soka
vya wachezaji mbalimbali ambao wamegeuka
nguzo ya timu za Taifa za nchi hiyo kufanya
vyema kwenye mashindano mbalimbali ya
kimataifa ambayo yanashiriki.

Kuna kundi la nyota wa Uganda ambao ni zao la
mashindano hayo kama kina Emmanuel Okwi,
Farouk Miya, Allan Okello, Ssekisambu Erisa,
Khalid Aucho, Murshid Juuko, Hamisi Kiiza,
Moses Waisswa na wengineo.
Wengi wao waliibuka na kung’ara wakitokea
shuleni jambo ambalo lina faida kubwa kwao
kwani mbali na kucheza soka, wana faida
nyingine ya kuwa na elimu ambayo inawapa
msaada mkubwa katika maisha ya kisoka.
Moja ya faida ya mchezaji wa aina hiyo ni kuwa
na fikra na mtazamo mpana kuhusu mchezo wa
soka anaweza kuishi katika mazingira yoyote na
hilo linajidhihirisha kwa jinsi ambavyo
wachezaji wa Uganda wamekuwa wakiondoka
nchini mwao kila kukicha kwenda nje kucheza
soka la kulipwa.
Jambo hili linalofanywa na Uganda linapaswa
kuigwa na kutekelezwa hapa nchini kwa faida
na maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu

ambao bado haufanyi vizuri kulinganisha na
nchi nyingine.
Kama nchi ni vyema sasa tukaanza kutilia
mkazo soka la vijana kwa vitendo kupitia
programu mbalimbali ambazo tutazifanyia
uwekezaji mkubwa kama ambavyo Uganda
wanafanya ili tuweze kupata idadi kubwa ya
wachezaji bora vijana ambao watakuwa na faida
kwa nchi siku za usoni.
Kwa sasa tuna upungufu wa mashindano ya
soka kwa vijana jambo linalochangia tukose
idadi kubwa ya wachezaji waliopevuka mapema
ambao wanaweza kudumu na kuwa na mchango
kwa Taifa ndani ya kipindi kirefu kulinganisha
na wenzetu.
Kuna sababu ya kuimarisha mashindano ya
vijana kama vile yale yanayohusu timu ndogo
za klabu za Ligi Kuu zenye vijana wenye umri
chini ya miaka 20 lakini pia yale ya Shule za
Sekondari (Umisseta) na Shule za Msingi
Tanzania (Umitashumta).

Serikali inapaswa kuwekeza kwenye michezo
kama moja ya sekta ambayo inatoa ajira za
kutosha kwa watu kwa kushirikiana na TFF
katika kuhakikisha kunakuwa na mtaala bora na
walimu wazuri wa soka ambao watasaidia
kuzalisha wachezaji wenye viwango vya juu
shuleni, taasisi za elimu na vyuo.
Pia kuandaliwe utaratibu maalumu wa
kuwafanya wazazi kuwa chachu ya maendeleo
ya soka kwa watoto wao kwa kuwapa elimu ya
kuwajengea msingi bora ili kuwa na maendeleo
mazuri ya elimu na soka.
TFF inapaswa kutumia nguvu kubwa
kushawishi kampuni na taasisi kuweka nguvu
katika maendeleo ya soka la vijana kwa
kuanzisha mashindano ambayo yatashirikisha
timu na vituo vya soka kwa vijana wenye umri
mdogo.
Mashindano kama Copa Coca Cola na Airtel
Rising Stars yalikuwa chachu kubwa ya kuibua
vipaji vya soka ambavyo baadhi leo hii

vimekuwa tegemeo kwa timu ya Taifa Stars na
klabu mbalimbali.