MWAMKO MPYA: Kamusi Kuu ya Kiswahili yenye maneno ya kidijitali yazinduliwa

Kamusi Kuu ya Kiswahili

Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang’i pamoja na Balozi wa Lugha ya Kiswahili barani Afrika Mama Salama Kikwete huku wadau wa lugha hiyo wakishangilia wakati wa uzinduzi rasmi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK) katika Taasisi ya Ukuzaji mtaala nchini KICD, jijini Nairobi Julai 25, 2017. PICHA/ GEORGE AJOWI 

Na GEORGE AJOWI

Imepakiwa - Wednesday, July 26   2017 at  18:40

Kwa Mukhtasari

WIZARA ya Elimu inapania kupeleka mswada katika Bunge la Afrika Mashariki kwa lengo la kuhakikisha mwanachama anakitumia na kukienzi Kiswahili. Haya ni kulingana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Fred Matiang’i.

 

Dkt Matiang’i aliyasema haya katika uzinduzi rasmi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK) katika Taasisi ya Ukuzaji mtaala nchini KICD, jijini Nairobi hapo Jumanne.

“Nitazungumza na warizi mwenzangu Phillys Kandie ambaye anasimama maswala ya Afrika Mashariki kwamba tutakapokutana katika mkutano ujao tupendekeze mswada bungeni. Hii ndio njia pekee ambayo tunaweza kukuza umoja wetu kanda ya Afrika Mashariki,” Dkt Matiang’i alisema.

Aidha, waziri huyo alidokeza kuwa wizara yake iko tayari kushirikiana na wizara ya elimu ya Tanzania ili kuhimiza shughuli na matumizi ya Kiswahili katika shughuli zote za serikali.

Mama Salma Kikwete ambaye alikuwa mgeni wa heshima na ambaye pia ni balozi wa lugha ya Kiswahili alisisitiza umuhimu ya bidhaa hii adhimu; ambayo ni Kiswahili. Aliwataka wote waliohudhuria kujitolea na kuipigania lugha ya Kiswahili.

“Utungaji wa kamusi kubwa ya KKK ni mfano mzuri wa kuigwa na kukabiliana na changamoto ya kukiteteta Kiswahili. Ni fursa ambayo tukiitumia vizuri itatunehemesha na pia kutoa ajira kwa vijana wetu katika bara la Afrika,” alisema Mama Salma Kikwete.

Kamusi Kuu ya Kiswahili ina upekee wake ikilinganishwa na kamusi zingine kwani ina zaidi ya maneno 45,500 huku zaidi ya maneno 2,000 yakiwa mapya. Hakuna kamusi nyingine ambayo imewahi kuchapishwa na maneno kiasi hiki.

Kamusi hii inajumuisha maeneo ibuka katika maswala ya kilimo, teknolojia na teknohama na kukiwezesha Kiswahili kujisimamia bila kutegemea utohozi.

Maneno ya kidijitali

Kwa mafano: Zanamango=Computer visuals, Kinyonyi=flashdisk, Zanatepe=computer command, kiwambo=icon na kadhalika. Pia inaelezea jinsi ya kutamka maneno flani na vile vile etimolojia ya maneno mbalimbali.

Kamusi hii iliandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa BAKITA na kuchapishwa na Longhorn Publishers. Mama Salma Kikwete aliyahimiza mashirika haya mawili kuzidi kueneza  ubia wao.

“Itakuwa bora kama Longhorn na Baraza la Kiswahili la Taifa BAKITA zitaanzisha miradi ya pamoja na kutunga vitabu vya kujifunzia Kiswahili kama lugha ya kigeni. Tungeni pia kamusi za Istilahi kwa ajili ya masomo ya nyanja mbalimbali,” akasema Mama Salma.

Mwakilishi wa BAKITA, Dkt. Selemani S. Sewangi akidokeza kuwa kamusi hii imekubalika rasmi Kenya na Tanzania ndio maana ikachapishwa na bendera ya mataifa yote mawili.

Bendera si umiliki

“Tutakapoenda Uganda, kamusi hii itakapozinduliwa katika bunge la Afrika Mashariki na waseme hii Kamusi ni yetu tutaweka bendera yao pale, Rwanda wakikubali tutaweka bendera yao pale na Sudan Kusini, DRC na Burundi pia.

Hizi bendera si kusema ati mataifa haya ni wamiliki wa kamusi hii bali ni alama za kibiashara za kukubalika rasmi,” alisema Dkt. Swewangi.

Mkurugenzi mkuu wa Longhorn Simon Ngigi alisema kuwa KKK itakuwa kurunzi kwa wanafuzi na wadau wote wa elimu kwani ubora wake ni wa hali ya juu.

“Kamusi hii ina ubora wa juu na ni kitu cha kujivunia kwani bali na kuandikwa na BAKIKA, kamusi hii imeidhinishwa na KICD nchini Kenya na pia Taasisi ya Elimu nchini Tanzania kwa hivyo ni bidhaa iliyo halali kimataifa,” alisema Ngigi.

Kamusi Kuu ya Kiswahili ilizinduliwa rasmi nchini Tanzania mnamo Juni 16, 2017 katika ukumbi wa Bunge la Tanzania jijini Dodoma.

Kamusi hii itakudhi mahitaji ya wanafuzi wa shule za msingi, walimu, wahadhiri, na wale wa ngazi za juu katika nyanja za elimu. Vile vile itawafaa sana wakalimani, watafsiri, watalii, watafiti na wadau wote wa Kiswahili kwa jumla.