Ijue kaunti ya Kajiado

Joseph ole Lenku

Gavana wa Kaunti ya Kajiado, Joseph Ole Lenku. Picha/MAKTABA 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Saturday, April 14  2018 at  14:26

Kwa Mukhtasari

Kajiado ni mojawapo ya kaunti katika eneo la Bonde la Ufa nchini Kenya.

 

KAJIADO imepakana na kaunti ya Nairobi na upande mwingine nchi jirani ya Tanzania.

Jamii ya Maasai ndiyo ina idadi kubwa ya wakazi katika kaunti hiyo. Aidha wakati wa hofu za kabla na baada ya uchaguzi nchini Kenya, kaunti hii hutajwa kuwa ni mojawapo ya maeneo ya mijini, yaani Metropolitan; kumaanisha hapa kuna makabila mengi yanayotangamana na kutafuta riziki kwa pamoja.

Awali ufugaji ndio ulikuwa umeshamiri Kajiado, mashamba mengi na makubwa yakifanywa kuwa maeneo ya lishe ya mifugo. Ufugaji wao ulikuwa ule wa kuhamahahama, wengi wakionekana kuanza kuingia Nairobi kwa ajili ya kutafutia mifugo chakula na maji.

Hata hivyo, taswira hiyo sasa imeanza kubadilika na kuwa ya kijani kibichi cha kilimomseto.

Wakazi wa Kajiado wamekengeuka na kuwa miongoni mwa wanaolenga kuafikia mojawapo ya ajenda kuu ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuangazia usalama wa chakula nchini.

Unapozuru kaunti hiyo kwa sasa, kinachokukaribisha kwa umbali ni mimea aina mbalimbali.

Bi Judith Nduva ni mkazi wa mtaani Korompoi, na anasema shamba lake lenye ukubwa wa ekari tano ameligeuza kutumika kwa kilimo cha mboga za kienyeji kama kunde, managu, mchicha, saga, ikiwa ni pamoja na nyanya na mboga aina ya spinachi.

"Kitambo nilikuwa mfugaji, lakini haukuwa na mapato vile," aeleza. Katika shamba lake, amechimba bwawa lenye urefu wa futi 150 na kuweka matenki ya kuhifadhi maji, hasa ya kunyunyizia mimea maji. Anaeleza kwamba tangu azamie kilimo, ameweza kupiga hatua kubwa maishani. "Kilimo kina natija chungu nzima, ndio sababu unaona wakazi wa Kajiado wanaacha ufugaji ili kukiingilia," akaambia Swahilihub.

Mkulima huyo aidha amekumbatia kilimo kwa mfumo wa kisasa wa kutumia mifereji (Drip Irrigation), kunyunyizia mimea yake maji.

Kununua

Bw Peter Mugo, ingawa alihamia Kajiado ni mkulima wa boga karibu na ilipo reli ya kisasa almaarufu SGR. Shamba analokuza zao hilo alianza kwa kukodi, na kwa sasa amefanikiwa kulinunua.

"Kilimo Kajiado ni dhahabu, mchanga wake una rutuba tele," asema.

Ukulima kwenye mahema 'Greenhouse' pia umesheheni. Hasa wakulima wa mahema hukuza nyanya, na pilipili mboga.

Ni kufuatia mfumko wa kilimo katika kaunti hiyo ambapo ambapo sekta ya biashara imeweza kustawi. Mazao yanayotolewa shambani ndiyo yayo hayo yanauzwa katika mji kama vile Kitengela.

Kajiado ina ukubwa wa kilomita 21,292.7 mraba, na kukadiriwa kuwa na zaidi ya watu 687,312 kwa mujibu wa sensa ya 2009.

Aidha, imeundwa kwa maeneobunge matano; Kajiado ya Kati, Kajiado Kaskazini, Kajiado Kusini, Kajiado Mashariki, na Kajiado Magharibi.

Kaunti hiyo yenye makao yake makuu mjini Kajiado, inaongozwa na aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani Joseph Ole Lenku, kama gavana. Viongozi wengine ni, seneta Peter Ole Mositet na Mwakilishi wa Wanawake Bi Janet Teiyaa.