http://www.swahilihub.com/image/view/-/4088542/medRes/1748227/-/nx1kohz/-/kamau.jpg

 

Josh wa Lampshade asema kazi ya taa ina natija kubwa

Joshua Kivungi Kimeu

Joshua Kivungi Kimeu, muundaji wa Lampshade akionyesha zinavyoundwa. Kifaa hiki hupunguza mwangaza wa stima kando na kutoa mwangaza wenye rangi maridadi. Mfanyabiashara huyu ashikilia kazi hii humpa donge nono; hata akiajiriwa kazi atakayolipwa zaidi ya Sh40,000 kwa mwezi hataikubali. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Saturday, September 9  2017 at  13:30

Kwa Mukhtasari

Hata nikilipwa zaidi ya Sh40,000 kwa mwezi sitaacha uundaji wa vifaa vya ama kupunguza mwangaza au kutoa mwangaza wenye rangi za kuvutia, anasema Josh.

 

KUVUNJIKA kwa mwiko sio mwisho wa mapishi, hivi ndivyo walisema wavyele wetu.

Licha ya masaibu chungu nzima aliyokumbana nayo Josh wa Lampshade, nyota yake haikuzimwa hasa ikizingatiwa ana kipaji katika sanaa.

Kifo cha mzazi wake wa kiume akiwa katika shule ya upili na aliyekuwa akimlipia karo mnamo mwaka wa 2002 kilisababisha agure masomo ili asake riziki yake binafsi.

Ari yake ya kufikia kidato cha nne haikudidimia, mwaka wa 2004 alijisajili kama mwanafunzi wa kujitegemea na kufanya mtihani wa kitaifa mwaka wa 2006 akazoa alama C+.

Hata hivyo hakuweza kujiunga na chuo kikuu kwa sababu ya ukosefu wa pesa ambazo husemekana 'ndio sabuni ya roho'. Mungu hamuachi mja wake, eneo bunge la Ruiru Kaunti ya Kiambu ukitaja jina 'Josh wa Lumpshade' utaelekezwa kwa Bw Joshua Kivungi Kimeu, ambaye anafanya kazi anayosema kuwa ni ya sanaa ya kuunda vifaa vya kupunguza mwangaza wa stima na vile vile kubadilisha miale iwe maridadi.

Takriban mita 500 hivi kutoka katika kituo cha polisi cha Kimbo, Progressive Ruiru nyumba anayoishi Bw Kivungi, mkewe na watoto watatu ndiko karakana yake ya kutengeneza vifaa hivyo iliko.

Anavitambua kama 'Lampshade' ama 'Lamp balls' kwa Kiingereza. Bw Kivungi 31, akihadithia kati ya mwaka wa 2007 hadi 2015 amefanya kazi katika kampuni kadhaa ikiwamo ya Manji Biscuits na Benki ya Equity kwenye sekta ya soko.

"Nimewahi pandishwa madaraka hadi nikafikia ngazi ya maneja wa uhusiano mwema," asema.

Lakini utamu wa kujiajiri kijana huyu ndiye anaufahamu kwa kina baada ya kuonja maisha ya gange ya kuajiriwa na yale ya kuwa bosi wake mwenyewe. "Hakuna kazi inayopiku ya kujiajiri, mimi ndiye bosi wangu mwenyewe na hufanyia kazi katika maskani yangu," afichua Kivungi.

Kukumbuka

Anakumbuka vyema mwanzoni mwa mwaka wa 2016 kaka yake mkubwa ndiye alimshawishi kiasi cha kumfungulia milango ya heri katika sekta ya sanaa.

"Kaka ndiye akifanya utafiti wake kwenye mtandao wa intaneti alipatana na vifaa vya Lumpshade akaneleza 'Josh kuna kitu kizuri nimeona na chaonekana kuwa rahisi kuunda'. Mja hakatai wito ila hukataa aitiwalo, nilienda kwake nikapata ameunda kimoja, nikakikagua kwa makini na hata bila ya kunifunza alivyofanya nikatengeneza changu," asimulia msanii huyu akiongeza kuwa hivyo ndivyo alianza uundaji wa Lumpshade.

Ilimgharimu mtaji wa Sh1,500 pekee kuanzisha uundaji wa vifaa hivyo.

"Nilinunua nyuzi za sweta na fulana, guluu ya mbao na muundo wa mpira. Siku ya kwanza nilitengeneza vifaa vinne na kufikia jioni nikawa nimeuza kimoja kwa Sh450," aeleza Kivungi.

Huo ukawa mwanza wa kusema 'buriani kazi ya kuajiriwa'.

"Niliona ni jambo ninaloweza kufanya kupitia mapenzi yangu ya sanaa tangu nilipokuwa mdogo. Bila mapenzi hata mtu akiajiriwa kazi hataifanya kwa dhati na mwishowe ataiacha tu. Lampshade zikaongoa mapenzi yangu ya sanaa na nikaichukulia kama kazi iliyoniajiri hadi kwa sasa," asema.

Aongeza: "Ninapenda kwa dhati kazi ninayofanya. Nimekuwa nikieleza watu hata leo nikiitiwa kazi inayonilipa Sh30,000 kwa mwezi sitaacha kazi yangu. Katu kwa dawa nikipata kazi ninayoahidiwa kulipwa Sh40,000 kwa mwezi, uundaji wa Lumpshade sitauacha, ujira ninaopokea ni mkubwa. Vifaa hivi vimenipa jina."

Kulingana na Kivungi ni kwamba kifaa kimoja hukiunda kwa muda wa saa moja na huwa na rangi tofauti kwa mujibu wa nyuzi.

Kwa siku huunda zaidi ya Lumpshade 10 ambapo moja hugharimu kati ya Sh400-900, japo bei yake hutegemea ukubwa wa kila kifaa.

"Kila siku hupata oda zaidi ya vifaa 10, hata hushindwa kukimu mahitaji ya wateja kwa sababu ni wengi sana," akafichua.

Kando na oda, kuzichuuza, mfanyabiashara huyu hutumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook kufikia wateja wake ambapo anafahamika kwa jina la kampuni yake 'Brighter Ceilings Lanterns' na kwa mtandao wa WhatsApp vilevile.

"Wateja ndio hunitafuta kwa ajili ya kazi bora ninayofanya, wajua chema chajiuza kibaya chajitembeza," asema na kusisitiza kuwa Lumpshade zake ni za kipekee kwa kuwa ni za mviringo ama umbo la duara.

"Kazi ziko kwa wingi hususan zile za juakali. Vijana wawache kuegemea ajira za ofisi ambazo ni finyu mno. Tuwe wabunifu wa kazi ili tuajiri wengine," ashauri.

Vifaa hivyo huvianika kwenye miali ya jua ili nyuzi hizo zinate na kushikanishwa vyema na guluu, kwa karibu masaa mawili hivi.

"Majira ya baridi na msimu wa baridi huathiri utendakazi wangu," aeleza changamoto zinazositisha kazi yake.

Bw Kivungi asema hivi karibuni analenga kufungua duka kubwa la kuuza bidhaa anazounda.