Kumbe tumetofautiana katika aina ya ujanja tu

Na Edo Kumwembe

Imepakiwa - Thursday, April 11  2019 at  12:57

 

Macho yalikwenda kwa Ustaadhi Assad jana. Alikuwa ana makaratasi yake mezani akisoma vitabu. Sisi ambao tumeishia darasa la saba tulibakia tunatumbua macho tu; baadaye tukadhani anaigiza. Namba zilikuwa kubwa kubwa.

Watu wanapiga pesa. Hesabu zinatisha; nyingi zinaanzia mabilioni. Siku hizi bilioni imekuwa kama laki mbili tu. Watu hawauogopi ukali wa Namba Moja. Watu wanalipa pesa kununua vitu ambavyo havipo. Inafikirisha sana.

Kina Chadema, CCM wote wapo. Ni ndugu hawa ambao kila siku wanashindana kudai kwamba kila mmoja ndiye anayestahili kuikomboa nchi kutoka katika ujanja ujanja ambao unaendelea hapa na pale. Hakuna aliyenusurika mbele ya Assad. Wanaopaswa kuwa walinzi wa nchi nao wapo. Wanatofautiana katika aina ya ujanja tu. Huyu anajua lile, mwingine anajua hili.

Kuna wakati ilionekana kama vile ripoti ingehusu habari za trilioni 1.5. ahh wapi!. Kumbe kuna watu Hanang huko walikuwa wanajificha chini ya habari kubwa kama hizi, huku wakifanya mambo yao kimya kimya. Inaonekana ujanja ujanja umekuwa njia yetu ya maisha.

Lakini kwa sababu ripoti hii ipo ndani ya utawala wa Namba Moja unajiuliza jinsi ambavyo Watanzania wasivyo waoga. Yaani licha ya watu kupanda Kisutu kila siku, lakini kuna watu wala hawaogopi kutia hizi bilioni katika mifuko.

Hapo hapo unajiuliza, kwa wizi huu na ujanja ujanja huu, kwa nini pale Mjengoni hawataki kufanya kazi na mtu kama Ustaadhi? Kumbe anawasaidia kazi kwa kiasi kikubwa namna hii? Wakati mwingine tulioishia darasa la saba tunajiuliza kama kweli Watanzania wana nia ya dhati na nchi yao.

Kama tuna nia ya dhati basi kitu cha kwanza kabisa tusimsumbue huyu Assad na ofisi yake. Wizi wa kijinga tulidhani ungetoweka katika utawala huu lakini bado kuna watu hawana hofu na Namba Moja. Wanatazama hotuba zake jinsi anavyoongea kwa uchungu lakini wanacheka kichichini na kuendeleza mikakati yao ile ile ya miaka nenda rudi.

Kitu ambacho nilijiuliza ni kwamba inawezekana hata ofisi ya Ustaadhi nayo inahitaji ukaguzi. Si ajabu yeye akawa mtu safi lakini kuna watu chini yake nao wanapiga taratibu. Tunatofautiana katika ujanja tu.