http://www.swahilihub.com/image/view/-/5061810/medRes/2306231/-/yrtu9jz/-/seif+pic.jpg

 

Maalim Seif anaongezewa sifa kwa bei nafuu

Na  Bakari Kiango

Imepakiwa - Monday, April 8  2019 at  12:45

 

Mwalimu Nyerere katika ubora wake wa kufikiri tofauti mwaka 1995, alipoona Polisi wana jazba kubwa na umaarufu wa ghafla wa Mzee Lyatonga akatoa neno jepesi kuzuia umaarufu huo kusambaa zaidi. Wakati ule wananchi walikuwa wanambeba Mzee Lyatonga kila anapomaliza kuhutubia. Polisi wakawa wanachukia, wakawa wanawatawanya watu kwa mabomu.

Mwalimu na kile kifimbo chake siku moja akasema “waacheni tu, hata jeneza linabebwa”. Kweli kuanzia hapo Polisi wakaacha kuwatawanya watu wanaombeba Lyatonga. Wakambeba, wakamtua, wakambeba, wakamtua, wakamchoka wakamuacha. Sasa yupo kwake pale Sinza.

Ndicho ambacho wenye dola wanapaswa kufanya kwa Maalim Seif. Kadri wanavyokataza asiende redioni kuongea au asikutane na vigogo wenzake katika mikutano ya ndani nadhani wanamuongezea umaarufu. Wangemuacha tu.

Seif ataongea lipi jipya? Atasema CUF yake imehujumiwa na Serikali ndio maana ameenda ACT. Atasema ACT itakuwa tishio. Atasisitiza kwamba watu wake wote wamfuate ACT. Kuna jambo gani jipya hapo? Kabla hata hajasisitiza wote tunajua kwamba kuna waaminifu wa Seif na waaminifu wa Profesa. Hakuna unachoweza kuwabadili. Kudhulumiwa urais? Hilo amelisema mara ngapi?

Sasa kadri unavyomzuia Seif ndivyo anavyopata umaarufu. Watu wanaanza kuvutika zaidi “Seif anataka kusema nini jamani?” Wengine wataanza kumpa sifa “Si unaona wanamzuia Seif ni kiboko yao!”.

Kitu kikubwa zaidi ni kwamba kurasa zote za mbele zitakuwa ni Seif, Seif, Seif. Nyingine zitakuwa ni ACT, ACT, ACT. Kufikia hapo Zitto Kabwe atakuwa anacheka kimoyomoyo tu. Waliosoma huwa wanasema Seif na ACT wanapata ‘mileage’.

Achilia mbali hilo la Mwalimu na Lyatonga, lakini tukumbuke jinsi ambavyo Mzee Ben alivyowahi kuwapa umaarufu CUF kwa kuzuia maandamano yao kila siku. Yaliporuhusiwa yakapoteza umaarufu. Huwezi kuandamana kila siku. Waandamanaji wanachoka.

Huu mtego ambao wakubwa wanauingia hauna maana. Hata sisi ambao hatujasoma huwa tunatafakari sababu za jeshi la Polisi kuwazuia ACT kufanya mikutano yao ya ndani. Kwamba CUF watakuja kuleta fujo. Kazi ya polisi ni kuzuia fujo, pia ikiwa hivyo msajili siitabidi aifute CUF kwa kufanya vurugu? Siasa bwana!