http://www.swahilihub.com/image/view/-/4396294/medRes/1940967/-/gdbwlc/-/herasa.jpg

 

Kipchumba, Cherotich washinda makala ya 11 ya Lake Maggiore Half Marathon

Daniel Kipchumba

Mkenya Daniel Kipchumba ashinda makala ya 11 ya Lake Maggiore Half Marathon nchini Italia, Aprili 15, 2018. Picha/HISANI 

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, April 16  2018 at  17:42

Kwa Muhtasari

Wakenya Daniel Kipchumba na Daisy Cherotich walianza maisha katika mbio za kilomita 21 kwa kishindo baada ya kushinda makala ya 11 ya Lake Maggiore Half Marathon nchini Italia, Aprili 15, 2018.

 

WAKENYA Daniel Kipchumba na Daisy Cherotich walianza maisha katika mbio za kilomita 21 kwa kishindo baada ya kushinda makala ya 11 ya Lake Maggiore Half Marathon nchini Italia, Aprili 15, 2018.

Walizawadiwa Sh124,413 kila mmoja kwa juhudi zao.

Kipchumba aliongoza Wakenya wenzake Mangata Ndiwa, Josphat Kiptoo na Joel Maina kuzoa nafasi nne za kwanza katika kitengo cha wanaume.

Alitumia dakika 59:06 kukata utepe.

Alimaliza sekunde moja mbele ya Ndiwa nao Kiptoo na Maina wakakamilisha kwa dakika 59:19 na saa 1:01:43, mtawalia. Ndiwa, Kiptoo na Maina walizawadiwa Sh 99,529, Sh74,641 na Sh49,761, mtawalia.

Wiki moja baada ya kuwekea Erick Kiptanui kasi na kumsaidia kushinda Berlin Half Marathon kwa kasi ya juu mwaka 2018 ya dakika 58:42 nchini Ujerumani, Kipchumba alifaulu kujishindia taji la Lake Maggiore katika hatua za mwisho.

Kipchumba, Ndiwa na Kiptoo walichukua uongozi baada ya kilomita tatu za kwanza.

Walikamilisha kilomita 10 kwa dakika 27:47 na kukamaliza kilomita tano zilizofuata kwa dakika 14:16.

Waliongeza kasi na kukamilisha kilomita tano zilizofuata kwa dakika 14:05 kabla ya Kipchumba kumzidi Ndiwa maarifa katika hatua ya mwisho na kunyakua taji.

Cherotich alibeba taji la wanawake kwa saa 1:09:44. Alifuatwa kwa karibu na Mkenya mwenzake Leonidah Jemwetich Mosop (1:10:26) naye Mswidi Charlotta Fougberg akafunga tatu-bora (1:11:58).