Lugha ya maandishi na ya mazungumzo

Na Stephen Maina

Imepakiwa - Thursday, May 9  2019 at  12:36

 

Makala ya leo yanahusu makosa yanayotokana
na utamkaji wa maneno ya Kiswahili
Baadhi ya makosa yanayojitokeza yanatokana
watangazaji kuathirika na lahaja za Kiswahili
ambazo bado hazijasanifiwa, pia lugha za asili
na zile za kigeni. Mwanahabari anatakiwa awe
makini sana anapoandika na pia anapotangaza
kwenye redio na runinga. Nitatoa mifano
michache.
a) Kuchanganya herufi p na b
Tusiseme bonda bali iwe ponda
Tusiseme pasi badala ya basi
b) Kuchanganya z na s
Tusiseme guza badala ya gusa
Tusisema lasima badala ya lazima
Tusiseme chesa badala ya cheza.
c) Kuchanganya f na v

Tusiseme mtu amevutwa kazi badala ya
mtu amefutwa kazi.
d) Kuchanganya r na l
Tusiseme chakura kizuri badala ya kusema
chakula kizuri.
Tutofautishe kati ya mahali (sehemu au
eneo) na mahari (posa au tozo kwa ajili ya
kuoa).
e) Sauti ya t na ch
Katika baadhi ya lahaja za Kiswahili sauti ya
ch hubadilishwa na kuwa t kwa Kiswahili
sanifu. Kwa mfano katika lahaja ya Kimvita
inayozungumzwa pwani ya Kenya maneno
timbo la mawe yatatakiwa kuandikwa
chimbo la mawe; samaki aina ya tewa
husemwa samaki aina ya chewa.
Tukua mzigo iwe chukua mzigo.
Utungu wa kuzaa ni uchungu wa kuzaa.
f) Yako makosa ya kuweka herufi n kwa
baadhi ya maneno. Hali hii inatokana na
lugha ya mazungumzo na hasa lugha za
bara. Kwa mfano:

Ndini badala ya dini
Ngeuka badala ya geuka
Ngari badala ya gari,
g) Makosa ya kuchanganya sauti ya th na dh.
Kwa mfano:
Tusitumie idhibati badala ya ithibati
Tusiseme adhirika badala ya athirika
h) Makosa ya kuchanganya g na gh.
Kwa mfano:
Kitabu kimenigarimu badala ya kitabu
kimenigharimu
Luga badala ya lugha.
i) Sauti sh na ch
Tusiseme pashika bali pachika
Tusiseme mshele bali mchele
j) Sauti ya dh na th
Tusiseme idhibati bali ithibati
Tusiseme dhamani bali thamani
k) Sauti ya gh na k
Tusiseme bei kali bali bei ghali
Tusiseme kala la nafaka bali ghala la
nafaka.

l) Sauti ya g na j : Tusiandike agenda bali
ajenda
Tusiseme somo la Biologia bali ni somo
la Biolojia

m) Kuondoa na kuongeza irabu:
Kwa mujibu wa misingi ya uandishi wa
maneno ya Kiswahili, maneno takriban yote
huishia kwa irabu. Hata hivyo yako maneno
machache sana ya Kiswahili ambayo
hayaishii kwa irabu kwa mfano mathalan,
takriban, hususan. Vilevile yako maneno
yanayotakiwa kuishia na irabu. Kwa mfano
maneno yafuatayo yanaishia kwa irabu /u/
kama maalumu, salamu, mwalimu,
mtaalamu, nk.
n) Pia neno neema lisiandikwe nema,
rehema siyo rehma, azima badala ya azma,
riziki badala ya rizki, rutuba badala ya rutba,
nk.
n) Epuka kuongeza viambishi kama ma
mbele ya maneno hasa yale yenye asili ya
kigeni. Hili ni tatizo linalojitokeza katika

hotuba za viongozi wa siasa. Baadhi yao
hutoa hotuba zilizohaririwa na wengine
hutoa hotuba ambazo ni za moja kwa
moja.
Ni lazima kuihariri kazi ya kiongozi kwa
lengo la kutekeleza wajibu wako kama
mwandishi bora.
Wako wanasiasa na pia wataalamu wa fani
mbalimbali wanaotumia maneno kadhaa ya
Kiswahili ama kwa kuongeza au kupunguza
viambishi vya awali: Kwa mfano yako
maneno kama mapungufu badala ya
upungufu, maamuzi badala ya uamuzi,
mashirikiano badala ya ushirikiano, mashule
badala ya shule, mahospitali badala ya
hospitali, mabenki badala ya benki,
manunuzi badala ya ununuzi.
Kwa mujibu wa maadili ya kazi ya uandishi
ni lazima kufanya masahihisho bila kujali
hadhi ya mzungumzaji au mwandishi.
0754 861 664
Stphenjmaina@tz.nationmedia.com