Hongera Taifa Stars,hongera Watanzania

Imepakiwa - Tuesday, March 26  2019 at  09:31

 

Hongera Taifa Stars, hongera Watanzania. Ndiyo maneno yanayoweza kubeba ujumbe tulio nao kwa wachezaji na Watanzania wote baada ya timu ya taifa ya soka kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 2019 nchini Misri.

Tanzania iliishinda Uganda kwa mabao 3-0 katika mechi ya mwisho ya Kundi L la michuano hiyo iliyofanyika Uwanja wa Taifa. Kwa matokeo hayo, Tanzania imeshika nafasi ya pili ikiwa na pointi nane na hivyo kuungana na Uganda yenye pointi kumi.

Lesotho na Cape Verde, ambazo pia zilikuwa zina matumaini ya kusonga mbele zimetolewa baada ya kutoka sare ya bila kufungana mjini Praia. Lesotho imemaliza ikiwa na pointi sita na Cape Verde popinti tano.

Kwa ushindi huo, Taifa Stars inaungana na Burundi, Uganda na Kenya kuingia fainali hizo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mataifa manne ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufuzu kwa pamoja.

Mafanikio hayo yamekuja baada ya miaka 39 ya kujaribu bila mafanikio kufuzu baada ya kufanya hivyo kwa mara ya mwisho mwaka 1980 wakati fainali hizo zilipofanyika nchini Nigeria kwa kushirikisha mataifa nane tu.

Kwa kuwa ni muda mrefu umepita tangu tupate fursa hiyo, ni muhimu kuwapongeza wachezaji, walimu, viongozi wa timu na wote waliochangia kufikia mafanikio hayo.

Hatua iliyofikiwa ni kubwa kwa kuwa wakati Tanzania ikifuzu, zipo nchi kadhaa tena zenye majina makubwa katika soka na zilizowahi kushiriki mashindano hayo, zimekwaa kisiki na hazitashiriki.

Bila shaka ushindi uliofikiwa ulitokana na mambo mengi kama maandalizi, ushirikiano, programu za muda mrefu na mfupi, ari ya wachezaji na hamasa ya Watanzania kuiunga mkono timui nyao wakati wote.

Tunajua kuwa kufuzu kucheza fainali hizo ni jambo moja, na kufanya vizuri kwenye fainali hizo ni jambo nyingine. Kwa kuwa tayari tumeshafuzu, sassa tunatakiwa kuanza mikakati kabambe ya kujiandaa kushiriki fainali hizo zitakazofanyika mwezi Juni.

Katika fainali hizo kuna timu zinazojulikana kuwa ni vigogo ambazo zina wachezaji nyota wanaosakata soka barani Ulaya na Asia, na hata zile ambazo si vigogo zitajiandaa vizuri kuhakikisha zinafanya vizuri, hivyo hakuna shaka kuwa yatakuwa mashindano magumu.

Hata hivyo, wanasema hakuna lisilowezekana katika soka ili mradi timu inafanya maandalizi ya kutosha na sahihi, hivyo mipango inatakiwa ianze sasa.

Mfano wa maandalizi hayo ni pamoja na Shirikisho la Soka (TFF) kupanga mambo yake kuhakikisha kunapatikana muda wa kutosha kuiandaa timu, kama kumaliza mapema mashindano ya ndani kwa ajili ya kuwezesha wachezaji kujiunga na timu kwa ajili ya maandalizi.

Pia kutafuta mapema mechi za kirafiki kulingana na mahitaji ya kocha na kufanya mikakati ya kuhakikisha unapatikana usafiri nafuu utakaowawezesha Watanzaniua wengi kwenda Misri kuishangilia timu yao, huku ikishirikiana na ubalozi wetu kuhamasisha wale wanaoishi au kusoma nchimi humo kuipa timu nguvu.

Pia wachezaji hawatakiwi kuridhika na kiwango chao, bali kuhakikisha wanaendelea kujitunza ili muda wa mashindano utakapokaribia, kocha aweze kuteua wale ambao alikuwa nao wakati wa kufuzu na kuongeza wachache kuziba mapengo ya majeruhi.

Wadau wengine pia hawana budi kuiunga mkono TFF katika maandalizi hayo, kuhakikisha inapata kile inachohitaji kufanikisha maandalizi na ushiriki wa timu na mashabiki kwa ujumla.

Kipindi hiki ni kigumu kuliko tulichopitia na hivyo tusipojiandaa vizuri tunaweza kupata fedheha itakayozidi furaha ya kufuzu.