http://www.swahilihub.com/image/view/-/4801162/medRes/2137439/-/2xbsclz/-/pancho.jpg

 

Jinsi starehe za kisiwa cha Mbudya zilivyokatisha maisha ya Pancho Latino

Aliyekuwa mtayarishaji wa muziki, Joshua Magawa ‘Pancho Latino’  

Na Mwandishi wetu

Imepakiwa - Thursday, October 11  2018 at  12:34

Kwa Muhtasari

Ni kisiwa chenye upepo mwanana, miti ya kuvutia na mandhari nzuri

 

 

Dar es Salaam. Siku moja baada ya kifo cha mtayarishaji wa muziki nchini, Joshua Magawa maarufu Pancho Latino, baadhi ya mabaharia na wananchi wanaotembelea kisiwa cha Mbudya wamesema vifo vingi eneo hilo vinasababishwa na unywaji wa pombe kupita kiasi.

Pancho aliyejizolea umaarufu baada ya kutengeneza nyimbo kama Dar es Salaam Stand Up wa Chid Benz, Closer wa Vannesa Mdee, Baadaye Sana wa Mabeste na Amore wa Baby Madaha alifariki akiwa njiani kuwahishwa hospitali baada ya kuokolewa akizama.

Kaka wa Pancho, Aidan Magawa alisema mdogo wake alikutwa na mauti akiwa katika kazi zake kisiwani hapo.

Alisema mdogo wake amekuwa akifanya kazi za sanaa muda mrefu na alikwenda katika kisiwa hicho kwenye moja ya mihangaiko yake.

Mmoja wa marafiki aliyejitambulisha kwa jina moja la Amani alisema alikuwa na Pancho wakiogelea na ghafla mtu mmoja aliwashtua akiwauliza mbona mwenzao amekaa muda mrefu ndani ya maji na uso umeelekea chini ya maji.

Amani alisema kwa kuwa wanajua alikuwa hodari katika uogeleaji, walimwambia mtu huyo asiwe na wasiwasi kwa kuwa hiyo ni moja ya aina za uogeleaji wake. Hata hivyo, alisema dakika kadhaa zilipita bila kugeuka ndipo wakaenda kumuangalia na kugundua kuwa alikuwa akizama.

Alisema walimtoa na kumtapisha maji aliyokuwa ameyanywa, lakini walipomfikisha hospitali waliambiwa alikuwa amekwishafariki.

Vijana waendelea kujirusha

Jana Mwandishi Wetu aliyetembelea kisiwa hicho aliwashuhudia vijana wakivuta sigara na kunywa pombe wakati wa mchana. Kabla ya kuanza safari mhudumu wa boti inayosafirisha abiria kwenye kisiwa hicho aliwasisitizia wageni kuwa makini na kutosogea kwenye eneo lenye kibao kilichoandikwa ‘hatari’.

“Ndugu zangu mkifika kule msiogelee kwenye kibao kilichokataza pale kuna mkondo mkali wa maji na jana kuna mtu amefariki,” alisema mhudumu huyo.

Nauli ya kwenda Mbudya

Katika Hoteli ya Slipway, usafiri kwenda katika kisiwa hicho ni Sh30,000 kwa mtu mmoja na ili boti iondoke inapaswa kuwa na walau abiria wanaoanzia sita.

Katika Hoteli ya Whitesends nauli ya usafiri ni Sh10,000 kwa mtu mmoja na boti hutumia dakika 20 kufika. Watalii wa nje hulipa Sh26,000 wakati wale wa ndani hutozwa Sh2,500 ambazo hupokewa baada ya kuwasili kisiwani hapo.

Mmoja wa watumiaji wa bahari, Ally Hashim alisema watalii kutoka nje ya nchi wanaotembelea kisiwa hicho siyo wengi kama walivyo wa ndani. “Miaka ya hivi karibuni Watanzania ndiyo wamekuwa wengi zaidi, wageni ni wachache kwa sababu hawapendi kelele. Kwa hiyo soko la wazawa ndilo kubwa zaidi,” alisema Hashim.

Alisema kisiwa hicho ni eneo la starehe ambako ulevi, uasherati na kuogelea ndiyo mambo yanayotawala.

“Ni kisiwa chenye upepo mwanana, miti ya kuvutia na mandhari nzuri. Kwa hiyo mwisho wa wiki na hata siku za kawaida watu wengi sana wanakuja kula bata (kustarehe) huku,” alisema.

Matumizi ya pombe

Kwa sababu pombe ni kati ya starehe kwenye kisiwa hicho, baadhi ya wahudumu walisema ni rahisi kupoteza maisha ikiwa mtu ataogelea akiwa amelewa.

Walisema wakati mwingine baadhi ya watu hulazimisha kuogelea na kusogea kwenye eneo lenye mkondo mkali wa maji licha kukataliwa kufika eneo hilo.

“Unawezaje kuogelea ukiwa umelewa? Sasa kinachowaumiza wengi ni hicho, wanaingia kwenye maji wakiwa na pombe kichwani,” alisema mmoja wa wahudumu. “Mfano mimi nipo huku halafu mtu ameenda kwenye kile kibao (anaonyesha kibao) nawezaje kumuona? Cha ajabu utakuta amevua nguo na kutundika hapohapo kwenye kibao chenye katazo.”

Mmoja wa viongozi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Nasoro Mohamed alisema kwa kuwa si mzungumzaji, hawezi kueleza chochote kuhusu kisiwa hicho.

“Mkaongee na wakubwa wetu au wao wakiwaruhusu sisi ndio tutaweza kuzungumza nanyi. Hamtakiwi kupiga picha wala chochote huku,” alisema.