Kutana na msomi anayeuza vyungu

Na  Mwandishi wetu

Imepakiwa - Thursday, April 4  2019 at  14:22

 

Changamoto zinaikabili jamii mara nyingi hutatuliwa na wenye maono tofauti. Kama wanavyofanya wengine, Ndaki Wanna (30) amejitosa kuwapunguzia wafugaji kuku gharama za kuendesha miradi yao.

Licha ya changamoto ya kupata vifaranga wa uhakika na bei kubwa ya chakula cha kuwakuza, joto huhatarisha maisha ya vifaranga hasa kwa wafugaji waio na umeme.

Kwa wafugaji wanaozingatia mambo yote yanayohitaji kukuza vifaranga, hupata hasara kubwa endapo watazembea kuwapa joto linalohitajika kwani baridi huviua.

Kukabialiana na hali hii, wapo wanaotumia umeme na wengine taa za chemli, jiko la mkaa au gesi ili kuongeza joto kwa vifaranga hao.

Kwa kuzitambua changamoto hizo, Ndaki ambaye ni mhitimu wa shahada ya uandishi wa habari na uhusiano wa umma anauza vyungu vinayoongeza joto kwenye mabanda ya kuku ili kuwapunguzia mzigo wafugaji.

Alianza biashara hiyo mwaka juzi akiwa na mtaji wa Sh80,000 kwa kununua vyungu 10.

“Nilienda kuuza kwa Sh12,000 kila kimoja na nikapata faida iliyonihamasisha kuendelea kuifanya zaidi biashara hiyo,” anasema Wanna.

Mpaka sasa mtaji wake umekua na anaagiza kati ya vyungu 30 hadi 35 kila baada ya wiki tatu au nne kulingana na mahitaji ya wateja.

Katika biashara hiyo, anasema changamoto iliyopo ni kuvisafirisha kwa umakini kwani kosa lolote linaweza kusababisha vikavunjika.

“Mbali na kuuza vyungu natotoleaha vifaranga pia. Malengo yangu ni kuwa mfanyabiashara mkubwa wa vyungu nitakavyovisambaza nchi nzima ili kuwarahisishia namna ya kuongeza joto kwenye mabada ya kuku wao,” anasema.