Jeshi la Polisi iwe linatoa majibu ya maswali ya wananchi

Kikosi maalumu cha jeshi la polisi kikionyesha ukakakamavu wa utekelezaji wa majukumu yao 

Imepakiwa - Wednesday, March 6  2019 at  11:22

 

 Utendaji wa Jeshi letu la Polisi umeguswa kwa mara nyingine. Mara hii aliyeligusa ni Rais wa nchi, ambaye katika hotuba yake juzi alizungumzia namna ambavyo uchunguzi wa baadhi ya matukio ya kihalifu unavyoacha maswali kwa Watanzania.

Tunajua kwamba jeshi letu linafanya kazi nzuri, tena iliyotukuka katika mambo mengi. Hata hivyo yapo matukio ambayo kwa hakika yanahusiana na uhalifu yaliyopaswa kuwa tayari na majibu muafaka kwa wananchi, lakini ama yalichelewa au kukosa majibu.

Juzi wakati akiwaapisha mawaziri wawili Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais John Magufuli alitumia mfano wa tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed ‘Mo’ Dewji lilivyoacha maswali hadi sasa, licha ya kwamba lina zaidi ya miezi mitano tangu lilipotokea. Mo alitekwa Oktoba 11, mwaka jana saa 11:00 alfajiri akiwa Hoteli ya Collesum iliyopo Barabara ya Haile Selassie, Oysterbay jijini Dar es Salaam alikokwenda kufanya mazoezi ya viungo. Mfanyabiashara huyo alipatikana Oktoba 20 eneo la Gymkhana katikati ya jiji hilo.

Katika hotuba yake hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa ilizungumzia utendaji wa jeshi hilo, Rais alilipongeza kwa kazi nzuri linayoifanya ambayo nasi tunaiona na kuungana na kiongozi huyo mkuu wa nchi kulipongeza jeshi hili lililokabidhiwa jukumu la kuhakikisha usalama wa maisha na mali za wananchi.

Hata hivyo, Rais Magufuli aligusia namna ambavyo jeshi hilo limekuwa likiacha maswali mengi bila majibu katika uchunguzi wa baadhi ya matukio, akilitaja tukio la Mo kuwa miongoni mwa matukio hayo. Katika hotuba hiyo alihoji mambo kadhaa kuhusiana na tukio hilo ambayo hata gazeti hili miongoni mwayo limewahi kuhoji, ikiwemo kwa nini hadi sasa baadhi ya watuhumiwa waliotajwa na jeshi hilo hawajafikishwa mahakamani.

Vilevile kiongozi huyo alihoji iweje waliomteka mfanyabiashara huyo walimrejesha na kumtelekeza katikati ya jiji huku gari walilolitumia wakiliacha sehemu hiyo, tena ndani yake likiwa na silaha ilhali walikuwa wakisakwa, na kuhoji iwapo wangejikuta katika makabiliano na polisi baada ya hapo wangefanyaje.

Rais Magufuli alisema zipo kasoro katika utendaji wa polisi na kuwatahadharisha kuwa Watanzania sasa wanaelewa na wanahoji masuala mengi. Alisema tukio hilo limeacha maswali mengi ambayo yanahitaji majibu na Watanzania si wajinga.

Yapo matukio mengi ambayo jeshi letu la polisi bado linadaiwa majibu na Watanzania yatakayokata kiu yao. Miongoni mwayo ni ya baadhi ya watuhumiwa kudaiwa kufa wakiwa mikononi mwa polisi na kutoweka kwa mwandishi wa habari wa Mwananchi, Azory Gwanda mwaka juzi wilayani Kibiti mkoani Pwani.

Mengine ni kutekwa kwa Idrissa Ally (13), Septemba 26, 2018, kutoweka kwa kada wa Chadema, Ben Saanane Novemba 2017 na pia shambulio la risasi la Septemba 7, mwaka huo dhidi ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.

Si hayo tu, lakini jeshi letu limekuwa likilalamikiwa katika baadhi ya maeneo kutokuwa na huduma nzuri kwa wateja ambao ni wananchi ikiwamo watuhumiwa kushikiliwa vituoni muda mrefu bila kufikishwa mahakamani.

Wakati tunaamini kauli ya Rais aliyoitoa juzi kuwa ni agizo kwa Jeshi la Polisi kuitekeleza, tunalisihi jeshi hilo pia liwe na utamaduni wa kutoa majibu ya maswali ambayo Watanzania hujiuliza pindi matukio yatokeapo ili kuwajengea imani katika utendaji wake.