Hongera Mkuchika, tabia hii sasa ikome

Imepakiwa - Wednesday, April 17  2019 at  11:22

 

Juzi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika alisema wakuu wa mikoa (ma-RC) na wilaya (DC) watakaowaweka watu ndani kinyume cha sheria, watashtakiwa wao binafsi na hawatatetewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Akijibu baadhi ya hoja bungeni zilizoulizwa na wabunge katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Mkuchika alisema tayari AG amekwishatoa waraka kuelezea juu ya dhamira hiyo na kwamba, iwapo ma-RC na DC wataziba pamba masikioni, basi wanaowaweka ndani watawashtaki wao binafsi na si kwa vyeo vyao.

Hii ni hatua njema kwani licha ya Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 kuwapa mamlaka ma-DC na RC kuwaweka kizuizini watu kwa saa 48 wanaoonekana kutenda kosa la jinai au kuvunja amani, baadhi yao wamekuwa wakiitumia kinyume chake.

Kifungu cha 7(5) cha sheria hii kinasema ni lazima mkuu wa mkoa au wilaya anayemuweka mahabusu raia aandike maelezo ni kwa nini amemuweka ndani, lakini inaelezwa kuwa baadhi yao wamekuwa hawafanyi hilo na hivyo hatua yao ya kuwaweka ndani watu kutafsirika sawa na kuwakomoa.

Mwishoni mwa Januari, Rais John Magufuli aliwaonya wakuu wa wilaya na mikoa wanaoendekeza tabia ya kuwaweka mahabusu wananchi wakiwatuhumu kufanya mambo wasiyoyapenda.

Rais Magufuli alionya kuwa tabia hiyo imekuwa ikilalamikiwa, lakini pia imekuwa ni kero kwa sababu viongozi hao hata pale ambapo wangetumia busara tu kuzungumza na wahusika, wao wamekuwa wakitumia mamlaka yao kuwaweka ndani kwa saa 48 bila sababu za msingi.

Rais Magufuli hakuwa kiongozi wa kwanza katika utawala wake kuwaonya ma-DC na RC juu ya tabia hiyo, bali wasaidizi wake akiwamo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wamekwishaonya mara kadhaa. Mbali na hao, wapo mawaziri wengine ambao pia walionya kuhusu hatua hizo na baadhi ya tuhuma za waliowekwa ndani wakizitaja kuwa ni nyepesi zisizohatarisha amani wala usalama katika maeneo wanayoyaongoza kama sheria inavyotaka.

Mara kadhaa tumeandika katika safu hii tukionya kukiukwa kwa misingi ya utawala bora na wakuu hao wa wilaya na mikoa, kwani matukio mengi tuliyoyashuhudia tunapoyatafsiri kulingana na sheria inayowapa mamlaka, hayakubaliki kisheria.

Hata unapotafakari matukio mengi ambayo wakuu hao wamehusika nayo kwa kuwaweka watu ndani, huoni mantiki ya uzito wa makosa yaliyofanywa kiasi cha hatua hiyo kubwa kufikiwa dhidi ya wahusika.

Mathalani, hivi mtu aliyemilikishwa shamba kwa njia zisizo sahihi anawekwaje ndani? Ni usalama na amani gani aliyotishia mpaka akamatwe na kuwekwa mahabusu badala ya kushtakiwa mahakamani?

Kama tulivyowahi kusema katika safu hii, matumizi mabaya ya sheria hii yanaweza kusababisha watu wengi hasa wanyonge, wasio na nafasi au wasio na madaraka kunyanyasika na kukosa amani.

Wakati tunamshukuru waziri Mkuchika kwa kuweka wazi kuwa sasa viongozi watakaoitumia vibaya sheria hii watabanwa wao binafsi, ni vyema wananchi watakaoonewa wasibaki kulalamika na kunung’unika mioyoni, bali wachukue hatua stahiki dhidi ya wakuu wa wilaya au mikoa watakaoingilia haki zao.

Ni vyema misingi ya demokrasia na utawala bora ikaheshimiwa na kila mmoja katika nafasi yake.