http://www.swahilihub.com/image/view/-/4759168/medRes/1129070/-/4f97r0z/-/lukuvi.jpg

 

Lukuvi amtimua afisa ardhi kwa kumilikisha ardhi kinyume cha sheria

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi    

Na Mwandishi wetu

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  12:57

Kwa Muhtasari

Alisaini hati za kimila ili kumilisha ekari zaidi ya 1,500 za kijiji kwa watu binafsi kinyume cha sheria

 

Monduli. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameagiza kufukuzwa kazi kwa ofisa ardhi wa Wilaya ya Monduli, Kitundu Mkumbo kwa kukiuka sheria na taratibu za utoaji wa hati miliki za kimila.

Waziri Lukuvi ametoa agizo hilo mbele ya wakazi wa Kijiji cha Engarooji wilayani Monduli mkoani Arusha ambao wamekuwa katika mgogoro wa ardhi kwa muda mrefu na kugawanyika katika makundi mawili.

Katika mkutano huo wananchi walimueleza Lukuvi kwamba ofisa huyo alisaini hati za kimila ili kumilisha ekari zaidi ya 1,500 za kijiji kwa watu binafsi kinyume cha sheria.

Alisema mwenye mamlaka ya kumilikisha mtu ardhi zaidi ya ekari 50 ni Rais pekee.

“Ofisa huyu wa ardhi ambaye japo hapo awali mlishawahi kumsimamisha kazi kwa makosa mengine kama haya, lakini makosa haya ni makubwa na sasa afukuzwe kazi, haiwezekani amilikishe ekari zaidi ya 1,500 kinyume na sheria,” alisema Lukuvi.

Awali waziri Lukuvi amezifuta hati zote za kimila zilizotolewa na ofisa huyo kwa sababu zimetolewa kinyume na utaratibu kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya mwaka 1999 ambayo hairuhusu kutoa hatimiliki za kimila zaidi ya ekari 50 bila idhini ya Rais.