http://www.swahilihub.com/image/view/-/4929032/medRes/2220951/-/12ct2l5z/-/richard.jpg

 

JNIA yakumbwa na kashfa ya wizi

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Richard Mayongela  

Na Bakari Kiango, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  12:50

Kwa Muhtasari

Matukio hayo yatachunguzwa na ikibainika ukweli wahusika watawajibishwa.

 

bkiango@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baadhi ya watumiaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wamedai kumekuwapo tabia ya wizi wa vifaa vya abiria kwenye mabegi uwanjani hapo.

Walitoa madai hayo juzi wakati wakichangia andiko la msanii nyota wa filamu nchini, Vincent Kigosi ‘Ray’ aliyeposti kwenye akaunti yake ya Instagram yenye jina la raythegreatest akidai kuibiwa vifaa mbalimbali ikiwamo viatu katika begi lake wakati akielekea Dubai.

Nyota huyo aliyecheza filamu mbalimbali ikiwamo ‘Fake Pastor’ na ‘Tajiri mfupi‘ alitoa malalamiko hayo juzi kupitia akaunti hiyo kwa kuandika “Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar es Salaam kuna tabia mbaya sana ya kuiba vitu vya abiria vilivyopo kwenye mabegi yao.”

“Wiki iliyopita mliniibia raba pamoja na pafyumu (mafuta ya manukato), sasa swali langu? Kwa nini uongozi hauwachukulii hatua kali hao wafanyakazi wenu wenye tabia ya udokozi wanaoharibu sifa ya uwanja wa ndege huu wa kimataifa?” alihoji.

Mmoja wa wachangiaji ambaye ni msanii mwenzake mwenye jina la @Gabozingamba aliandika “Wakati tunakwenda Kigali (Rwanda) nilikuambia wameniibia laptop (kompyuta mpakato) na manukato wamezuia ukaniambia tulia dogo ndiyo ukubwa. Basi na wewe utulie kaka ndiyo uzee huo kumradhi.”

Kwa upande wake @Queen_tee chokala akichangia andiko hilo, alidai kuwa kuna raia wawili wa kigeni waliibiwa simu mbili na kompyuta mpakato na kuwataka wahusika kubadilika kuhusu hali hiyo.

Naye @lukuwielizaberth aliwashauri waliokumbwa na mkasa huo kutoa taarifa sehemu husika na siyo katika mitandao ya kijamii ili tatizo hilo lishughulikiwe kwani JINA kuna kamera za ulinzi.

Akizungumzia madai hayo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Richard Mayongela alianza kwa kuhoji: “Hivi mtu ukiibiwa nyumbani kwako unaweza kukimbilia au kulalamika kwenye mitandao ya kijamii? Si unakwenda kwenye vyombo vya dola kutoa taarifa, alichokifanya si kitendo kizuri pale uwanja wa ndege kuna vyombo vya usalama kwa nini asitoe taarifa.

Alisema matukio hayo yatachunguzwa na ikibainika ukweli wahusika watawajibishwa.