Liwepo jicho zaidi usafiri wa bodaboda nchini

Imepakiwa - Tuesday, April 23  2019 at  11:59

 

Usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda umekuwa msaada mkubwa katika maeneo mbalimbali nchini hususani yale yaliyokuwa na changamoto ya kutofikika kwa urahisi.

Wakazi wa mijini na vijijini hivi sasa ni mashahidi wa hilo kwani katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza au Mbeya suala la mtu kutoka sehemu moja kwenda nyingine limekuwa rahisi zaidi ikilinganishwa na miaka 15 nyuma, na moja ya sababu ni uwepo wa bodaboda.

Si usafiri pekee, bodaboda pia zimetoa ajira kwa maelfu ya vijana ambao wameendelea kuwa msaada katika familia zao na kuchangia ukuaji wa pato la Taifa.

Hata hivyo, licha ya faida zote hizo, bodaboda zinatajwa kusababisha vifo vya watu 8,004 kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita. Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslim anasema idadi hiyo ya vifo inatokana na rekodi za kuanzia mwaka 2009 hadi 2018.

Muslim aliyekaririwa na gazeti hili, toleo la jana anasema katika kipindi hicho ajali za pikipiki zilifikia 37,421 zilizosababisha majeruhi 35,231. Hata hivyo, kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2016 hadi 2018 ajali zilipungua kutokana na juhudi mbalimbali zilizochukuliwa ikiwamo operesheni za ‘kamata viroba na nyakuanyakua’.

Kwa kifupi madhara ya ajali za bodaboda yameendelea kuwa mwiba kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa kutokana na kupoteza maisha ya watu wengi ambao ni nguvu kazi iliyotarajiwa kuendeleza familia, huku wengine wakibaki na ulemavu wa kudumu, hivyo kuwa tegemezi wakati walikuwa wakitegemewa na jamii zao.

Jambo hili halipaswi kuendelea kushughulikiwa kwa mazoea, juhudi na mikakati iwekwe kukabiliana na vifo, ulemavu na athari mbalimbali zinazotokana na ajali za bodaboda. Juhudi hizo zihusishe jamii nzima bila ya kuuachia upande fulani uwajibike.

Dereva wa bodaboda anapaswa kuwa wa kwanza kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kujilinda binafsi na abiria aliyembeba kwenye chombo chake, na kwa kufanya hivyo atakuwa ametimiza wajibu wake kuepusha ajali na kulinda maisha.

Kwa upande wa abiria wanaotumia usafiri huo wazingatie miongozo na taratibu ikiwamo uvaaji wa kofia ngumu (helmet) ambazo zimekuwa msaada mkubwa kupunguza madhara pindi ajali zinapotokea. Baadhi ya abiria hususani wanawake wamekuwa wakitajwa kukataa kuvaa kofia hizo wakihofia kuharibu mitindo ya nywele zao.

Ni vyema ifahamike kuwa usalama ama wa abiria au dereva wa bodaboda unapaswa kuanza kusimamiwa na yeye mwenyewe tena bila ya kushurutishwa, na iwapo hilo litatekelezwa hakuna shaka kuwa juhudi za kukabiliana na ajali zitafanikiwa.

Kwa upande wa askari wa usalama barabarani ambao ni wadau muhimu katika kusimamia sheria wajiongeze zaidi kwa kushirikiana na wadau wengine, wageukia pia kuongeza utoaji elimu kwa wananchi kama mkakati mmojawapo wa kudhibiti ajali.

Hakuna ubishi kuwa waendesha bodaboda wengi ni vijana wa umri mdogo, tena wengine hufundishana mitaani bila ya uangalizi na usimamizi wa kitaalamu, hivyo iwapo watapatiwa elimu watakuwa mahiri na bora zaidi katika utoaji wa huduma hiyo.

Ni vyema mamlaka zinazohusika zikalichukulia kwa uzito wake suala hili kwa sababu pikipiki zinazidi kuongezeka nchini.