http://www.swahilihub.com/image/view/-/3463068/medRes/1301333/-/wimb89z/-/dnnakurumututho0401%252819%2529.jpg

 

John Mututho: Yuazijua sana sheria za kupinga ulevi wa kiholela

John Mututho

Aliyekuwa mwenyekiti wa Bodi ya Kukabiliana na Pombe na Dawa za Kulevya (Nacada) John Mututho akagua pombe katika maduka eneo la Salgaa, Rongai Januari 4, 2016. Picha/SULEIMAN MBATIAH 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, March 13  2018 at  11:24

Kwa Muhtasari

John Mututho ndiye anahusishwa na sheria za kupinga ulevi wa kiholela maarufu kama 'Sheria za Mututho'.

 

JOHN Mututho ndiye anahusishwa na sheria za kupinga ulevi wa kiholela maarufu kama 'Sheria za Mututho'.

Sasa ameteuliwa na gavana wa Kiambu kuwa mshauri wake wa kuja na mikakati ya kukabiliana na ulevi wa kiholela.

Mututho alizaliwa mwaka wa 1957 na kupewa jina John Michael Njenga Mututho.

Ni hasidi mkuu wa ulevi wa kiholela na utumiaji wa mihadarati.

Amekuwa akipambana na uraibu huo hapa nchini Kenya kiasi cha kuteuliwa na utawala wa Jubilee kuwa mwenyekiti wa mamlaka ya kupambana na ulevi na mihadarati (Nacada).

Tukielekea uchaguzi mkuu wa 2017 aliondolewa katika nafasi hiyo.

Alipewa wadhifa mwingine ambapo aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya kutatua mizozo katika sekta ya uchukuzi, wadhifa ambao hakunukuliwa popote akiandaa kikao au akiwajibikia.

Alikuwa pia analenga kuwania ugavana wa Nakuru na aliishia kushindwa katika mchujo wa Jubilee na hatimaye licha ya kuruka hadi kwa uwaniaji huru, akarambishwa sakafu na Lee Kinyanjui ambaye kwa sasa ndiye gavana wa Kaunti hiyo.

Alikuwa amehudumu kama mbunge wa chama cha Kanu katika eneo bunge la Naivsha kati ya 2007 na 2013 ambapo alitimuliwa mamlakani kwa kura katika uchaguzi mkuu wa 2013 baada ya walevi na watengenezaji pombe hasa wa Naivasha kujiunga katika mrengo wa kumtimua kufuatia sheria yake ambayo waliiona kuwa hasi.

Ushindi wake mkuu ulikuwa katika mwaka wa 2016 ambapo alimshawishi Rais Uhuru Kenyatta kuzindua kampeni ya kumwaga pombe za sumu na kuweka mikakati ya ukadiriaji ubora wa vileo sokoni.

Huku akishabikia hilo, nao wapiga kura wakawa wamemvizia na ambapo walimwonyesha mlango wan je ya siasa.

Ana shahada kuhusu usimamizi wa maeneo kame kutoka Chuo Kikuu cha Egerton na pia kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Pia, ni mwanauchumi aliyefuzu katika chuo cha Latrobe kilichoko nchini Australia.

Ashawahi kufanya kazi kama afisa wa umma kwa miaka 11 akiwajibikia uthabiti wa lishe, uvunaji maji ya mvua na pia kushirikisha taasisi na mashirika ya ufadhili katika usimamizi wa maeneo kame nchini.

Mwaka wa 2005, Mututho alishtakiwa kwa madai ya ufisadi ambapo alisemwa kutapeli hospitali kuu ya Kenyatta Sh 41.5 mllioni kupitia kughushi stakabadhi za kudai malipo.

Miaka tisa baadaye, kesi hiyo ikatupwa nje na mahakama, huku akiwa tayari amehudumu kama mbunge wa Naivasha na hadi leo, anashikilia kuwa alilengwa kisiasa.
Februari 2014, Mututho alijipata taabani tena wakati nusura mali yake ipigwe mnada baada ya kulemewa kulipa gharama ya mahakama kufuatia kesi yake ya kupinga ushindi wa mbunge aliyerithi Naivasha.

Lengo kuu

Mututho anasema kuwa alitoka kazini pale Nacada kabla ya kutimiza lengo lake kuu la kutaka sheria ipendekeze adhabu ya kifo kwa yeyote ambaye atapatikana na hatia ya kuuza pombe za sumu.

Ana mke na mtoto mmoja kwa jina, Daniel Njenga ambaye hivi majuzi naye alikuwa mahakamani kujibu mashtaka ya utapeli.

Kwa sasa, Mututho anashughulika na biashara ya kurekebisha walevi waliozama kabisa ndani ya mtindi katika Kaunti ya Nakuru ambapo amewekeza biashara hiyo yake; anatoa matangazo kuwa hugharimu tu Sh60,000 na pia ada zaidi kutoka kwa kadi ya hazina ya afya nchini (NHIF).