http://www.swahilihub.com/image/view/-/5053050/medRes/2299864/-/vt7342/-/mahiri+pic.jpg

 

Kutana na walimu mahiri wa tovuti ya kasome international

Na Elizabeth Edward, Mwananchi

Imepakiwa - Tuesday, April 2  2019 at  13:01

Kwa Muhtasari

Ni tovuti yenye lengo la kuwafundisha wanafunzi masomo ya sekondari

 

Upungufu wa walimu shuleni ni sababu mojawapo inayowafanya wanafunzi kuhangaika kutafuta msaada wa masomo ya ziada, hasa kutoka kwa walimu wanaosifika kwa umahiri wa kufundisha.

Kwa wanafunzi wa shule za sekondari za Dar es Salaam, neno Mchikichini ni maarufu kwao. Hili ni eneo lenye vituo kadhaa vya masomo ya ziada yanayotolewa na walimu wanaotajwa kuwa mahiri na msaada mkubwa katika ufaulu wa wanafunzi.

Majina maarufu hapo ni ya walimu kama Mbuga (Bailojia/Kemia), Aiden (Hisabati), Mudy (Fizikia) na Mtegetwa (Jiografia).

Ukiacha ufundishaji wa darasani, walimu hawa wanasifika katika utungaji wa maswali katika mitihani yao ambayo mara nyingi maswali hayo hutokea kwenye mitihani ya taifa. Sifa hizo na nyingine nyingi zinawafanya wanafunzi wakiwemo wa mikaoni kutamani kufundishwa na walimu hawa, lakini mazingira hayawaruhusu kutokana na umbali hivyo wachache huishia kusoma matini zilizoandaliwa tayari.

Mtandao wa kasome

Hilo ndilo lililomsukuma kijana Michael Sayi kuanzisha tovuti ya Kasomeinternational.com. Katika tovuti hii amewakusanya walimu wote wanaosifika kuwa ni wazuri na kufundisha kwa njia ya mtandao mada mbalimbali kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.

Kupitia programu hiyo yapo pia masomo yanayotolewa kwa wanafunzi wanaorudia mitihani na wale wanaofanya mitihani ya maarifa, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kujibu maswali na kufanya vizuri kwenye mitihani hiyo huku wakipata maarifa ya kutosha.

Sayi ameingia makubaliano na walimu hao na kazi kubwa anayoifanya ni kuwarekodi wakiwa wanafundisha na kuweka mafundisho hayo kwenye tovuti.

Sasa wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wanapata fursa ya kujifunza moja kwa moja kutoka walimu hao bila kujazana kwenye madarasa yao Mchikichini.

Kabla ya kuanza programu hiyo kijana huyu alianza kujifundisha upigaji picha za video, fani ambayo hakuwahi kuingia darasani, lakini kwa kuwa alikuwa na nia alihakikisha anajifunza na anaweza.

“Nilijifunza kupiga picha za video kama shughuli ya ujasiriamali lakini baadaye nikaona utaalamu huo naweza kuchanganya na teknolojia nikatengeneza kitu ambacho kinaweza kuwasaidia wanafunzi; hapo ndipo programu ya kasome ilipochukua nafasi,”anasema Sayi

Ubunifu huo wa tovuti ya elimu umemfanya Sayi ashinde tuzo ya mwaka ya Startupper iliyotolewa na kampuni ya Total kwa vijana wenye miradi ya kibunifu inayolenga kuinua kiwango cha elimu.

Nini kilimsukuma kuja na ubunifu huo

Akiwa mwanafunzi wa sekondari ya Kiluvya, Sayi naye alikumbana na changamoto hiyo ya kuhitaji kwenda kwa walimu hao mara kwa mara lakini alishindwa kutokana na umbali.

Haikuwa rahisi kwake kila siku kutoka Kiluvya kwenda Mchikichini kwa ajili ya kupata masomo hayo ya ziada ingawa mara moja chache alikuwa akijaribu.

Hakufanya vizuri kwenye mtihani wake wa kidato cha sita, kwa kile anachoamini hakuwa na msingi mzuri wa masomo na hivyo safari yake ya elimu ikakwamia hapo, kwa sababu familia yake haikuwa na uwezo wa kumsomesha tena.

“Baada ya kumaliza kidato cha sita nikafanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali, lakini bado akili yangu ikawa kwenye changamoto ya uhaba wa walimu na jinsi gani ambavyo wanafunzi wamekuwa wakiteseka kutafuta matini ya walimu wa Mchikichini,’’ anasema na kuongeza:

Ni ukweli usiopingika kwamba shule nyingi hasa za Serikali zina uhaba wa walimu na hilo ndilo linalowafanya wanafunzi kwenda kutafuta walimu wa ziada Mchikichini; sasa walio mbali wanafanya nini ndio nikafikiria kuanzisha hiyo programu ili kuwasaidia wote wenye uhitaji na wenye uwezo wa kufikia teknolojia.”