http://www.swahilihub.com/image/view/-/5015330/medRes/2274137/-/4295hy/-/maana+pic.jpg

 

Hii ndiyo maana halisi ya kuwa mwanamke

 

Na  Florence Majani

Imepakiwa - Friday, March 8  2019 at  13:12

 

 Jeni John ameketi kwenye kiti chumbani kwake. Anajitazama kwenye kioo. Anautazama uzuri wake, umbile na gauni lake zuri.

Anaridhika mno anapojiona amekamilika kila ‘sekta’. Anaamini hilo linamtosha kuitwa mwanamke.

Hii ndiyo dhana ambayo baadhi ya wanawake wameibeba katika maisha yao. Wengine wamezaliwa na kuirithi kutoka kwa wazazi na wakaishi hivyo hadi kufa kwao. Baadhi wamefundishwa na ulimwengu na wakaishi hivyo hivyo wakiamini uzuri au ‘uanamke’ wao ndiyo msingi wa maendeleo.

Wakati leo tunaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, ni wakati wwa kutafakari nini maana halisi ya kuwa mwanamke.

Kaulimbiu ya mwaka huu kitaifa inasema, ‘Badili fikra kufikia usawa wa kijinsia, kwa maendeleo endelevu.’

Natamani wanawake wabadili fikra zao na waelewe kuwa mwanamke ni zaidi ya sura, mavazi yako na umbile lako. Ukiachia lile umbile la kibaolojia, mwanamke halisi ni yule aliye imara kihekima, kinidhamu, kiimani, kinadharia na kivitendo.

Mwanamke anahitaji kuelewa maana ya jina lake kwa kuwa tupo katika karne ambayo watoto wetu wa kike na kiume wanajifunza kutoka kwa wasanii maarufu wanaosifika kwa uzuri wao wa sura na maumbile.

Kutokana na hilo wanakuwa wakiamini uzuri wa sura na kuwa na wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii ndiyo msingi wa maendeleo kwa mwanamke.

Tunahitaji kupenyeza sindano za elimu kwa wanawake wote waelewe maana halisi ya kuwa mwanamke katika jamii ili kufikia hayo maendeleo endelevu. Maana ya mwanamke ni kuchukua nafasi muhimu katika jamii yake. Kama ni mechi ya mpira wa miguu basi anacheza nafasi ya beki, refa, kipa na kapteni wa timu. Mwanamke ana nafasi lukuki zinazomfanya awe mfano wa kuigwa , fahari ya mume wake, mshindi kwa jamii na nguzo kwa familia.

Wasomi na viongozi mbalimbali wametaja maana halisi ya kuwa mwanamke wa sasa.

Kwa mfano Jess Phillips, mwandishi wa kitabu cha Everywoman anasema, “Kuwa mwanamke ni kuwa kinara wa mabadiliko. Kusimama kwenye mabega ya wanawake werevu waliofanya vyema kabla yangu na kujifunza waliyotenda.”

Jess anaamini katika mabadiliko na kuiga yale yaliyofanywa na wanawake wengine kabla yake. Ina maana kwamba mwanamke anatakiwa kujaribu kuleta mabadiliko katika jamii yake badala ya kuharibu, kufarakanisha na kutumia nafasi yake vibaya.

Mabadiliko haya si lazima yawe makubwa kama yale ya wanawake maarufu duniani kwa mfano; Oprah Winfrey au Maya Angelou hata ukarimu wako kwa wageni, ni muhimu kwa jamii yako na hakika unaweza kukufanya uwe wa kukumbukwa milele.

Mwanamke halisi ni yule anayejitoa kwa jamii wakati wa matukio muhimu. Je, wanawake wa sasa wanatumia vipi matukio hayo kuonyesha ukarimu na umahiri wao?

Kwa mfano, Florence Nightangle alikuwa muuguzi huko Uingereza. Wakati wa Vita Kuu vya Pili ya Dunia alitumia taaluma ya uuguzi kuwatibu majeruhi wa vita nchini Uingereza, wakati huo vita vilivyojulikana kama Crimean War.

Huduma yake ilisaidia kupunguza vifo vya wanajeshi wakati huo. Mpaka leo, Nightangle anakumbukwa kwa huduma yake. Je, wewe umeifanyia nini jamii kwa kutumia taaluma yako?

Kwa upande wake Rosette Pambakian, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Comms at Tinder ya Marekani anasema, “Wanawake wa sasa wanatakiwa wajue kuwa kuwasaidia wanawake wengine kufikia ndoto zao ni muhimu kama ilivyo kuyafikia mafanikio yao wenyewe.”

Pambakin anasema kama tunataka mabadiliko katika jinsia ili wanawake na wanaume wawe na fursa sawa, ikiwamo mishahara na ajira, ni lazima wanawake wawe tayari kusaidia wanawake wenzao. Maneno ya Pambakin yana tija. Je, ni wangapi katika tasnia zao wamewahi kuwashika mkono na kuwaelekeza wanawake wengine ili kufikia maendeleo?

Uzuri wako wa sura na umbile lako zuri halitasaidia iwapo utakuwa na roho ya kutu kwa wenzako. Muonekano huo hauna maana iwapo hauna maadili mazuri kwenye jamii.

Si sura wala umbile vitakavyomsaidia mwanamke kuwa na familia yenye watoto wenye nidhamu la hasha, bali malezi mema. Si kibarua chepesi kuwa mwanamke wa kweli, ni zaidi ya sura yako. Ni vita, hekima, nidhamu, akili, na zaidi ya yote, Mungu awe kiongozi wako.

Frolence Majani ni mwanahabari anayefanya kazi katika Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa). Anapatikana kwa simu namba 0715-773366