http://www.swahilihub.com/image/view/-/2840302/medRes/1097628/-/d8hx0l/-/DNCOURTNGANGA2008j.jpg

 

Mchungaji James Maina Ng'ang'a: Ametajwa kwa utata hapa na pale

Pasta James Ng'ang'a

Pasta James Ng'ang'a wa Kanisa la Neno Evangelism katika Mahakama ya Limuru Agosti 20, 2015 wakati wa kusikizwa kwa mashtaka dhidi yake ambapo anadaiwa kusababisha kifo cha Bi Mercy Njeri kupitia uendeshaji mbaya wa gari, kukosa kuripoti ajali na kutoa habari za kupotosha. Picha/GERALD ANDERSON 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, May 15  2018 at  06:59

Kwa Muhtasari

Mchungaji James Maina Ng’ang’a wa kanisa lake la Neno  Evangelism lililopo jijini Nairobi kwa sasa yuachambuliwa kwa kina kutokana na hali kwamba amehusishwa na ajali ya barabarani iliyosababisha kifo cha mwanamke.

 

MCHUNGAJI James Maina Ng’ang’a wa kanisa lake la Neno  Evangelism lililopo jijini Nairobi kwa sasa yuachambuliwa kwa kina kutokana na hali kwamba amehusishwa na ajali ya barabarani iliyosababisha kifo cha mwanamke.

Ng'ang'a alishtakiwa na akaachiliwa huru na mahakama ya Limuru.

Huyu ambaye hukiri kuwa utotoni mwake umasikini ndiyo ulikuwa suti yake ya kimaisha na ambapo katika harakati zake za kujinasua aliishia kukumbana na vifungo gerezani, kwa sasa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i ametoa amri kuwa rufaa ikatwe dhidi ya hukumu hiyo ya kumwondolea lawama Askofu Ng’ang’a.

Akifahamika kwa mahubiri yake ya madoido, mbwembwe na madai ya kutekeleza miujiza na kudai upanzi wa hela mkobani mwake kama sadaka, alizindua kanisa lake mwaka wa 1992.

Amejipata huru mikononi mwa hakimu Godfrey Oduor na ambapo Matiang’i anashikilia kuwa "mchungaji huyu tunaamini kuwa alitekeleza kosa kuu la mauaji kupitia uendeshaji wa gari kiholela na kamwe hakuna nafasi ya kutuhimiza tukubaliane na uamuzi huo wa mahakama".

Hakimu aliamua kuwa upande wa mashtaka haukutoa ushahidi wa kutosha kumhusisha Askofu Ng’ang’a na mauaji ya Mercy Njeri katika barabara kuu ya Naivasha hadi Nairobi katika eneo la Manguo katika ajali ya Julai 26, 2015.

Aliaminika kuwa yeye ndiye alikuwa anaendesha gari lake la kifahari aina ya Range Rover lakini baada ya mauti hayo, akajitoa eneo hilo haraka na akamwachia dereva wake gari hilo ili ionekane kana kwamba dereva huyo ndiye aliyesababisha ajali hiyo.

Kukazuka sokomoko nchini, maandamano na mito ya kukamatwa kwake na presha ilipozidi, maafisa wawili wa polisi wakasimamishwa kazi na pamoja na dereva yule wa Askofu Ng’ang’a, kwa pamoja wakaandaliwa mashtaka katika mahakama ya Limuru.

Sasa uamuzi wa wananchi hasa katika mitandao ya kijamii ndio huo na wa mahakama ndio huo, hukumu ya Mungu ikibakia kujidhihirisha.

Askofu huyu ameorodheshwa miongoni kwa wakwasi kupindukia na ambapo kanisa lake katika barabara ya Haile Sellasie na ambalo liko katikati mwa vituo viwili vya Petroli, vyote kwa ukadiriaji vikiwa ni uwekezaji wa zaidi ya Sh100 milioni.

Mwaka wa 2012, Ng’ang’a alikuwa mahakamani kufuatia kisanga cha mzozo wa kindoa na ambapo katika sokomoko la kesi, mwanamke husika alitangaza kuwa Ng’ang’a huishi katika mtaa wa Karen akiwa na magari kadhaa ya kifahari na jumba la kutamanika.

Wakati Swahilihub ilimpigia simu katika maandalizi ya makala haya, Ng’ang’a alisema: “Usijali ndugu yangu na masaibu haya yangu. Nimepitia mengi, nikavuka mengi na hata kwa hili usiwe na shaka nitaibuka mshindi kwa kuwa nafsi yangu iko wazi kuwa sikuhusika katika ajali hiyo wala katika matukio mengine mengi ambayo jnimeandaliwa ya kuangamiza bidii yangu.”

Changamoto za ushindani

Ng’ang’a alisema kuwa mahasidi wake ni wengi sawa na jinsi kazi ya Mungu huingiwa na changamoto za ushindani wa mvuto wa shetani akijaribu kutekeleza hujuma.

Kwa sasa amemuoa Bi Loise Murugi Maina baada ya mauti kwa bibi yake wa kwanza aliyejaliwa watoto wanne katika ndoa hiyo.

Harusi yake ya pili ilifanyika katika Mkahawa wa Windsor kukiwa na ulinzi na urembeshaji mkuu mwaka wa 2012.

Kalonzo Musyoka alikuwa mgeni wa heshima katika harusi hiyo.

Raha kidogo ndani ya ndoa na hatimaye kukazuka kezi mahakamani ambapo kidosho huyu anasaka usaidizi wa kisheria kumshinikiza Pasta huyu awajibikie malezi ya mtoto wao akikiri katiika stakabadhi zake mahakamani kuwa “Ng’ang’a ni mkorofi, mwingi wa dhuluma na mlevi.”

Katika kezi hiyo, anadai kitita cha Sh535,000 kila mwezi, akisema kuwa “huyu kwake hizo ni pesa nane kwa kuwa ukwasi wake ni wa kimaajabu”.

Naye akijibu, Ng'ang’a anasema kuwa mwanamke huyu ni tapeli wa kindoa katika boma lake ambaye hata ametoroka bila ya kumfahamisha sababu kwa hivyo akifaa kuorodheshwa kama mtoro wa kindoa wala sio mwaathiriwa wa dhuluma.

Ni mengi ambayo yako katika stakabadhi hizo na ambayo hakuna maana ya kuyapa mkazo hapa kwa kuwa hayo ni yao na uamuzi ni wa mahakama ambako wameamua kulumbania.

Kwa uhakika, kilio kwa masikini, kilio kwa matajiri, misukosuko kwa wote na huku maana kamili ya maisha na nini hasa huzua utulivu ikibakia kuwa kitendawili cha kuteguliwa.