Kodi TRA zinavyowatesa wajasiriamali nchini

Na Bledina Nyakeke

Imepakiwa - Wednesday, April 10  2019 at  11:29

 

Kwa muda mrefu Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikitilia mkazo wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kuwa wanajikwamua katika hali ya umaskini.

Kama ilivyo kwa nchi nyingine, Wataanzania wanajishughulisha na shughuli mbalimbali za kujipatia fedha wakiwamo walioajiriwa na waliojiari katika shughuli mbalimbali zikiwamo za kilimo na biashara.

Kwa upande wa wafanyabishara wapo wakubwa na wadogo ambao wote kwa pamoja wanalo lengo la kuboresha hali za maisha na kuchochea uchumi wa Taifa.

Ili lengo hilo litimie wanapaswa kuungwa mkono na wadau mbalimbali zikiwamo taasisi za umma ambazo zinahusika moja kwa moja kuwawezesha wananchi.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni miongoni mwa taasisi hizo za umma ambazo zinao wajibu wa kuhakikisha wajasirimali wanaandaliwa mazingira rafiki ili waweze kufanya biashara zao kwa faida na hatimaye kulipa kodi.

Hata hivyo, licha ya mamlaka hiyo kubeba wajibu huo mkubwa, bado imeshindwa kuwashika mkono wafanyabishara wadogo, badala yake imekuwa ni kikwazo kikubwa katika ukuaji wa wajasiriamali wadogo.

Mara nyingi TRA wamekuwa wakitoa elimu kwa umma juu ya masuala ya ulipaji kodi na umuhimu wake katika ujenzi wa Taifa. Katika mikutano hiyo wamekuwa wakijinadi kuwa kodi inayotozwa ni rafiki kwa wafanyabiashara kulingana na mtaji na hali halisi ya biashara. Lakini hali ni tofauti.

Mathalan ukifika katika ofisi za TRA kulipia kodi utakachokutana nacho ni tofauti na kile ulichoelezwa wakati maofisa wa kodi wanapotoa elimu kwa umma, hali hii imekuwa chanzo kikuu kwa baadhi ya wajasirimali na wafanyabiashara kufikiria njia mbadala hata kama siyo sahihi.

Kwa mfano huduma za ushuru wa forodha wa bidhaa zinazotolewa katika mpaka wa Tanzania na Uganda eneo la Mtukula ambako wafanyabiashara wengi hasa wadogo na wa kati hupitishia bidhaa zao kutoka nchini Uganda kuingia Tanzania katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kuna tatizo.

Hivi karibuni mfanyabiashara mmoja aliingiza bidhaa zenye thamani ya Sh1 milioni, na alipoonana na maofisa wa TRA kwa ajili ya kulipia ushuru, walimkadiria kulipa kiasi cha Sh499,000 kama ushuru wa forodha wa bidhaa hizo ambazo ni za viatu na mikoba ya akinamama ambayo haizalishwi hapa nchini kwa kuwa hakuna viwanda.

Huu ni mfano mmoja tu kwa wajasiriamali wadogo wengi ambao wao wameamua kutumia fursa ya uwepo wa mpaka huo sambamba na ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki, lakini wanakumbana na tozo kubwa ambazo haziendani na hali halisi ya biashara zao.

Kwa hali hii wafanyabiashara wengi wataendelea kutafuta njia za magendo ili kukwepa kodi ambazo si rafiki katika ukuaji wa biashara zao kwa kuwa hakuna mfanyabishara anayekubali hasara.

Wafanyabishara wote wanalo lengo la kupata faida katika shughuli zao, hivyo hakuna atakayekuwa tayari kulipia ushuru wa forodha na wakati huohuo anapaswa kulipa kodi ya mwaka ya TRA huku bado akiwajibika kulipa gharama nyingine za uendeshaji kama usafirishaji wa bidhaa zake.

Ni ukweli usiopingika kuwa hivi sasa biashara imekuwa ngumu na watu wengi wamefunga biashara, hivyo TRA inapaswa kujitathmini upya ili kuweka mazingira bora na rafiki kwa wafanyabiashara wadogo - lengo likiwa ni kuwawezesha kufanya biashara katika mazingira rafiki.

Kwa hali ilivyo sasa, TRA inaonekana kana kwamba inawaumiza badala ya kutengeneza mazingira mazuri ili kuwavutia wengi wakiwamo wale wanaotumia njia za panya ili waache na kuona umuhimu wa kulipa kodi kwa kwa hiyari.

Wafanyabishara wengi wamejiingiza katika mikopo kwa lengo la kujiongezea kipato, lakini matokeo yake wanajikuta wakitumia fedha nyingi kwa ajili ya kulipia kodi kubwa serikalini matokeo yake mitaji yao inaishia njiani na kubakia na madeni yasiyolipika.

Rai yangu kwa TRA ili kuvuka malengo ni vyema kuwa na uhusiano mzuri na wajasiriamali waliothubutu kujitosa kufanya biashara kwa kuwakadiria ushuru stahiki, badala ya kuwabambikizia kodi ambazo mwisho wa siku zinakuwa mzigo kwao na kuishia kufunga biashara.

Beldina Nyakeke ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Mara