MASHAIRI YA MALUMBANO

Na  Gora Haji

Imepakiwa - Thursday, April 4  2019 at  09:37

 

Shairi la Malumbano limetungwa na gwiji wa mashairi kutoka Kisiwani Tumbatu huko Zanzibar kwa jina la Haji Ghora. Alizaliwa Mtaa wa Kokoni, Kisiwa cha  Tumbatu mwaka 1933.

Haji Gora anaamimi kuwa mashairi ya malumbano  ni mtindo wenye faida nyingi. Kwanza ni kwa ajili  ya kuwa na mafumbo ili kufumbuliwa. Hatua hii inasaidia uelewa na kukuza kiwango cha uchambuzi. Pili husaidia kujenga kiwango cha kujenga hoja. Tatu huweza kuchota elimu ya uchangiaji na usambaza kwa umma.

Kwa utamaduni wa Waswahili, mashairi ya malumbano yapo  sehemu nyingi. Kwanza kwenye ngoma za asili, ambapo wale manju hurushiana vipande na kujibizana na mashabiki wakishangilia.

Mwaka 1998 kulipotokea ugonjwa wa kipindupindu, Haji Gora aliandika mashairi na kuanza kujibizana na mshairi kutoka Mkoani Pemba kwa jina la Ali Khamis Kijogoo. Aliandika:

Kijogoo wachekesha siki ya nakubarizi,

Weya funga madirisha, kwa kuhofu majambazi,

Kinacho niajabisha, mbona milango iwazi,

Usidharau milango, ndio stara ya nyumba.

Kijogoo hakumwacha tuli Haji Ghora na hiki ni kimoja ya vipande vya jawabu lake katika kuendeleza malumbano hayo kuhusiana na madhara ya kipindupindu.

Alijibu:

Leo naja jibu wazi, Gora  alivyonieleza,

Alipata bumbuazi, akaona miujiza,

Kuwacha milango wazi, madirisha nikakaza,

Sikuwa nijipumbaza, kuwacha milango wazi.

Mshairi mwingine aitwaye Juma Machano wa Kinazini, Nungwi,   alianzisha malumbano kutaka kujua Chunusi ni nani. Aliandika shairi lililoitwa Chunusi ni nani mwaka 1996.

 Chunusi kiumbe Gani ?

Bismilahi naanza, kwa jina la Rahmani,

Hii si mara ya kwanza, kwa kushiriki mitamboni

Ingawa kwa kuuliza, naomba nipokeeni

Chunusi kiumbe gani na wapi anapoishi?

Gora alichukua kalamu na kumjibu ni kiumbe jini  kwa beti aliyoandika:

Mtitiri nimekuja, haraka bila kubeza

Penye redio Unguja, mahiri nimechomoza,

Chunusi uliyeuliza, Jawabu kukieleza,

Sikiya bila kungoja, huyu kiumbe jini.

 Haji Gora alifanya malumbano mengine na mshiriki mwingine Musa Juma Musa aliyekuwa anaandikia gazeti moja la Jua lililochapishwa Ujerumani aliyeandika shairi la Nisaidieni 

 Aliandika

Mwenzenu umenikaa, ulinzi huu mashaka,

Nina mtoto nalea, pabaya ataniweka,

Kutwa kucha analia, sitambui pa kushika,

Nisaidiwe ulezi, mwenzenu, umenikaa.

Haji Gora alimjibu:

Mwana uwapo walea, kwa vitimbi humuwezi,

Bado ya kuvumiliya, Fwata yangu uwamuzi,

Utapo mng’ang’ania, mwenyewe unajihizi,

Huleya alelekaye, huyo mrudishe kwao.

Katika kiendeleza hoja hii, mshairi ajulikanaye kama Jiwe Jeusi wa Tanzania Bara aliandika:

Pigo la mke viboko na pia kipande kimoja cha khanga.

Lakini Haji Gora anajibu:

Ni makofi na viboko, pigo la mke si vazi,

Kusudi aniite nyoko, na kuwatusi wazazi,

Halafu nimpe heko, kwa doti mekuwa chizi,

Anaendelea:

Shehe Mwinyi avumaye, afiko wazo lako,

Kwa aolewae, makofi sio tambiko

Pigo la mke avae, vizuri kila aliko.

Mke hapigiwi khanga, na kila yanayo heko.

Ni wajibu kumjenga, kwa mazuri matamko,

Unapomuengaenga, hatohisi kwengineko.

Hata kama akutusi, muonyeshe kauli yako,