MASHAIRI YA MALUMBANO

Imepakiwa - Thursday, May 9  2019 at  12:45

 

Shairi la Malumbano limetungwa na gwiji wa mashairi
kutoka Kisiwani Tumbatu huko Zanzibar kwa jina la Haji
Ghora. Alizaliwa Mtaa wa Kokoni, Kisiwa cha Tumbatu
mwaka 1933.
Haji Gora anaamimi kuwa mashairi ya malumbano ni
mtindo wenye faida nyingi. Kwanza ni kwa ajili ya kuwa
na mafumbo ili kufumbuliwa. Hatua hii inasaidia uelewa
na kukuza kiwango cha uchambuzi. Pili husaidia kujenga
kiwango cha kujenga hoja. Tatu huweza kuchota elimu ya
uchangiaji na usambaza kwa umma.
Kwa utamaduni wa Waswahili, mashairi ya malumbano
yapo sehemu nyingi. Kwamza kwenye ngoma za asili,
ambapo wale manju hurushiana vipande na kujibizana na
mashabiki wakishangilia.
Mwaka 1998 kulipotokea ugonjwa wa kipindupindu, Haji
Ghora aliandika mashairi na kuanza kujibizana na mshairi
kutoka Mkoani Pemba kwa jina la Ali Khamis Kijogoo.
Aliandika:
Kijogoo wachekesha siki ya nakubarizi,
Weya funga madirisha, kwa kuhofu majambazi,
Kinacho niajabisha, mbona milango iwazi,

Usidharau milango, ndio stara ya nyumba.

Kijogoo hakumwacha tuli Haji Ghora na hiki ni kimoja ya
vipande vya jawabu lake katika kuendeleza malumbano
hayo kuhusiana na madhara ya kipindupindu.
Alijibu:
Leo naja jibu wazi, Ghora alivyonieleza,
Alipata bumbuazi, akaona miujiza,
Kuwacha milango wazi, madirisha nikakaza,
Sikuwa nijipumbaza, kuwacha milango wazi.

Mshairi mwingine aitwaye Juma Machano wa Kinazini,
Nungwi, alianzisha malumbano kutaka kujua Chunusi ni
nani. Aliandika shairi lililoitwa Chunusi ni nani.
Kiumbe gani chunisi .
Bismilahi naanza, kwa jina la Rahmani,
Hii si mara ya kwanza, kwa kushiriki mitamboni
Ingawa kwa kuuliza, naomba nipokeeni
Chunusi kiumbe gani na wapi anapoishi?

Gora alichukua kalamu na kumjibu ni kiumbe jini kwa
beti aliyoandika:
Mtitiri nimekuja, haraka bila kubeza
Penye redio Unguja, mahiri nimechomoza,
Chunusi uliyeuliza, Jawabu kukieleza,
Sikiya bila kungja, huyu kiumbe jini.
Haji Gora alifanya malumbano mengine na mshiriki
mwingine Musa Juma Musa aliyekuwa anaandikia gazeti
moja la Jua lililochapishwa Ujerumani aliyeandika shairi
la Nisaidieni
Aliandika
Mwenzenu umenikaa, ulinzi huu mashaka,
Nina mtoto nalea, pabaya ataniweka,
Kutwa kucha analia, sitambui pa kushika,
Nisaidiwe ulezi, mwenzenu, umenikaa.
Haji Gora alimjibu:
Mwana uwapo walea, kwa vitimbi humuwezi,
Bado ya kuvumiliya, Fwata yangu uwamuzi,
Utapo mng’ang’ania, mwenyewe unajihizi,
Huleya alelekaye, huyo mrudishe kwao.

Katika kiendeleza hoja hii, mshairi ajulikanaye kama Jiwe
Jeusi wa Tanzania Bara aliandika:
Pigo la mke viboko na pia kipande kimoja cha khanga.
Lakini Haji Gora anajibu:
Ni makofi na viboko, pigo la mke si vazi,
Kusudi aniite nyoko, na kuwatusi wazazi,
Halafu nimpe heko, kwa doti mekuwa chizi,
Anaendelea:
Shehe Mwinyi avumae, afiko wazo lako,
Kwa aolewae, makofi sio tambiko
Pigo la mke avae, vizuri kila aliko.

Mke hapigiwi khanga, na kila yanayo heko.
Ni wajibu kumjenga, kwa mazuri matamko,
Unapomuengaenga, hatohisi kwengineko.

Hata kama akutusi, muonyeshe kauli yako,
Matumizi na libusi, mpe kwa ongezeko,
Ukumeleza basi, yabaki manung’ung’uniko

Pindi kimfumania, aucheze mdundiko,
Ajue kakusudia, kuirusha roho yako,
Usije mng’ang’nia, mwache aende atakako.

Makofi jozi kwa jozi, mbali ngumi na viboko,
Mwanamke kumuhizi, unakiuka miiko,
Hata punda mchukuzi, hapewi hivyo vituko.

Kwa zilivyo desturi, ndani ya mtiririko,
Haitakuwa fakhari, kumpiga mke wako,
Na iwapo hakukiri, duniani wangalipo.

Siwafundishi vijana, yasokuwa na mashiko,
Katu sio uungwana, kumpiga mke wako,
Akiwa ni wako mwana, huwaje moyoni mwako?
Shehe watangaza vita, kuwachongea wenzako,
Waume wenye matata, kwa maelekezo yako,
Wake zao watajuta, kwa kupata masumbuko.

Wewe unategemewa, mwambao na kwingineko,
Kila unalolitowa, kwa wengine ilimwiko
Jaribu kujikosowa, kwenye yako matamko.
Kiitikio:
Pigo la mke si makofi na viboko, pigo la mke ni vazi.

KADHIA YA MAZIMWI
Haji Ghora alianza kutupiana vimondo na magwiji wa
mashairi akiwamo Ameir Anandenga wa Dar es Salaam.
Tungo yenyewe ilikuwa kama hivi:

Mazimwi viumbe gani, nambieni mjuawo,
Haraka nitajieni, pasiwe na mshangao,
Ni wapi ulimwenguni kwamba huko ndiko kwao.

Kuna nyingi simulizi, kuhusu viumbe hao.
Kauli zile na hizi, sisi tusimuliwao,
Habari za bmuwazi, kwa kutojua makwao.

Wanaotusimuliya, Mazimwi wasifu wao,
Husema wana mikiya, na pembe vichwani mwao,
Na meno yanayozidiya, pamwe na makucha.

Ukiwapigia ngoma, huridhika nyoyo zao,
Mfano kama Wanyama, hulana wao kwa wao,
Mazimwi ukiwapima, ni ipi jamii yao?

Wao wanahadithiya, Mazimwi habari zao,
Kwa vile zao hisia, Huwa kama kwaba ndio,
Wanavyotuashiria, kwamba ni mfano wao.

Usiku wanapolala, kubwa sana zogo lao,
Mayowe pasi muhula, huzidi wakati huo,
Kaka sauti kiza, Darisalama mwambao.
Andanega sitobeza, wewe ndio wetu ngao,
Nijile kukuuliza, mazimwi ni watu kwao.

Kiitikio
Mashairi mtungao, Mazimwi viumbe gani?
Andanenga hakuchelewa akachukua kalamu na karatasi
na kuandika beti za kumjibu Haji Ghora na ulizo lake
kuhusu shairi la Mazimwi.

Bwana Haji Ghora Haji, kwangu mimi amekuja,
Toka Chumbu kitongoji, cha Unguja nakitaja,
Kaja hapa kwenye jiji, kuniletea viroja,
Ameniomba kutaja, Mazimwi viumbe gani.

Mazimwi viumbe gani, ameniomba kutaja,
Ni swali la makini, si vizuri kulifuja,
Kwetu hawaonekani, labda huko Unguja,
Ameniomba kutaja, Mazimwi viumbe gani

Ndugu yangu Bwana Ghora, Jawabu la yako hoja,
Ni viumbe vya kuchora, yaelezwa na wataja,
Watajwa wa misogora, na mizuka lao tija,

Ndivyo wao nawataja, Mizimwi viumbe gani.

Viumbe wa mawazoni, havonwi nasi waja,
Wenye akili razini, si viumbe ni miuja,
Vipandishwavyo pungoni, hudanganya wamekuja
Kwa uzui wanataja, Mazimwi viumbe gani.

Zimwi kiumbe refu, unene wake mapaja,
Nyangumi kumi alifu, hubwakia kwa pamoja
Kwake sawa na kinofu, kisokidhi yake haja,
Hutaja wanao taja, Mazimwi viumbe gani.

Zimwi sawa na shetani, au juja wa majuja,
Watajao vitabuni, mawe wanayobuguja,
Hadi siku ya ilani, mpiga panda kikija,
Na wa mizuka hutaja, Mazimwi viumbe gani
Hakuna mwenye dalili, hata za kujikongoja,
Licha ilo kamili, hakika yenye daraja,
Ya kuonwa dudu hili, kwa maonzi ya kiuja,

Bali kwa dhana kutaja mazimwi viumbe gani.

Kaditama shairi, lenye kina cha jaja,
Mtunzi ndimi Amiri, niliyevikwa makoja,
Medali za majohari, kwa tungo zenye faraja,
Kwa taswira imetaja, Mazimwi viumbe gani.

Mara baada ya majibizano haya ya Mazimwi
Kuisha, malenga Amir Andanenga akaja na mengine
mpya. Akamchokoza Ghora Haji Ghora akitaka apewe
ufafanuzi wa nni vimbanga na ili kuelewa hoja yake
aliandika shhairi kama hivi:

Haji Ghora nahodisha, Anandenga muwa shingo
Nijile kwa kukupasha, kwamba umeziba pengo
Ya Mazimwi yamekwisha, jadili ya vimbwenga
Visanamu vya udongo, au viumbe halisi,

Kabla kuendeleza, mahiri wangu utungo,
Kwanza ninakupongeza, kwa kufikia kiwango,
Mazimwi ukichunguza Makhuluku wa uongo,
Kusitawisha mitengo, hauanza Zimwi halisi.

Niilianziya Unguja, kafika Mwanarumango,
Kuwasaka hao waja, weye shepu ya mafungo,
Kila unapowataja, hugeuziwa migongo
Kusitawisha mitengo, hakuza Zimwi halisi

Ya Mizimwi kudhahili, tulipo penye ukingo.
Tuyaachilie mbali, kwa hayana mpango,
Ya Vimbwengo tujadili, nakutolea michango,
Visanamu vya udongo, au viumbe halisi.

Kuna nyingi simulizi, kuhusu hao vimwengo,
Wa mashairi na tenzi, huronga hayo marongo,
Bali zao simulizi, zinavuruga ubongo,
Visanamu vya udongo, au viumbe halisi,

Husikia ni vifupi ya Mbilikimo wa Kongo,
Na wala haviogopi, hata mawe na vigongo,
Viliko sijui wapi, najoneya songo mbingo
Visanamu vya udongo, au viumbe halisi,

Kaka sauti ya kiza, mwambao chetu kijengo,
Mtiriri nauliza, nijibu pasi kinyongo,
Usije nifidikiza, kunifitunika kwa ungo,
Visanamu vya udongo, au viumbe halisi,
Kaka sauti ya kiza, mwambao chetu kijengo
Mtiriri nauliza, nijibu pasi kinyongo,
Usije nifidikiza, kunifunika kwa ungo,
Visanamu vya udongo, au viumbe halisi,
Hapo ndipo Haji Ghora alipotabaruku na kujibu suala la
Andanenga kwa tungo yake aliyoita, Wa kucheka na
kulia.
Aliandika:
Wa kucheka na kulia, wote hupiga kelele,
Na kwenda na kukimbia, dhamira ni ileile,

Kimbwengo na Zimwi pia, ama yao maumbile
Maumbile yale yale, ya Mazimwi na Vimbengo.

Mazimwi na Vimbengo, ni mamoja maumbile,
Ya michoro ya uongo, naomba nikujuzile,
Usiharibu ubongo, la kweli usidhanile,
Ni mamoja maumbile, ya Mazimwi na Vimbengo.

Hako aliyewaona, si leo tokea kale,
Huonekana kwa dahana si kwa mboni aonile,
Hako aliyemuona, kwa nyuma au kwa mbele,
Ni mamoja maumbile, ya Mazimwi na Vimbwengo.
Michoro ni tofauti, kwa dhana si kwa ubale,
Kimbwengo ni vibutushi na Zimwi rudana tele

Alowaona hupati, ni hofu iwazingile,
Ni mamoja maumbile, ya Mazimwi na Vimbengo
Yasemwa Zimwi juani, samaki huchomwa kule,
Kimwengo meli mwendoni, hupindua kwa kidole,

Haya yote ya kudhani, hayana ukweli ule,
Ni mamoja maumbille, ya Mazimwi na Vimbengo.
Kaditama Haji Ghora, heri ya nyimno za kale,
Zinaleta itijara, kwa wana kubembezile,
Zimwi, Kimbengo si bara, na pwani hawapo kule,
Ni mimi mzungupule, mtatua mazingile

Baadaye akiandika beti zake saba kumaliza majadiliano
hayo.
Aliandika:

Malenga wa Kinondoni, Ghora Haji nikujile,
Nijile kwako mwendani, kuyakariri hayale,
Nakutaka uamini, viwengo pwani vitele,
Kama hawaji utamgule, miyongoni wa majini

Maneno waliyonena, wahenga hata wavyele,
Kwa hili shaka hapana, Amiri usikatale
Kwa wengine huviona, vyenenda huku na kule

Haka hawiji utambule, miyongoni mwa Majini.

Wazungu na Mabanyani, nawashwa kimaumbile,
Rangi achiya mbali ni, bali yao moja kole,
Kadhalika na Majini, mfano ni ule ule,
Kama hawiji utambule, miyongoni wa Majini, ya msitari
wa mbele,

Kuna Majini ruhani, nataja unisikie,
Hayo kwa kutenda dini, ya msitari wa mbele,
Ambao masubiyani, kwa watu huleta ndwele,
Kama hawiji utambue, miyongoni mwa Majini.

Viwako vinyamkera, vya madogori pungule,
Si viumbe vya kuchora, ya hivyo usizanile,
Kaumba mweneye kudura, nanena kwa makelele,
Kama hawiji utambue, miyongoni mwa Majini.
Yote yao makabila, hitaka nikutajile,
Sisozi kwenye nakala, bora nikubakishile,

Machache tayaola, itakuwa yatoshele,
Kama hawiji utambule, miyongoni mwa Majini.

Wanazo daraja zao, pamoja na vipengele,
Pia kwa tawala zao, na ambao watawale,
Kuna vimbwengo ni ndio, sawa na viganakale,
Kama hwiji utambule, miyongoni mwa Majini.
Mwisho