Hukumu hii itukumbushe nafasi ya viranja shuleni

Na  Phinias Bashaya, Mwananchi

Imepakiwa - Tuesday, March 19  2019 at  10:14

Kwa Muhtasari

 

 

Viongozi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kibeta, ni miongoni mwa mashahidi tisa upande wa Jamhuri waliofika Mahakama Kuu kuongeza uzito kwenye shtaka la mauaji ya kukusudia dhidi ya walimu walioshtakiwa kwa kosa kwa kumuua kwa makusudi mwanafunzi Sperius Eradius .

Pamoja na kuwa tukio la kumuadhibu Sperius na kusababaisha kifo lilishuhudiwa na wanafunzi wengi, ni wanafunzi wawili pekee waliosajiliwa kwenye orodha ya mashahidi upande wa Jamhuri ambao ni dada na kaka mkuu.

Mbali na nafasi yao kama wanafunzi, katika hatua hii walitakiwa kubeba jukumu la kiuongozi na kuileza mahakama ni hatua ipi walichukua kama viongozi wa wanafunzi wakati wa tukio la Sperius kupiga kelele ya kuomba msaada wakati likiendelea.

Katika hukumu iliyosomwa na Jaji Lameck Mlacha na kumtia hatiani mwalimu Respicius Mutazangira, aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa na kumwachia huru Heriet Gerald, ilisema ushahidi wa wanafunzi hao ulikuwa thabiti.

Jaji wakati akiisoma alikuwa akijibu hoja ya upande wa utetezi uliotaka ushahidi wa wanafunzi hao utiliwe shaka.

Upande huo ulidai kwamba mtu kuwa eneo la uhalifu haithibitishi kuwa naye ni mhalifu na walikuwa na kauli kinzani kuhusu eneo mwalimu Heriet alipompiga viboko mwanafunzi huyo.

Hatua ya wanafunzi hao kusimama kizimbani kutoa ushahidi dhidi ya walimu wao na hukumu iliyofuata vinakumbusha umuhimu na uzito wa nafasi zao kama viongozi wa wanafunzi na kwamba, kuna wakati wa kuwajibika kwa nafasi zao.

Kama hivi ndivyo, viongozi wa wanafunzi wanatakiwa kushirikishwa hatua zote zinazohusiana na masuala yaliyozunguka shule yao na kuruhusu sauti zao kusikika kwenye vikao vya walimu na kamati za shule.

Viongozi hawa ‘watoto’ wanafahamu mambo mengi yanayohusu kero zinazolalamikiwa na kundi wanaloongoza na pengine hata sababu za baadhi ya walimu kupewa majina bandia na wanafunzi kulingana na tabia zao.

Hata kabla ya kusimama kizimbani, inawezekana viongozi hao walikuwa wanafahamu mengi kuhusu mwalimu aliyehukumiwa, lakini hawakuwa na jukwaa la kufikisha malalamiko waliyosikia kutoka kwa wanafunzi wanaowaongoza.

Kutokana na muundo wa kamati za shule ulivyo, hakuna upenyo unaotoa nafasi kwa viongozi wa wanafunzi kuzungumza kwa niaba ya wenzao na kueleza malalamiko wanayotoa wanafunzi dhidi ya walimu wao.

Ni katika shule hii ya Kibeta ambayo wakati wa zamu ya mwalimu Respicius Mutazangira, wanafunzi walilazimika kuamka mapema zaidi kuliko kawaida ili kuwahi shuleni.

Kwa wanafunzi wengi ilikuwa bora mtu arudi nyumbani kuliko kumkuta mwalimu huyo akiwa amewahi shuleni.

Aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya shule lakini ikavunjwa, Methodia Method aliwahi kulalamikiwa katika kikao cha wazazi na madai hayo yalikosa nguvu kwa madai mwalimu wa nidhamu ndiye sababu ya kulaumiwa.

Pengine kama muundo wa kamati ungekuwa unaruhusu uwakilishi wa wanafunzi, haya yangejulikana mapema kwamba wanafunzi wanaogopa kuamka usiku wakati wa zamu za mwalimu huyo na hata kutoa mapendekezo yao.

Wanafunzi wana uwezo wa kusimama na kuzungumzia changamoto kupitia kwa viranja wao wakiwamo kaka na dada mkuu. Na hii ni kama watapewa nafasi. Pale walimu na kamati wanapaomua kwa niaba ya wanafunzi, ni mwanzo wa kukaribisha migomo, chuki, ulipizaji visasi na uharibifu wa mali.

Siku moja baada ya kifo cha Sperius wanafunzi walikusanyika shuleni na kugoma kuingia madarasani.

Mgomo wa aina hii hauwezi kuzimwa na mwalimu mkuu au kikosi cha polisi na mabomu, bali na viranja wakuu ambao wanajua lugha ya wanafunzi wenzao ambao kimsingi ni miongoni mwao.

Baadhi ya shule nchini zimewahi kukumbwa na migomo na uharibifu wa mali ambao hutokea baada ya walimu na kamati kutoa uamuzi wa mambo yanayowahusu wanafunzi bila kutoa nafasi ya wao kusikika kupitia kwa viongozi wao.

Wajibu wa viongozi wa wanafunzi ni zaidi ya kusimamia shughuli za usafi shuleni.

Hawa ni viongozi ambao sauti zao zinatakiwa kuchukua nafasi kwenye vikao vya walimu na kamati za shule ili kujibu sehemu ya changamoto za kundi hilo.

Phinias Bashaya ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Kagera 0767489094