http://www.swahilihub.com/image/view/-/4567790/medRes/1976942/-/o9rcfdz/-/aisi.jpg

 

Iceland: Nchi ambayo amani imedumu kwa kipindi kirefu

Gudni Thorlacius Johannesson

Rais wa Iceland, Gudni Thorlacius Johannesson akiwa na mkewe Eliza Jean Reid wawasili katika ukumbi wa Finlandia, Helsinki, Finland Mei 16, 2018. Picha/AFP 

Na SAMMY WAWERU na MASHIRIKA

Imepakiwa - Friday, May 18  2018 at  09:46

Kwa Mukhtasari

Iceland ni nchi ambayo amani imedumu kwa kipindi kirefu, kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Biashara na Amani ya Australian Think-Tank ya 2017.

 

KWA mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Biashara na Amani ya Australian Think-Tank ya 2017, nchi tano ziliorodheshwa kuwa zilizoshamiri amani duniani.

Nchi hizo zilikuwa Aisilandi (Iceland), Nyuzilandi (New Zealand), Ureno (Portugal), Austria na Denmark.

Aisiland ndiyo iliongoza katika orodha hiyo.

“Amani imetawala Aisilandi tangu 2008,” ikadokeza ripoti hiyo.

Maswala yaliyozingatiwa na utafiti wa taasisi hiyo ulioendeshwa kati ya 2008 hadi 2017, yalikuwa visa vya uhalifu, mashambulizi ya kigaidi, kuimarika kwa kiwango cha uchumi, ghasia, ukiukaji wa haki za kibinadamu, uwiano na utangamano miongoni mwa raia, na mengine muhimu.

Utafiti huo ulionesha mataifa 93 yaliimarisha amani, huku 68 yakidorora kwa sababu ya visa vya ugaidi. Hata hivyo, taasisi hiyo ilidokeza kuwa kiwango cha amani duniani kiliimarika kwa asilimia 0.28. Mwanya kati ya nchi zenye amani na zinazoshuhudia utovu wa kukithiri kwa visa vya ugaidi, unaendelea kupanuka.

Mabadiliko madogo yalishuhudiwa katika nchi zinazokumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya kigaidi kama Syria, Afghanistan, Iraq, Sudan Kusini na Yemen.

Aisilandi, taifa lililoongoza kwa ukwasi wa amani ni taifa la aina gani?

Ni nchi ya Ulaya ambayo ni kisiwa kilichozungukwa na Bahari ya Atlantiki, Kaskazini. Aidha, iko kilomita 300 kutoka Greenland, upande wa Magharibi na kilomita1000 kutoka Norwei, upande wa Mashariki. Aisilandi ilitokana na asili ya kivolkeno. Ina ukubwa wa kilomita 103, 000 na kukadiriwa kuwa na watu 300, 000 pekee.

Hali ya hewa ya nchi hiyo ni baridi, na barafu zinafunika sehemu kubwa hasa nyanda za juu ambazo ni baridi mno, hivyo basi hakuna mimea. Watu wanapatikana Pwani yake.

Kusini mwa kisiwa hicho, volkeno husababisha kuwepo kwa maji ya moto mahali kwingi. Raia wa nchi hiyo wanapenda kuogelea nje katika mabwawa hata wakati wa theluji kwenye maji moto kutokana na joto la kivolkeno.

Joto linaloshuhudiwa hutumika kufanya kilimo, na hupasha moto nyumba za vioo na kuwezesha mimea kuzaa matunda misimu yote ya mwaka wote, hata wakati wa baridi kali. Ni kufuatia hali hiyo ambapo Aisilandi inavuna ndizi na machungwa yake.

Kujitawala

Wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia (WWII), Aisilandi ilipoona Denmark imevamiwa na Ujerumani, iliamua kujitenga kama kisiwa, na ikajitawala kabisa.

Mnamo 1944, nchi hiyo ilipata uhuru kamili.

Baada ya vita kwisha, Aisilandi ilijisajili kuwa mwanachama wa muungano wa NATO lakini kufikia leo haina wanajeshi.

Ilifanya mkataba na Marekani kuwa Waamarekani wapewe haki ya kutumia kituo cha ndege kisiwani humo ili iwatetee.

Karibu watu wote wa Aisilandi ni Waskandinavia wanaowakilisha asilimia 92.62, na wanaosalia ni Wapolandi.

Waziri Mkuu wa Aisilandi ni Bw Sigurdur Ingi Johannsson. Alichukua hatamu za uongozi Aprili 2016 baada ya kujiuzulu kwa Sigmundur David Gunnlaugsson aliyeshinikizwa kuchukua hatua hiyo kufuatia kuhusishwa kwake na kashfa ya ukwepaji kodi.

Ufichuzi wa kashfa hiyo ulitolewa na kampuni moja ya kisheria nchini Panama, Mossack Fonseca.

Ilidaiwa kuwa Gunnlaugsson anamiliki kampuni ya Wintris yeye pamoja na mkewe, na kwamba hakuweka wazi umiliki huo baada ya kujiunga na bunge la nchi hiyo.

Alituhumiwa kuficha mamilioni ya dola na mali zinazomilikiwa na familia yake.

Hata hivyo, alipinga kuhusishwa na madai hayo.

Kujiuzulu kwake kulitokana na shinikizo la mamia ya watu walioandamana mbele ya ofisi yake wakimtaka ang'atuke.

Rais wa Aisilandi ni Gudni Johannesson aliyemrithi Olafur Ragnar Grimsson 2016 ambaye amekuwa mamlakani tangu mwaka wa 1996.