http://www.swahilihub.com/image/view/-/4801450/medRes/2137680/-/fj2bsg/-/kasanda.jpg

 

Kasanda: Wanawake msiwakubali wanaume wasiotahiriwa

Mkuu wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, Rachael Kasanda  

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Thursday, October 11  2018 at  15:31

Kwa Muhtasari

Wanaoshiriki tendo la ndoa na wasiofanyiwa tohara wapo hatarini zaidi kuambukizwa VVU

 

Sumbawanga. Mkuu wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, Rachael Kasanda amewataka wanawake wa mkoani Rukwa kutokubali kushiriki tendo la ndoa na mwanamume ambaye hajatahiriwa ili kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Kasanda alitoa kauli hiyo jana katika uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha wananchi hususan wanaume kupima VVU na kuanza kutumia dawa mapema.

Mkuu huyo wa wilaya aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Amos Makala alisema kwamba wanawake wanaoshiriki tendo la ndoa na wanaume wasiofanyiwa tohara wapo hatarini zaidi kuambukizwa VVU.

“Hata kama mwanamume huyo akitaka kutoa pesa nyingi kiasi gani msikubali mpaka umchunguze, na kama ana mkono wa sweta achane naye hadi atakapofanyiwa tohara ndipo mfanye tendo hilo la ndoa,” alisema.

Pia, aliwataka wanaume wenye umri mkubwa kutoona aibu kwenda kufanyiwa tohara kwani hata wakifanyiwa hakuna atakayewabaini kuwa wamefanyiwa kitendo hicho ukubwani.

Alitoa wito kwa wanaume kujitokeza kwa wingi kupima VVU kwenye uzinduzi huo kwa kuwa wataalamu mbalimbali wa afya wamejipanga pia kufanya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, huduma ya uchangishaji damu salama, kisukari na shinikizo la damu.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Katavi, Wilybrod Malandu alisema wanaume wengi hawapimi VVU na wamekuwa wakiishi kwa kutegemea majibu ya wake zao wanapokwenda kupima wakiwa wajawazito.