http://www.swahilihub.com/image/view/-/5015342/medRes/2274164/-/adn80c/-/ukwaju+pic.jpg

 

Hii ndiyo raha ya kunywa juisi ya ukwaju

 

Na Hadija Jumanne, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, March 8  2019 at  13:19

 

Ukwaju ni tunda lenye faida nyingi katika mwili ikiwamo afya na urembo.

Scolastica Mlinda ni mtaalamu wa lishe kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), anasema ukwaju husaidia watu kupata choo, lakini pia tunda hilo lina vitamin C, ambayo ni nzuri kwa afya ya binadamu.

Anasema sifa kubwa ya ukwaju ni kutibu matatizo ya nyongo, huondoa tatizo la mtu kuvimba lakini husaidia kuua minyoo tumboni (kwa watoto wadogo).

Unywaji wa juisi ya ukwaju iliyochangaywa na pilipili manga, hiliki, mdalasini au tangawizi husaidia mtu kupata hamu ya kula.

Anasema ukwaju pia ni chanzo cha vitamin B na husaidia kuongeza nguvu na uchangamfu mwilini, hutibu kuwashwa kwa koo na homa ya manjano.

Mtaalamu huyo anasema ukwaju husaidia kumeng’enya chakula, kurahisisha choo, hushusha joto la mwili na huondoa homa.

Wataalamu wa afya wanasema nywaji wa glasi moja ya juisi ya ukwaju kwa siku, huleta matokeo mazuri kwa afya mwili.

Pia, hulinda mwili dhidi ya mafua, hupunguza wingi wa lehemu na kuimarisha afya ya moyo.

Katika urembo; ukwaju husaidia kung’arisha ngozi na kuwa nyororo, huondoa weusi kwenye shingo na kutibu chunusi kwa kupaka sehemu hizo.

Pia, husaidia kuzuia kukatika kwa nywele, husaidia kutibu ngozi yenye mafuta na huponya ngozi iliyoungua na yenye vidonda kwa kupaka juisi ya ukwaju (isiyo na sukari) katika sehemu hizo na kuacha ikauke kwa muda wa dakika 20 kisha unaosha na maji ya uvuguvugu.

Makala haya yameandikwa na mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Hadija Jumanne anayepatikana kwa barua pepe; hjumanne@mwananchi.co.tz