http://www.swahilihub.com/image/view/-/2961142/medRes/1179697/-/11dejliz/-/snKamaru.jpg

 

John Joseph Kamaru: Shujaa wa ujasiri kimuziki

Joseph Kamaru

Mwanamuziki Joseph Kamaru wa kutoka jamii ya Agikuyu aimba studioni Aprili 15, 2009. Picha/LIZ MUTHONI 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, May 15  2018 at  15:16

Kwa Mukhtasari

Miaka 79 iliyopita katika Kaunti ya Murang’a alizaliwa mtoto wa kiume kwa jina Joseph Kamaru ambaye aliishia kuwa na ushawishi mkuu katika safu ya nyimbo za ushauri kwa mtindo wa Benga.

 

MIAKA 79 iliyopita katika Kaunti ya Murang’a alizaliwa mtoto wa kiume kwa jina Joseph Kamaru ambaye aliishia kuwa na ushawishi mkuu katika safu ya nyimbo za ushauri kwa mtindo wa Benga.

“Kero langu kuu hadi sasa ni kupambana na mawimbi ambapo katika kipindi cha miaka mitatu sasa, wasambazaji udaku wa kimitandao wameniua mara tatu,” Bw Kamaru ameambia Swahilihub katika mahojiano

Anasema kuwa wiki jana alipigiwa simu kutoka kwa wapenzi wa usanii wake wakimuuliza kama bado angali hai baada ya habari kuchipuka mitandaoni kuwa ameaga dunia.

Akiwa na rekodi ya kipekee ya kuwa mtunzi wa nyimbo 1,011 hadi sasa, anakumbuka tu kuwa mwaka wa 1966 alitoa kibao kwa jina “Ndari ya Mwalimu (kipenzi cha mwalimu” ambacho kilikashifu uhusiano wa kimapenzi kati ya walimu na wanafunzi na ambapo muungano wa walimu nchini (KNUT) baada ya kuusikiza, ukaitisha mgomo wa kitaifa.

“Ni Rais Hayati Mzee Jomo Kenyatta ambaye alikuwa mwandani wangu aliyenitetea kwa walimu hao na kisha akawaomba warejee kazini. Lakini walimu hao walipiga marufuku uteja wao kwa kanda zangu, Hata wabunge walinijadili bungeni wakinikemea,” asema.

Huku uzee ukionekana kumzonga, Kamaru anasema kuwa raha yake kuu ya kimaisha imekuwa katika safu ya utunzi na uimbaji wa muziki, sekta ambayo anasema ndiyo kiini cha chote alicho nacho hadi sasa.

Mwandani wa Rais Uhuru Kenyatta ambaye humuona mara kwa mara kushauriana kuhusu hili au lile, Kamaru anasema kuwa taifa liko katika mkondo sawa kimaendeleo na pia mikononi sawa ya UhuRuto.

Muziki wake wa miaka ya 1960 umekuwa na ufuasi hadi leo hii, huku wasanii wengi wakimsifu kwa kuwapa mkono wa mwongozo walipokuwa wanasaka njia ya kujipenyeza katika safu hii ya utumbuizaji.

Usanii wake ulianza mwaka wa 1965 ambapo alitunga wimbo huo wa Ndari ya Mwalimu na ambao kufuatia sokomoko hilo na walimu, akapata umaarufu uliosambaa kwa kasi katika jamii ya Agikuyu.

Akabakia katika umaarufu huo hadi pale muziki wa kufokafoka ulipoingia nchini miaka ya 1990, lakini hadi sasa akibakia na ule umaarufu wa kuwa kama makavazi ya muziki nchini na pia kutoa ushauri kwa watafiti kuhusu mila na desturi za jamii yake.

Ingawa mwaka wa 2009 alitangaza kuokoka na akazindua kanisa lake katika mtaa wa Tea Room Jijini Nairobi, amebakia kuwa na ule msimamo wa utamaduni na uabudu wa Mungu kwa njia za kitamaduni, hali ambayo imemnyima wafuasi wengi katika Injili yake.

Anasema kuwa hilo halimpotezei hata lepe la usingizi kwa kuwa “mimi kama Kamaru sibadiliki, kimawazo na imani na niwe na wachache au wengi, bado itikadi zangu ni zilezile”.

Alizaliwa katika Kaunti ndogo ya Kangema na ambapo amejiimarisha kimuziki hadi historia kumpa nembo ya 'mtabiri wa kijamii' kwa kuwa zile mada alizokuwa akiweka katika muziki wake wa miaka ya 1960 na 70 zimekuja kushuhudiwa kwa uhakika miaka ya 1980 hadi leo hii na kusonga mbele.

Biashara

Aliachana na elimu mwaka wa 1957 na akaingia Jijini Nairobi akiwa mchuuzi wa bidhaa za kila aina, zikiwemo dawa za kuua wadudu, mboga na chochote kingine alifikiria kingempa hela kama biashara.

Maisha yalipozidi kuwa magumu kwake, aliajiriwa kama ‘yaya’ katika familia moja ya kizungu ambapo majukumu yake yalikuwa kulea watoto na kutekeleza majukumu ya usafi pamoja na kutumwatumwa mtaani kutekeleza hili na lile.

Marais Kenyatta, Daniel Moi na Uhuru Kenyatta kwa sasa ni miongoni mwa wale muziki wake ulimsaidia kuingia katika kambi zao na akanufaika hapa na pale, akipoteza pia hapa na pale.

Kati ya 1975na 1985 anasema ndio wakati wake wa kuafikia kilele cha talanta yake ambapo alianza hata kupewa kandarasi za kutumbuiza ndani ya mikahawa na mabaa, huku kwa jina lake na ushawishi wake akipokezwa ada za juu.

Kuna wakati nyimbo zake ziliumiza wandani wa rais Moi na kwa muda akapigwa marufuku ya kurekodi kwa msingi kuwa alikuwa na uchochezi.

Kamaru hakujali marufuku hayo na kichinichini akawa bado anaachilia kanda baada ya nyingine.

"Nilikuwa na ngoma nyingi; hivyo nikiulizwa nilikuwa najitetea kuwa wimbo huo mpya sio mpya kwa kuwa ulikuwepo katika soko kabla ya nipigwe marufuku,” asema.

Kuna wakati Mzee Kenyatta alimualika katika boma lake huko Gatundu ambapo alitaka kutumbuizwa na Kamaru.

“Aliagiza kuwa kusichezwe ala zozote za Muziki, kuwa alihitaji tu kusikia sauti yangu na ikawa  hivyo. Nilifanikiwa kusukuma mzee apige marufuku upenyo wa Kihindi katika soko letu la kimuziki na hilo liliamrishwa mara moja mwaka huo wa 1972,” asema.

Urafiki huo wa Kenyatta na Kamaru ulidumu hadi ikawa alipewa kazi ya kutumbuiza katika haruzi za Ngengi Muigai na pia ya Rais wa sasa, Uhuru Kenyatta.

Mwaka wa 1975 ambapo mwanasiasa wa Nyandarua, Josiah Kariuki aliuawa kikatili, Kamaru akaachilia kanda ya kukashifu mauaji hayo na ambapo alielekeza kidole cha lawama kwa “wakubwa serikalini.”

Huku itikadi yake kuu ikiwa ni “sema ukweli Shetani aaibike”, Kamaru hakujali kuwa Kenyatta alikuwa mwandani wake na alisema kinaga ubaga kuwa “wauaji wa Kariuki wasitafuwte mbali kwa kuwa walikuwa ndani ya ufalme wa nchi.”

Uhusiano wao ukatamatika lakini hata baada ya kupokezwa jumbe nyingi za kutisha uhai wake, akaponyoka akiwa tu hai lakini bila ule usaidizi wa urafiki wa urais.

Wakati Kenyatta aliaga dunia 1978, alirithi ule urafiki na uongozi wa taifa na Kamaru akawa wa kuonekana ikulu kwa urahisi.

Mwaka wa 1980 Moi aliandamana na Kamaru hadi nchini Japan na aliporejea nchini, akatunga wimbo kwa jina “Safari ya Japan” na ampao alimiminia rais Moi sifa kemkem.

Upendo wa Moi kwake ukazidi na akanufaika si haba.

Miaka ya 1980 ambapo mito ya kudai demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa ilishika kasi, Kamaru aligeuka kuwa mwiba kwa Moi baada ya kujiunga na wale waliokuwa wakimsukuma rais akubali yaishe.

Mwaka wa 1988 akatia ngoma kwa jina “Mahoya ma Bururi (Maombi kwa taifa)" na akasema waziwazi kuwa mawimbi hayo ya kidemokrasia yalikuwa yakumbatiwe na kila yeyote aliyekuwa na utu na pia uongozi ambao ni mwito kutoka kwa Mungu.

Aliitwa Ikulu na akajitetea kuwa wimbo huo ulikuwa maombi kwa taifa.

“Moi alinipa Sh800,000 za kutafsiri wimbo huo kwa lugha ya Kiswahili na akaniagiza nirejee Ikulu siku iliyofuata ili ausikize na alinganishe na ripoti ambazo alikuwa amepokezwa kuwa wimbo huo ulikuwa wa uchochezi dhidi ya utawala wa Moi,” asema.

Aliporejea Ikulu siku hiyo, alikumbana na uhasama wa wazi ambapo alitimuliwa kutoka Ikulu, akipewa onyo kuwa “Moi sio wa kuichezewa”.

Raha yake ikulu ikafika kikomo lakini kukawa na hujuma ambapo mwaka wa 1992, waliokuwa wanaunga mkono harakati za kukumbatiwa kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa walimuorodhesha Kamaru kama msanii katika hafla ya sherehe za Madaraka Dei.

Kamaru hakuwasaliti wakereketwa hao waliokuwa wamemsajili kwa kuwa kabla ya kuzindua utumbuizaji wake, alimwelekeza Moi hotuba ya papa kwa hapa uwanjani na akamwambia: “Acha kukaa kitako ukiwa na hiyo fimbo yako ukijituliza na maneno ya uongo kutoka kwa wandani wako ambao wanakudanganya kuwa wewe uko maarufu nchini. Ukweli ni kwamba wengi hawakupendi.”

Kamaru anakumbuka kuwa nusura aanguke chini azirai kwa uoga baada ya uwanja wote kukimya, akaamua kutoroka lakini akakumbuka kuwa hiyo ingekuwa kazi bure.

“Ni ile hali ya kuachilia risasi lakini ikilenga ndipo, unajuta ni kwanini ukaitoa. Lakini nikaamua kuwa hata mauti yangenipata, ujumbe ulikuwa umefika na hakuna vile angebadilisha maneno yangu na ambayo yalikuwa ya ukweli halisi kuhusu hali ya kisiasa wakati huo. Lakini sikuuawa,” asema.

Anasema kuwa kwa sasa bado ako chonjo na anashughulika sana na masuala ya kuwaleta watu wa Gikuyu Embu na Ameru (Gema) pamoja kujivunia kuwa wa asili ya lugha zao za mama na umoja wa kijamii kama ndugu na dada.