http://www.swahilihub.com/image/view/-/5061788/medRes/1422166/-/baly54z/-/lema+pic.jpg

 

Kumbe Lema anakopesheka, hongera zake

Na Mwandishi wetu

Imepakiwa - Monday, April 8  2019 at  12:40

 

Afadhali wiki iliyopita imeisha. Afadhali sana. Bosi wa pale mjengoni Dodoma alikuwa amechachamaa kweli kweli. Katika soka tunaweza kusema alilazimisha kupiga hat trick. Yaani alifunga mabao matatu.

Kwanza alianza kwa kutangaza kupiga chini ushkaji wa chombo chake na ustaadhi wa masuala ya hesabu za kikubwa. Professa Assad.

Baada ya hapo akampiga nyundo yule dada mbunge mwenye sauti ya zege kwa kumsapoti ustaadhi. Halafu akampiga nyundo ya kichwa chalii wa Arusha, Godbless Lema asikanyage mjengoni kwake mpaka mwakani.

Ndani ya bao la tatu la Lema bosi huyu wa mjengoni Dodoma akataka kufunga bao jingine la kisigino kwa kumkata maini Lema na wafuasi wake. Akasema Lema ana mkopo mkubwa kweli bungeni. Shilingi milioni mia sita na ushee hivi. Bao hili la mwisho kwa mtazamo wangu nadhani limegoma.

Mkopo? Cha ajabu nini hapo? Ni moja kati ya mbinu bora za maendeleo na kujikwamua kiuchumi. Achilia mbali mikopo ya mjengoni lakini mule ndani kuna wabunge tena matajiri ambao pia wamekopa.

Ukija huku nje matajiri kibao wanaishi kwa mikopo. Sisi maskini kila siku tumekuwa tukisisitiziwa kukopa ili tufanye biashara tupate maendeleo na nchi ipate maendeleo.

Sitaki kujadili suala lenyewe binafsi lilifikaje bungeni lakini ukweli ni kwamba kauli ya mkuu wa mjengo imetuacha tukiwa na wivu na mbunge huyu wa Arusha.

Kumbe pamoja na ‘uhuni’ wake wote bado anakopesheka? Na kumbe anaweza kulipa deni analodaiwa?

Wakati fulani wakubwa wetu tangu tawala zilizopita huwa wanajisifu wakisema ‘Nchi yetu inakopesheka kwa wahisani’. Huu wimbo umekuwa ukisikika sana hata katika miaka ya karibuni.

Kama ni kweli tatizo linakuja wapi kama wabunge wa vyama vyetu vya siasa nao wakiwa na mikopo binafsi? Mimi nilidhani hii ni sifa nzuri.