Kero ya mwendokasi imeshindikana kutatuliwa?

Imepakiwa - Wednesday, April 10  2019 at  11:25

 

Mradi wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam (Dart) ambao tangu uanze takriban miaka minne iliyopita umekumbana na migogoro, sasa unashindwa kukidhi matakwa halisi ya kuanzishwa kwake ambayo yalikuwa ni kuondoa msongamano wa watu vituoni.

Lengo jingine, kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa wakati mradi huo unazinduliwa, lilikuwa ni kusafirisha abiria wengi na kwa haraka ili kuwafikisha katika maeneo ya shughuli au miadi yao na ililengwa kwamba hata vituoni yasingekuwa yanatumia muda mrefu kupakia au kushusha abiria.

Jingine lilikuwa ni kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa na mfumo wa usafiri usiokuwa na malalamiko kwa wananchi, ikizingatiwa kuwa daladala zimekuwa na kero za aina mbalimbali kuanzia upakiaji, ushushaji, wingi wa vituo hadi kutojali muda wa wasafiri.

Pamoja na malengo hayo, kulikuwa na lengo jingine lililotajwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) wa wakati huo, Hawa Ghasia kuwa ni kupunguza msongamano wa magari yaliyokuwa yakiingia katikati ya jiji, badala yake wamiliki wa magari hayo watumie zaidi usafiri wa umma ili kuingia na kutoka mjini.

Tulipongeza mikakati na malengo yaliyoelezwa na Serikali kuhusu mradi huo ambao alikabidhiwa Udart kama mbia wa kuuendesha kwa kuwa mambo yote yaliyotajwa kabla na baada ya kukamilika kwa mradi yalilenga kumpunguzia mzigo mwananchi na kuboresha usafirishaji.

Hata hivyo, wakati Serikali ikiwa na mkakati wa kuanza awamu ya pili ya mradi huo kutoka katikati ya jiji kwenda Mbagala na maeneo mengine ya Dar es Salaam, dosari nyingi zimeonekana ndani ya muda mfupi, hivyo kuufanya mradi huo kuwa mzigo badala ya neema.

Tumeshuhudia dosari nyingi za kiuendeshaji kuanzia ukatishaji tiketi hadi usafirishaji. Ukatishaji tiketi kielektroniki ulisimama siku nyingi, hilo linaeleweka na hata Serikali imekiri kuwa inapoteza mapato makubwa kutokana na utaratibu wa ukataji tiketi wa sasa, lakini hili la uendeshaji ndilo tatizo kubwa zaidi.

Mradi huu hauna mabasi ya kutosha kwa muda sasa na watu wamekuwa wakisota vituoni muda mrefu kusubiri machache yaliyopo ili waende katika maeneo waliyopanga. Hali hii imekuwa ikiathiri shughuli za kiuchumi na kijamii.

Si hilo tu, hata mabasi hayo yanapokuwa vituoni kwa uchache wake, msongamano wa wasafiri ni mkubwa ndani na hivyo kunakuwa na kuibiana na kuwepo kwa tishio la kuambukizana magonjwa, hususan yatokanayo na kugusana au upumuaji ndani ya mabasi. Hili awali hatukulitegemea maana ilielezwa watu wangesafiri kwa raha bila kusongamana.

Hata hivyo, tunajiuliza hivi licha ya watendaji mbalimbali wa Serikali kuanzia wakuu wa wilaya, mkoa na hata mawaziri kujionea adha wanazopata wananchi kutokana na upungufu wa mabasi wameshindwa kutatua tatizo hilo? Au ndiyo wanasubiri Waziri Mkuu, Makamu wa Rais au Rais watatue kilio hicho?

Hivi kuna ugumu gani kama mabasi 70 ambayo yamekwama bandarini kutokana na tofauti za kiutendaji, yakitolewa na kuingizwa barabarani wakati tofauti hizo zikitatuliwa? Hivi vita hiyo kati ya Dart na Udart inamfaidisha nani kama wananchi wanaolipa kodi zilizozaa mradi huo wanasota?

Tumeandika kwa mara nyingine kilio cha watumiaji wa usafiri huu tukiamini kwamba sasa mamlaka husika zitachukua hatua za haraka kukimaliza na hatutarajii kwamba hili haliwezi kumalizwa, tena kwa haraka.