Jifunze kuwa mkweli kwa daktari wako

Dk Chris Peterson 

Imepakiwa - Friday, January 11  2019 at  09:50

Kwa Muhtasari

Umuhimu wa tiba unaanza tangu maelezo ya awali ya mgonjwa

 

Tabia ya kutosema ukweli kwa daktari ipo kwa wengi. Huenda sababu ni aibu mathalani inapotokea mgonjwa ana tatizo nyeti la kiafya na muhudumu wake afya au daktari wake ni wa jinsia tofauti.

Lakini aibu nyingine husababishwa na tofauti ya umri na hasa inapotokea kuwa umri wa daktari ni sawa na umri wa mtoto wa mgonjwa.

Naomba tu ifahamike kuwa, katika sehemu ambazo unatakiwa kuwa huru na mkweli basi ni kwenye chumba cha daktari.

Kuwa mkweli kwa daktari wako kutakusaidia akupe huduma bora zaidi kutokana na kile unachokipitia wakati huo au siku chache kabla hujapata tatizo.

Unapaswa kujua ukweli kuwa, kuficha tatizo la kiafya kwa daktari ni hatari kwa kuwa umuhimu wa tiba unaanza tangu maelezo ya awali ya mgonjwa kabla hata ya kufanyiwa vipimo.

Yafuatayo ni mambo ambayo watu hupendelea zaidi kuwaficha madaktari, hivyo nakusihi uache.

Sikunywa pombe

Wagonjwa wengi hukumbwa na aibu sana kueleza kwa daktari kama wamekunywa pombe muda mfupi kabla ya kulazimika kwenda hospitali kwa ajili ya huduma ya matibabu ya dharura.

Wakati unafikiria kumdanganya mtoa huduma wako wa afya unapaswa kuufahamu ukweli kwamba unywaji wa pombe unaweza kutoa majibu tofauti na tatizo lako kiafya ikiwa unalazimika kufanyiwa vipimo vya aina mbalimbali mwili wakati pombe ikiwa mwilini.

Hivyo ni vyema kuwa muwazi kwa sababu itamsaidia daktari aanze na huduma ya kuondoa kiasi cha pombe kinachozunguka mwilini ili utakapofanyiwa vipimo, upate majibu sambamba na tatizo lako la kiafya.

Nimeacha kuvuta sigara

Unaweza kudhani kama ni jambo la kawaida ili kumficha mtoa huduma wako wa afya kumficha kama unavuta sigara, kuna umuhimu mkubwa sana yeye kujua ukweli huu. Baadhi ya tiba hasa ya vidonge inaharibiwa na utendaji kazi wake mwilini na ile sumu inayopatikana kwenye moshi wa tumbaku ambayo kitaalamu inajulikana kama Nicotine.

Mwandishi wa makala hii ni daktari kutoka Hospitali ya TMJ