Vybz Kartel asema Gaza wa Kayole waache 'kumuabudu'

Vybz Kartel

Msanii wa Riddim, Vybz Kartel. Picha/HISANI 

Imepakiwa - Thursday, June 15  2017 at  14:56

Kwa Mukhtasari

Staa wa dancehall na riddim Vybz Kartel anayesotea jela kwa sasa kwa kosa la mauaji, ameliomba genge hatari la majambazi jijini Nairobi, Gaza, kuacha kumwabudu kama Mungu.

 

STAA wa dancehall na riddim Vybz Kartel anayesotea jela kwa sasa kwa kosa la mauaji, ameliomba genge hatari la majambazi jijini Nairobi, Gaza, kuacha kumwabudu kama Mungu.

Kartel alitupwa jela Aprili 2014 kwa kifungo cha maisha baada ya kupatikana na kosa la kumuua produsa wake wa zamani ila anaweza kuachiliwa huru baada ya kuhudumia kifungo cha miaka 35. 

Licha yake kuendelea kuozea nyuma ya nondo, Kartel ameeendelea kuachia hiti moja baada ya nyingine akiwa gerezani.

Wakati wa uhuru wake, alikuwa ameanzisha vuguvugu lake la Gaza, kundi ambalo limekuwa likimsukumia muziki wake.

Kutokana na umaarufu wake pamoja na muziki wa riddim na dancehall nchini, kundi hatari la majambazi wachanga kutoka mtaa wa Kayole, Nairobi lilikopa jina hilo na limekuwa likiwahangaisha sana wakaazi wa Nairobi.

Idadi kubwa ya wanachama wa Gaza wameua na polisi.

Genge hilo la Gaza linamuhusudu sana Vybz nyimbo zake pamoja na mtindo wake wa maisha ikiwemo uvutaji bangi.

Gaza limekuwa maarufu na limekiri wazi wazi kwamba linamhusudu na kumuabudu Vybz.

Souflo TV

Taarifa hizo hatimaye zilimfikia Vybz akiwa jela kupitia shoo maarufu ya televisheni ya dancehall nchini Jamaica  Souflo TV, ambayo vilevile aliitumia kuwapasha majambazi wa Gaza.

Kupitia video iliyorekodiwa na mtangazaji wa kipindi hicho aliyefikiwa na shabiki mmoja kutoka Kenya kupitia Youtube, Vybz anasikika akiwarai majambazi wa Gaza wabadilike na wakome kumuabudu.

Kwenye audio aliyomrekodi Vybz mwenyewe anasikika akiwarai kwa kusema, “… Nimesikia kuna genge la majambazi kutoka maeneo ya Kayole Nairobi. Limejiweka chini ya mwavuli wa Gaza, na ndivyo wanavyojiita. Nasikia wananiabudu mimi Vybz Kartel huku pia wakiwaua watu. Nawaomba, kupitia audio hii niliyowatengenezea na pia nitawaandikia barua kuwaomba waache maovu hayo wanayofanya. Wanahangaisha usalama wa taifa. Hayo maisha wanayoendesha ni maovu hawawajali watu wenzao katika jamii…”