http://www.swahilihub.com/image/view/-/4706288/medRes/2074879/-/vtijqlz/-/john.jpg

 

Kliniki za jioni kuongeza mapato Bugando

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella  

Na Jesse Mikofu

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  10:19

Kwa Muhtasari

Zaongeza motisha kwa madaktari wao ili wasiende nje

 

Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC) jijini hapa, imezindua kliniki za jioni, siku za mwisho wa wiki na sikukuu ili kuboresha huduma na kupunguza msongamano.

Mkurugenzi mkuu wa hospitali hiyo, Dk Abel Makubi alisema juzi kuwa mbali na kupunguza msongamano wa wagonjwa asubuhi, pia kliniki hizo zinasaidia kuongeza mapato.

Alisema awali, walikuwa wakitoa miadi ya muda mrefu kwa wagonjwa kuhudhuria kliniki kutokana na wingi wa watu lakini kwa sasa hali hiyo inapungua siku hadi siku.

“Wagonjwa wanaotoka mikoani walikuwa wakipata shida kubwa kwasababu wakati mwingine wanafika hapa (BMC) saa nane mchana, muda wa kawaida unakuwa umeisha, hivyo wanalazimika kurudi na kutumia gharama kubwa,” alisema Dk Makubi.

Pia, alieleza siri ya kufanikisha huduma hizo kwamba wameongeza motisha kwa madaktari wao ili wasiangaike kwenda kutafuta kipato cha ziada kwenye hospitali zingine.

Mkuu wa idara ya wagonjwa wa nje, Dk Nohrasco Mang’ondi alisema zilipoanzishwa kliniki hizo Novemba 2017, walikuwa wakiwahudumia wagonjwa kati ya 500 hadi 600 kwa mwezi lakini kwa sasa wanahudumia wagonjwa 2,000 kwa mwezi.

“Huduma hizi zinapatikana kuanzia saa tisa alasiri hadi saa mbili usiku kwa siku za kawaida, kwa siku za mwisho wa wiki na sikukuu zinaanza saa mbili asubuhi hadi saa nane mchana, wakati tunaanza tulikuwa na madaktari bingwa 16 lakini kwa sasa wapo madaktari 51 wanaowaona wagonjwa hao,” alisema Dk Mang’ondi ambaye pia ni mkuu wa idara ya magonjwa ya ngozi BMC.

Kabla ya kuzindua kliniki hizo hospitali hiyo ilianza kupima afya bure kwa wakazi wa mkoa huo.

Watu 274 walifanyiwa uchunguzi, 87 kati ya hao walipima saratani ya shingo ya kizazi, waliopima Virusi vya Ukimwi (VVU) ni 157, tezi dume walipima 25 na watano walipima ugonjwa wa selimundu.

Akizindua kliniki hizo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella alipongeza hatua hiyo inayolenga kutoa huduma bora na kuwashauri BMC huduma hizo zipatikane kwa saa 24.