Kwa nini wananchi wanakimbilia kuuza kahawa Uganda?

Msemaji wa jeshi la polisi, Barnabas Mwakalukwa  

Imepakiwa - Wednesday, October 10  2018 at  16:13

Kwa Muhtasari

Polisi watakiwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za misingi ya ajira zao

 

Akiwa mkoani Kagera katika ziara ya kikazi kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifika katika kiwanda cha kukoboa kahawa cha Nkwenda wilayani Kyerwa ambako alizungumzia biashara ya magendo ya zao hilo.

Katika hotuba yake wakati akizungumza na wananchi sehemu hiyo, Waziri Mkuu alieleza namna zao hilo la biashara linavyovushwa nje ya nchi na kuuzwa nchini Uganda kwa njia za panya kupitia Kumisongo, Kashaijo na Omukatoma huku wahusika wakidaiwa kusindikizwa na maofisa wa polisi.

Pia alieleza kuwa utoroshaji nje zao hilo wilayani Kyerwa umefikia hatua mbaya kiasi kwamba hadi vigogo wa polisi wanahusika na akamtaja kamanda wa polisi wa wilaya hiyo, Justine Joseph na kumuonya kuwa asipojirekebisha anaweza kupoteza kazi.

Hata hivyo, msingi wa kauli hiyo ya Waziri Majaliwa ni namna biashara ya magendo ya zao hilo ilivyoshika kasi ikipata msukumo kutoka kwa maofisa wa polisi.

Muda mfupi baada ya kauli hiyo, Jeshi la Polisi liliitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kuelezea hatua lilizochukua dhidi ya Justine. Msemaji wa jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa alieleza kuwa Joseph amehamishiwa mkoani Iringa kwenda kuwa chini ya uangalizi maalumu wa kamanda wa polisi wa mkoa huo wakati uchunguzi wa tuhuma dhidi yake ukifanywa.

Jeshi hilo lilikwenda mbali zaidi na kuwaonya maofisa wake kuacha kujihusisha kusaidia ufanikishaji wa biashara haramu huku likiwataka kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za misingi ya ajira zao.

Muda mfupi baada ya mkutano huo wa ACP Mwakalukwa na wanahabari, Ofisi ya Rais kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilitoa taarifa ikieleza kuwa Rais John Magufuli ameagiza maofisa wa polisi kuanzia kamanda wa mkoa huo, mkuu wa polisi Wilaya ya Kyerwa, mkuu wa upelelezi wa wilaya na mkuu wa kituo cha polisi Kyerwa wasimamishwe kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo.

Tunaunga mkono na kupongeza hatua zilizochukuliwa za uwajibikaji kwa viongozi waliopewa dhamana ya kulinda masilahi ya umma.

Hata hivyo, sambamba na pongezi hizo, tunaitaka Serikali kufanyia kazi na kuondoa sababu zinazowafanya wakulima na wafanyabiashara wa kati kuuza zao hilo nje ya nchi. Tunasema hivyo kwa sababu iwapo sababu ya wao kutafuta soko nje ya nchi - tena kwa njia ya panya ni kufuata bei nzuri, basi Serikali iangalie namna ya kulifanyia kazi haraka suala hilo ili kuwafanya wakulima waridhike na bei itakayopangwa nchini.

Iwapo suala ni wingi wa zao hilo kiasi cha bei kushuka katika soko nchini, basi iangalie namna bora ya kuratibu biashara hiyo ilimradi wakulima wasikae na mazao kwenye maghala yao na pia wauze kwa bei nzuri. Hatua hiyo itasaidia kuwawezesha wakulima kuboresha maisha yao.

Tunayasema haya kwa sababu kwa miaka mingi mkoani Kagera biashara ya magendo ya kahawa imekuwapo na kila mara licha ya hatua kadhaa kuchukuliwa, hivyo tunadhani umefika wakati wa kutafuta suluhisho la kisayansi la tatizo hilo.

Hivyo basi tunapohitimisha tunaziomba mamlaka husika ziangalie namna ya kuwawezesha wananchi hususan wakulima kuondokana na tamaa ya kuuza kahawa yao na mazao mengine nje ya nchi na badala yake kuuza ndani na kulinufaisha soko la ndani.

Wakati tukitafuta mwarobaini wa changamoto hiyo, tunasisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria, kanuni na taratibu tulizojiwekea katika udhibiti wa uuzaji wa zao hilo nje ya nchi.