http://www.swahilihub.com/image/view/-/2947934/medRes/1170416/-/cphqe0/-/longo.jpg

 

Kiswahili hakitaendelezwa na wageni

Kongamano chuoni Rongo

Washiriki wa Kongamano la Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili Afrika Mashariki (CHAWAKAMA) lililoandaliwa katika Chuo Kishirikishi cha Rongo Novemba 7, 2015. Picha/HISANI 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, May 11  2018 at  09:52

Kwa Mukhtasari

Hatua ya mtandao wa Twitter kutambua na kuitumia lugha ya Kiswahili katika matumizi yake ni mwendelezo wa mitandao ya kimataifa kuona umuhimu na fursa zilizomo katika Kiswahili.

 

MTANDAO wa kijamii wa Twitter umeamua kutambua na kuitumia lugha ya Kiswahili katika matumizi yake.

Takribani wiki ya pili sasa mtandao huo umekuwa ukitumia twiti za Kiswahili (tweets) na kutoa tafsiri inayokaribiana kama ilivyo katika lugha nyingi za kigeni.

Hatua ya mtandao wa Twitter ni mwendelezo wa mitandao ya kimataifa kuona umuhimu na fursa zilizomo katika Kiswahili.

Awali mtandao wa Facebook nao uliona haja ya kutumia Kiswahili na sasa watumiaji wengi wanatumia mtandao huo kwa lugha ya Kiswahili.

Haya kwa hakika ni mafanikio makubwa na ya kihistoria, kwa kuwa yamekifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza miongoni mwa lugha za Kiafrika kutambulika na kutumiwa na mitandao hiyo yenye watumiaji wengi duniani.

Kujichomoza kwa Kiswahili miongoni mwa lugha nyingi za Bara la Afrika, ni ishara kuwa lugha hii ina upekee wa aina yake. Kama ni lugha, Afrika ina utitiri wa lugha zikiwamo baadhi kama vile Kihausa zinazoweza kukipa changamoto Kiswahili kimatumizi. Tukiri kuwa Twitter na Facebook zimekipa Kiswahili hadhi, kukitangaza, kukiendeleza, kukienzi na kuwafanya watu wengine kujifunza lugha hiyo.

Wakati baadhi yetu wakiwamo wale ambao Kiswahili ni lugha yao mama wakikinanga kwa kukiona hakina maana, lugha hiyo sasa inachanja mbuga kimataifa.

Kama wageni wameona thamani ya Kiswahili na kuamua kukipa nafasi hiyo ambao kimsingi ni sawa na kukienzi, sisi wenye lugha tunapaswa kukienzi maradufu, huku tukikipa thamani kubwa zaidi.

Hatua hii ituchochee kuona haja sasa ya kukitumia Kiswahili katika nyanja mbalimbali za maendeleo hususan elimu, sayansi na teknolojia.

Hatuwezi kusema wamiliki wa Facebook na Twitter wana mapenzi na Kiswahili, ni dhahiri kilichowasukuma ni baada ya kung’amua fursa ya kibiashara iliyopo kwa watumiaji wa lugha hiyo waliosambaa kona mbalimbali za dunia.

Hii ndiyo fursa ambayo kwa siku nyingi Watanzania hasa wataalamu wa lugha hiyo walipaswa kuing’amua na kuitumia.

Ni wakati sasa wataalamu wetu wa Kiswahili wafikiri nje ya mipaka ya Tanzania au Afrika Mashariki. Wanapaswa kuyafumbua macho na masikio kung’amua kila fursa ya Kiswahili iliyopo duniani.

Leo tunapoitazama taasisi ya kukuza lugha ya Kiingereza duniani (British Council), Alliance francais kwa Wafaransa, Goethe ya Wajerumani na Confucius ya Wachina, hizi zote ni matunda ya juhudi za wataalamu wa lugha hizo waliopata msaada wa mataifa yao.

Watanzania tunaweza hasa kwa kuzingatia kuwa Tanzania ndipo chimbuko la Kiswahili. Haiwezekani Kiswahili hiki kilichozaliwa Tanzania kikatamba kimataifa kwa jitihada za wasiokuwa Watanzania.

Nje ya juhudi za wasomi na wataalamu wa Kiswahili, lazima tukiri kuwa Serikali yetu nayo ina wajibu mkubwa wa kukiendeleza Kiswahili.

Hata hiyo mifano tuliyotaja awali ya taasisi za lugha zinazoongoza duniani, kwa kiasi kikubwa harakati zake zina mkono wa serikali za nchi husika.

Nasi tunaweza hasa wakati huu wa utawala wa Serikiali ya Awamu ya Tano, ambayo tangu iingie madarakani imejipambanua kikamilifu kama Serikali inayojali maendeleo ya Kiswahili.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647