http://www.swahilihub.com/image/view/-/4928738/medRes/2195106/-/we8jao/-/mbogho.jpg

 

Ma-Dc watumie taasisi husika kuchukua hatua

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho 

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  10:14

Kwa Muhtasari

Wakuu wa wilaya na mikoa wanapaswa kusimamia majukumu yao kwa kufuata utawala bora

 

Suala la wakuu wa wilaya (ma-DC) kuweka mahabusu watu kwa saa 24 limeendelea licha ya kupigiwa kelele na watendaji kadhaa wa Serikali mkoani Kilimanjaro wameonja chungu hiyo wakituhumiwa na ma-DC kufanya makosa tofauti katika maeneo yao.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho aliwaweka mahabusu vigogo wawili wa halmashauri na Alhamisi iliyopita mwenzake wa Hai, Lengai Ole Sabaya alifanya hivyo kwa watendaji watano waandamizi wa kampuni ya uendeshaji wa Uwanja wa Ndege Kilimanjaro (Kadco).

Juzi, DC Mbogho aliamuru kuwekwa mahabusu kwa saa 24 mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga (DED), Zefrin Lubuva na mtendaji wa mji mdogo wa Mwanga, Justice Valentino.

Mbogho alisema amewasilisha kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), tuhuma dhidi ya watendaji hao akisisitiza kuwa sababu za kuwaweka mahabusu wawili hao hawezi kuzitaja kwa kuwa vyombo vya uchunguzi tayari viko kazini.

Kwa upande wake, Sabaya aliamuru kuwekwa mahabusu kwa vigogo watano wa Kadco inayosimamia uwanja huo wakiwamo wakurugenzi wawili na wasaidizi wao watatu Alhamis iliyopita. Alipoulizwa sababu za kufanya hivyo, alidai kuwa wanahusika na tuhuma mbalimbali za wizi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Tunajua kwamba wakuu wa wilaya wamekuwa wakitumia sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa ya 1997 kifungu cha 15(1-9) kuwaweka mahabusu viongozi wa kisiasa, watumishi wa umma na watu wengine wanapohisi kutenda makosa ya jinai.

Katika kifungu cha pili, sheria hiyo inasema pale ambapo DC ana sababu za kuamini kuwa kuna mtu anavunja amani au kuvuruga mshikamano wa wananchi, atamuagiza ofisa wa polisi kumweka mtu huyo mahabusu.

Wakati sheria hiyo ikiwapa madaraka hayo, wakuu wa wilaya na mikoa wamekwishaonywa mara kadhaa na viongozi wao, kuacha kuwaweka watu mahabusu ovyo, isipokuwa wanapaswa kusimamia majukumu yao kwa kufuata utawala bora. Mawaziri George Mkuchika (Utumishi na Utawala Bora), Selemani Jafo (Tamisemi), Ummy Mwalimu (Afya) na hata aliyekuwa Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene na katibu mkuu (Tamisemi) mstaafu, Mussa Iyombe waliwahi kuonya juu ya uwekaji watu mahabusu mara kwa mara.

Tulidhani kwamba kwa kuzingatia kauli za viongozi hao, Mbogho na Sabaya wangeviagiza vyombo hivyo kuwachunguza wahusika ili vyenyewe vikiona kwamba watuhumiwa wana makosa, viwafikishe kwenye mahakamani kwa mujibu wa sheria badala ya kutumia madaraka yao kuamuru wawekwe ndani. Je, wahusika wakionekana hawana hatia ilhali wakuu hao wa wilaya walishawatuhumu itakuwaje.

Hatupingi kazi nzuri ya kufichua utendaji mbovu au ubadhirifu unaofanywa na waliopewa dhamana katika maeneo mbalimbali zikiwamo wilaya na mikoa, lakini bado tunasisitiza kwamba hiyo si tiketi ya kuwahukumu watuhumiwa kwa kuweka ndani pasi na kufuata misingi ya kisheria.

Wakuu wa wilaya na mikoa wanavyo vyombo na taasisi za uchunguzi wa masuala mbalimbali chini yao. Rai yetu kwao ni kwamba wanapobaini kasoro yoyote ya kiutendaji, wavitumie badala ya kuchukua kwanza hatua ndipo waviagize.