http://www.swahilihub.com/image/view/-/4207130/medRes/402699/-/o89lbc/-/WaitituFed.jpg

 

Vuguvugu la umoja wa kumtimua Kabogo Kiambu lageuka mnara wa Babeli

Ferdinand Waititu

Ferdinand Waititu. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI na WANDERI KAMAU

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  16:15

Kwa Muhtasari

Muungano wa Kiambu ulioundwa 2017 kwa nia ya kumtimua mamlakani aliyekuwa gavana William Kabogo sasa uko mbioni kusambaratika baada ya kugeuka sasa kuwa wa kumpiga vita gavana wa sasa, Ferdinand Waititu.

 

MUUNGANO wa Kiambu ulioundwa 2017 kwa nia ya kumtimua mamlakani aliyekuwa gavana William Kabogo sasa uko mbioni kusambaratika baada ya kugeuka sasa kuwa wa kumpiga vita gavana wa sasa, Ferdinand Waititu.

Muungano huo ambao rasmi ulijulikana kama “United4Kiambu” ulimwandama Kabogo kwa hila na njama, ukizindua propaganda za kisiasa kwa ustadi mkuu na kuishia kumgeuza Kabogo kuwa kigae kisiasa.

Ni muungano ambao ulifanikiwa kumwangazia Kabogo kama mshirika wa siasa za Kinara wa Nasa, Raila Odinga na pia kuwa mtundu wa kimaongezi, kila kuchao kukitokea ‘ufichuzi’ wa jinsi Kabogo alikuwa akitoa matusi hapa na pale dhidi ya wapiga kura.

Kabogo alilemewa kabisa kujinasua kutoka kwa njama hizo na wakati wa kiama ulipofika, akajipata ameshindwa katika mchujo wa Jubilee na hatimaye hata baada ya kuteuliwa kuwa kinara wa wagombezi huru nchini na akagombea ugavana kwa kujitegemea, akaangukia pua.

Sasa, katika taswira wazi ya njia ya mhini na mhiniwa kuwa moja, baadhi ya viongozi waliokuwa ndani ya muungano huo na uliofanikiwa kumtoa mamlakani Kabogo sasa wanasema kuwa Waititu amegeuka kuwa dikteta ambaye haambiliki wala hasemezeki na pia anatumiwa rasilimali za Kiambu visivyo.

Muungano huo uliokuwa na mwakilishi wa wanawake katika bunge la kitaifa, Gathoni wa Muchomba, Naibu Gavana, James Nyoro na Kasisi David Ngare wakiwa washirika wakuu wa Waititu amtimue Kabogo sasa ndio wanaongoza njama kali za maangamizi ya Waititu kisiasa.

Kasisi Ngare ambaye anafahamika kwa kuwa na kampuni zake za uwekezaji ambao uko na utata na serikali wa Gakuyo na Ekeza amesema kuwa “Waititu alikuwa  mzuri tukifanya kampeni aingie afisini lakini akatugeuka baada ya kuafikia lengo hilo.”

Kasisi huyu anasema kuwa “kwa sasa Kiambu inahitaji ukombozi mwingine wa kisiasa ili kuwe na mwongozo wa kushauriana, wa haki na usio wa kudunisha wengine”.

Seneta wa Kiambu, Kimani wa Matangi tayari amemuonya Waititu kuwa “unatembea barabara telezi ya kisiasa na ambayo itakuelekeza kwa maangamizi.”

Amemuonya Waititu kuwa “usipobadili mtindo wako wa uongozi na uanze kufuata utaratibu uliowekwa kisheria basi mimi kama nyapara wa Kaunti kwa mujibu wa katiba ya Kenya, nitakuwa na shida sana na wewe”.

Wa Matangi ameteta kuwa Waititu anafanya maamuzi hata ya kifedha kwa msingi duni wa kujiwekea sharia zake kinyume na hali ya uadilifu wa kiutawala.

“Kwa mfano, hizi Sh2 milioni ambazo Waititu anatumia kwa siku kwa msingi kuwa anawasaidia vijana kujiepushana na ulevi ni kinyume na utaratibu wa ugavi wa rasilimali. Huwezi ukaanza kugawa pesa kwa umma kama njugu karanga bila kufuata utaratibu wa kisheria au kuweka mikakati ya kuhakikisha pesa zinatumika kwa lengo pana la kusaidia jamii,” akasema.

Waititu amekusanya pamoja vijana 5,000 wa Kiambu ambao kwa kila mmoja anawalipa Sh400 kila siku baada ya kuwapa kazi za kutekeleza usafi katika mitraa mbalimbali ya Kiambu.

Akitetea uamuzi huu, Waititu anasema kuwa mpango huo utaendelea mbele na utadumishwa kwa miezi sita ijayo na hatimaye wale ambao hawana taaluma yoyote, tuwahami na kozi katika taasisi zetu za kiufundi.

Akimjibu Wa Matangi, Waititu alisema kuwa hakuna shida yoyote kwa watu hao kupokezwa kitita hicho kwa siku “ikizingatiwa kuwa rasilimali za Kiambu ni haki kwa wote wa Kiambu, wawe ni matajiri au masikini au walio na tumbo kubwa au tumbo ndogo.”

Ni hivi majuzi tu ambapo Nyoro alitangaza hadharani kuwa Waititu ashampokonya afisi na gari rasmi na kwa sasa anahudumu tu kwa kujitolea bali sio katika ule ushirika wa umoja wa kumtimu Kabogo.

“Mimi ninanatangaza kuwa hakuna ushirikiano tena kati yangu na gavana Waititu nikiwa naibu wake. Amegeuka kuwa mtu wa wa kutuongoza kwa msingi wa udikteta na ukijaribu kumwambia kitu, huwa anakukemea. Ameteka nyara madiwani wengi na anathibiti bunge la Kaunti kwa vitisho na kutiana hofu,” akasema Nyoro.

Kwa upande wake, Wa Muchomba amejitokeza akisema kuwa ameandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Kiambu akiteta kuwa Waititu anamtishia maisha na kumhangaisha.

“Mnamo Juni 4, 2018 niliandikisha taarifa rasmi kuwa Waititu akitumia magenge ya vijana ananihangaisha na kunitishia maisha. Ni kiongozi ambaye amegeuka kuwa dikteta sawa na yule Herode katika Biblia aliyekuwa akiwakadamiza wote aliowaongoza kiasi kwamba hata idara ya Ujasusi (NIS) imenionya nichukue tahadhari kuhusu siasa zangu na pia maisha yangu kuhusiana na njama za Waititu dhidi yangu,” amesema.

Amesema kuwa njama hiyo ilijiweka wazi siku ya Madaraka Dei iliyopita ambapo “Waititu alikuwa amenipangia njama ya kupigiwa makelele na nipigwe mawe ikiwa ningejitokeza katika uwanja wa Ndumberi ambako alikuwa akiongoza sherehe za kuadhimisha hafla hiyo”.

Wa Muchomba aliteta: "Waititu amegeuka kuwa wa kutudunisha kama viongozi na ambapo hataki kuulizwa swali lolote la Kiambu na utawala wa kisiasa na akiona unasisitiza upewe jibu, anageuka kuwa hasidi wako kisiasa.”

Hata hivyo, Waititu amekanusha madai hayo akisema kuwa “hawa wako na njama fiche ya 2022 ambapo wanataka kusambaratisha utendakazi wangu ili nidunishwe machoni mwa wapiga kura wa Kiambu ili wanifurushe 2022.”

Amesema kuwa hajali na siasa hizo za “hao wanalialia kwa kuwa niko na tajiriba ya chaguzi tano nikishinda kura na ninafahamu vizuri kuhusu njama zao. Sijali na maneno hayo yao kwa kuwa kwa kukutana ni kwa debe baada ya kukadiriwa na wapiga kura kuhusu ufaafu wetu wa huduma kwa miaka mitano ambayo tuko afisini  katika awamu hii ya uongozi wa hadi 2022.”

Amesema kuwa kile kinachobishaniwa ni hela zipewe wakubwa wa Kaunti wala sio masikini wa Kaunti.

“Huyu Wa Muchomba ameanza makao yake ya kutibu walevi na anataka nimpe pesa za ufadhili. Ana pesa zake ambazo anapewa na serikali za kufadhili miradi yake. Asituone kama hatujui njama hizi anazoandaa za kutaka kutoa vitisho ili tuingiwe na kiwewe na tumpe pesa,” akasema.

Wa Muchomba ako na taasisi ya kurekebisha mienendo ya walevi kiholela na ambapo tayari ndani ya hifadhi hiyo ako na Martin Kamotho ambaye anafahamika na Wakenya wengi kama “Githeri Man.”

Kamotho alijipata katika vyombo vya habari na ufadhili kutoka kila pembe baada ya kunakiliwa na vyombo vya habari Agosti 8, 2017 akiwa foleni ya kupiga kura akiwa na mlo wake wa Githeri katika karatasi ya plastiki.

Sifa zake ziliishia kutuzwa na rais Uhuru Kenyatta lakini kwa upande wake ulevi ukamwandama hadi kugeuka kuwa ‘mgonjwa’ wa ulevi anayetibiwa kwa sasa katika kituo hicho cha Wa Muchomba.

Wa Muchomba anatoa onyo kuwa “sisi hatutakubali kutii uongozi usio na uwajibikaji kamwe”.

Anasema kuwa “chuma cha Waititu ki motoni na ni aidha abadili mienendo au ajipate hata naye akiandaliwa njama sawa na zile anazotekeleza dhidi yao kama viongozi wenza wa Kiambu.”

Pombe

Siasa na vita dhidi ya pombe haramu katika eneo la Kati zimegeuka kuwa kisiki kwa Gavana Ferdinard Waititu wa Kiambu, huku zikitishia mustakabali wake wa kisiasa.

Majuzi, gavana huyo amejipata kama yatima wa kisiasa katika kaunti hiyo, huku karibu viongozi wote katika kaunti hiyo wakimgeuka kwa kumtaja kama “msaliti.”

Miongoni mwa wale ambao wamejitokeza wazi kumkosoa ni Naibu Gavana James Nyoro, Mwakilishi wa Wanawake Gathoni Wamuchomba, Seneta Kimani Wamatangi, wabunge na baadhi ya madiwani.

Kama mtangulizi wake William Kabogo, Bw Waititu analaumiwa kwa kuendesha uongozi wa kaunti hiyo “kwa mabavu” huku baadhi ya viongozi wakidai kutishiwa maisha yao.

Miongoni mwa wale ambao wamejitokeza wazi kumkosoa ni Naibu Gavana James Nyoro, Mwakilishi wa Wanawake Gathoni Wamuchomba, Seneta Kimani Wamatangi, wabunge Kimani Ichungw’a (Kikuyu), Moses Kuria (Gatundu Kusini) na baadhi ya madiwani.

Hata hivyo, wachanganuzi wanasema kwamba mchipuko huo mpya una misukumo kadhaa, mojawapo ukiwa kumpiga vita Bw Waititu kwa dhana kuwa “mgeni” katika kaunti ya Kiambu, siasa zinazotokana na vita vyake dhidi ya pombe haramu katika kaunti hiyo na zile za 2022.

Wanasema kwamba wakazi wengi wa Kiambu wangali wanamwona Bw Waititu kama “mgeni kutoka Nairoi” ikizingatiwa kwamba ashawahi kuhudumu kama mbunge wa Embakasi.

“Siasa zinazoelekezwa Bw Waititu na viongozi wa Kiambu ni kufufua dhana kwamba yeye ni ‘mgeni’ kwa wakazi wa Kiambu, ili kuzua maasi zaidi kutoka kwa wananchi. Ni vita vya kisiasa vinavyoendeshwa kwa ukamilifu mkubwa ili kuhakikisha kwamba viongozi hao ‘asilia’ wanapata uungwaji mkono kutoka kwa wakazi hao,” asema Ndegwa Njiru ambaye ni mchanhanuzi wa kisiasa.

Bw Waititu aliwania kiti cha ubunge cha Kabete katika kaunti hiyo mnamo 2015 baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Bw George Muchai. Aliwania kwa tiketi ya chama cha Jubilee Alliance Party (JAP).

Baada ya ushindi huo, Bw Waititu alisema kwamba nia yake kuu ilikuwa kutumia nafasi hiyo kama jukwaa la kuzindua nia yake katika kuwania ugavana katika kaunti hiyo.

Lakini hata baada ya kumshinda Bw Kabogo, wachanganuzi wanaeleza kwamba Bw Waititu, aliyekubali msimbo wa “Baba Yao” kama jina lake halisi, ana kibarua kigumu cha kujinadi kisiasa ili “kukubalika kamili” na wakazi wa Kiambu.

“Uasi unaomwandama Bw Waititu pia unachangiwa na pengo la uasilia, kwani wengi wanamwona kama ‘mgeni’ aliyewageukia. Mwelekeo wa vita vyake ni ugeni dhidi ya wakazi asilia,” asema Bw Mwangi Muthiora ambaye ni mchanganuzi wa siasa za eneo la Kati.

Wanasema kuwa kuungana kwa viongozi hao dhidi yake kumlaumu kwa “vita” dhidi ya pombe haramu ni pia kunalenga kuzua taswira kwamba amewavamia wakazi hao kiuchumi.

“Kwa kumlaumu Bw Waititu kwa ‘kuingilia’ watengenezaji haramu, viongozi wanapalilia maasi zaidi dhidi ya Bw Waititu ili kuhakikisha kwamba wanabuni jukwaa la kuanza harakati za kumwondoa mamlakani,” asema Bw Muthiora.

Viongozi hao wanadai kwamba Bw Waititu anaendesha vita hivyo kwa njia ya kibaguzi, kwa msingi kwamba vinawasaza baadhi ya “watengenezaji wakubwa” wa pombe hizo.

Bi Wamuchomba pia amedai kwamba kuna genge la wanalifu lililobuniwab ili kumshambulia.

Kwa hayo, wachanganuzi wanasema kuwa huenda isiwe mshangao kwa kuibuka kwa hoja za kumwondoa Bw Waititu mamlakani.

“Wakati kuna vita dhidi ya tashwishi dhidi ya uasilia wa kiongozi, kuna uwezekano mkubwa sana kwake kung’olewa mamlakani. Ni hali sawa inayomwandama Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru, ambapo baadhi ya wakazi wanamwona kutokuwa mmoja wao,” asema Prof Ngugi Njoroge.

Zaidi ya hayo, wachanganuzi wanaeleza kuwa taswira hiyo pia inaashiria kinbarua kigumu kinachomwandama Rais Uhuru Kenyatta kuwaunganisha viongozi hao, kwani hiyo ndiyo kaunti anakotoka.